KIFO CHA MTU ASIYE NA HATIA - 02
Wakati bado akijiuliza maswali kichwani mwake alitokea rafiki yake mkubwa aliyeitwa Kategile na kusimama mbele yake.
“Pole sana Prosper bahati mbaya umechelewa mazishi!”
“Ya nani?” Aliuliza kwa mshangao Prosper.
“Baba yako!”
“Baba?”
“Ndiyo!”
“Baba kafariki lini?”
“Wiki iliyopita!”
Prosper alianza kulia na majirani wengine zaidi walifika na kuanza kumpa pole, walishangaa kuwa hakuwa na taarifa hizo!”
“Sasa mama na ndugu zangu wapo wapi?”
“Wapo kituo cha polisi kati mjini Tabora”
“Wamefanya nini?”
“Ni wao ndio walimpiga baba yako na kumuua!”
Siku iliyofuata asubuhi Prosper alikwenda moja kwa moja kituo cha polisi kati kuwaona ndugu zake pamoja na mama yake, alilia machozi alipomwona mama yake akiwa mahabusu, aliomba kuongea naye akaruhusiwa na wakapewa chumba yeye na mama yake pamoja na dada zake waongee.
“Mama kweli mlimuua baba?”
“Mwanangu nililazimika kufanya hivyo kwani alichukua kisu na kunikata sikio langu la pili…..”Mama yake Prosper alianza kulia.
“Alilitoa?”
“Halipo mwanangu, nimepoteza masikini yangu yote mawili baba yako alikuwa katili mno alistahili kufa na ninakiri nimemuua!”
“Ulimuua na nini?”
“Nilimpiga na mchi kichwani akaanguka na kufa! Huo ndio ukweli mwanangu!”
“Mama ulishindwa kweli kufuata ushauri wangu?”
“Nisamehe mwanangu!”
“Mama hautafia gerezani ni heri nifungwe mimi na kunyongwa lakini wewe uwe huru nakupenda mno mama!” Alisema Prosper huku akilia.
Baada ya maongezi Prosper alirejea mjini ambako alikwenda moja kwa moja kituo cha polisi kati mjini Tabora.
“Naomba kuonana na mkuu wa kituo!”
“Wewe nani na una shida gani?”
“Nina maongezi marefu kidogo siwezi kukueleza wewe!”
Alionyeshwa ofisi ya mkuu wa kituo na kuingia.
“Shikamoo mzee!”
“Marahaba nikusaidie nini kijana!”
“Mzee unakumbuka mzee Kabaka aliyeuawa siku chache zilizopita?”
“Ndiyo si yule aliyeuawa na mke wake?”
“Ndiyo! Yule ni baba yangu na aliyemuua si mama yangu ni mimi! Nilitoroka baada ya kitendo hicho na ninakueleza wazi kuwa nimerudi ili mama yangu aachiwe mimi ndiye niwekwe rumande!”
“Kweli?”
“Huo ndio ukweli ni mimi niliyempiga baba na mchi kichwani akafa!”
“Kwanini?”
“Kwa sababu alikuwa anamtesa mama yetu!”
“Mungu wangu!Afande Charles!”
“Naam Afande!”
“Hebu njoo hapa mara moja!”
Sekunde tano tu tayari askari alisimama mbele ya meza ya mkuu wa kituo.
“Ndiyo afande!”
“Mchukue huyu kijana umpeleke rumande, kumbe ndiye aliyemuua baba yake kule Tutuo na sisi tukawakamata mama yake na dada zake sasa amejileta mwenyewe! Peleka mahabusu haraka na mama yake na dada zake waachiwe mara moja?”
“Sawa afande!”
Askari alimnyanyua Prosper na kumzaba vibao kadhaa usoni, kisha akamchukua na kupelekwa chumba cha mahabusu, muda mfupi baadaye alishuhudia mama yake na dada zake wakitoka mahabusu wakati wanatoka kituoni walisikia sauti ya Prosper ikiita kutoka mahabusu.
“Mama!Mama! Acha mimi nife huku lakini wewe uwe huru baba alikutesa mno na ulikuwa na haki ya ku....!”
“Masikini mwanangu, umefanya nini tena?” Aliuliza mama yake Prosper huku akilia.
Hakuna mtu aliyekuwa tayari kuamini yaliyotokea yalikuwa kweli , Prosper alikuwa ameyatoa maisha yake kwa ajili ya mama yake! Ulikuwa ni upendo mkubwa mno kwa binadamu kuonyesha, wengi waliamini ni Yesu peke yake aliyeweza kulifanya hilo, Prosper alikuwa ameudhihirishia ulimwengu kuwa hata binadamu anaweza kuutoa uhai wake kwa ajili ya mwenzake.
“Namhurumia sana Prosper sikupenda ajiingize katika suala hili ni heri ningenyongwa kwa sababu ndiyo niliyemuua baba yenu! Nitafanya nini mimi Ili Prosper atoke mahabusu?” Alihoji mama Angelina huku akilia.
Alilia usiku na mchana kwa siku tatu na hakula chakula kabisa zaidi ya maji katika siku zote hizo, Nyamizi na Kasanda walimbembeleza mama yao lakini hakukubali, alikonda na kupoteza uzito mwingi sana mwilini mwake, sababu ya kumlilia Prosper.
*********************
Mahabusu:
Prosper alikuwa amekaa ndani ya chumba kidogo cha mahabusu mjini Tabora, kilichotoa harufu kali na mbaya ya mikojo! Tangu aingie ndani ya mahabusu hiyo siku mbili kabla alikuwa hajaongea na mtu yeyote kati ya watu wote waliokuwemo. Alikaa peke yake kwenye moja ya kona za mahabusu hiyo akiwa na mawazo mengi kichwani mwake.
“Acha nife mimi si mama yangu!” Aliongea kwa sauti kubwa Prosper na mzee aliyekuwa karibu yake aligutuka na kumgeukia.
“Kijana mbona unaongea peke yako?”
“Mh! Hapana mzee! Unajua? Mimi!......” Prosper aliongea maneno mengi yaliyochanganyika ambayo hayakutoa jibu la moja kwa moja kwa swali aliloulizwa!
“Niambie kijana ni kitu gani kimekufanya uje hapa mahabusu?”
“Shikamoo mzee!” Prosper aliamkia.
“Marahaba, hebusasa nieleze tatizo lililokufanya uje humu!”
“NIMEUA!”
“Umeua? Watu wangapi?”
“Mtu mmoja tena ni baba yangu!”
“Kha! Hilo ndilo linakufanya ulie? Mbona mimi nimeua watu hamsini na mbili na nimetulia tu!”
“Watu hamsini! Umewanyonga?”
“Hapana, nilizamisha mtumbwi tuliokuwa tukisafiria na watu wote wakafa mimi tu nikaokoka!”
“Kwanini ulifanya hivyo?”
“Nilitaka kuiba pesa zao, wote walikuwa ni wafanyabiashara wakitokea Burundi kuja Kigoma, baada ya mtumbwi kuzama nilichukua mifuko yao ya pesa na kuogelea nayo hadi ufukweni ambako nilikodisha gari likanileta hadi hapa Tabora lakini nilipoingia tu mjini nikakamatwa na ninajua nitahukumiwa kunyongwa lakini bado silii sasa wewe unalia kitu gani na umeua mtu mmoja tu? Nyamaza bwana usitupigie kelele usikigeuze chumba hiki kliniki, humu wanakaa wanaume bwana!”
“Sawa mzee!”
“Una miaka mingapi kijana?”
“Nina miaka 19!”
“Unaitwa nani?”
“Ninaitwa Prosper! Wewe unaitwa nani?”
“Ninaitwa Savimbi, ulimuuaje baba yako?”
“Nilimpiga na mtwangio kichwani!”
“Kwanini?”
“Sababu alikuwa akimtesa sana mama yangu!”
“Unasoma?”
“Ndiyo!”
“Shule gani?”
“St Magreth huko Moshi nipo kidato cha tano!”
“Sasa hivi shule tena basi! Maisha yako yatakuwa ya gerezani ambako kuna mateso makubwa sana lakini kwa sababu unakwenda na mimi usiwe na wasiwasi nitakusidia, utakula chakula kizuri, utalala mahali pazuri, unavuta sigara?”
“Hapana!”
“Bangi?”
“Hapana!”
“Sawa, lakini kila kitu nitakupatia, utakuwa lakini unalala karibu na mimi sawa?”
“Sawa nitashukuru sana!”
“Umeshaota ndevu?” Jambazi alimuuliza.
“ Zimeanza kuota kidogokidogo!”
“Aisee hebu nione!” Jambazi ali anza kumpapasa Prosper kidevu, ilikuwa kizani hakuna mtu aliyeona kitendo hicho kikiendelea.
“Mzee unafanya kitu gani hicho?”
Ghafla mlango wa mahabusu ulifunguliwa na majina ya watu kadha yakaanza kutajwa, waliosikia majina yao walitoka mmoja baada ya mwingine hadi nje ambako walikuta maaskari wawili wenye bunduki wakiwasubiri na kuwalinda.
“Haya wa mwisho ni Savimbi Mfugambwa,hebu toka nje upesi muuaji mkubwa wee!”
Prosper alipolisikia jina la Mfugambwa alielewa ni nani aliyekuwa amekaa naye mahabusu! Halikuwa jina geni kabisa kwake masikioni kwake, alishalisikia jina hilo mara nyingi tu tangu akiwa mtoto mdogo, Mfugambwa alikuwa jambazi aliyejulikana sana mikoa ya Tabora,Mwanza, Shinyanga na Kigoma ni yeye aliyeteka mabasi na treni za abiria na kuwanyanganya mali zao!
Alidaiwa kuwa na madawa yaliyomsaidia kushinda kesi aliyoyapata kutoka nchini Zaire, alishakamatwa mara nyingi kwa makosa hayo lakini alishinda kesi zote kiajabu ajabu na kuwa huru. Sekunde chache baadaye Prosper alisikia jina lake likitajwa na kutembea hadi mlangoni ambako alifungwa pingu mikononi na mlango wa mahabusu ukafungwa.
“Tangulieni nje nyie wauaji”
“Kwani kuua ni kitu cha ajabu bwana, usitunyanyase!” Savimbi alimjibu askari bila woga kwa jibu hilo alipokea kipigo cha kitako cha bunduki na kupasuka usoni,damu zikamtoka lakini bado hakuacha kutoa matusi.
Walipandishwa ndani ya gari la polisi na ulinzi mkali wa msafara wa magari kama matano hivi uliongoza safari kwenda mahakamani. Mahakamani waliteremshwa na kuanza kusukumwa kuelekezwa katika mahabusu iliyokuwepo nje ya mahakama, Prosper alipotupa macho pembeni alimwona mama yake akilia, machozi huku akiwa ameshikiliwa na dada zake.
Alionekana akijaribu kujitoa mikononi mwao ili asogee mbele lakini alishindwa, mdomo wake ulifunikwa na viganja vya binti zake ili maneno aliyokuwa akiyatoa yasisikike, lakini bado Prospe alisikia kilichosemwa na mama yake!
“Niachieni! Niende kwa mwanangu nikawaeleze polisi ukweli ili wamwachie”
Prosper aliposikia maneno hayo alimkonyeza mama yake lakini bado aliendelea kupiga kelele, jambo lililofanya dada zake waamue kumwondoa mahakamani haraka iwezekanavyo.
Prosper na Savimbi walisomewa mashtaka yao tofauti na kurudishwa mahabusu, hawakutakiwa kujibu kitu chochote sababu kesi zao zilikuwa za mauaji.
****************
Walipotoka mahakamani hawakurudishwa tena polisi bali walipelekwa moja kwa moja gereza la Isanga ambako waliwekwa mahabusu, huo ndio ukawa mwanzo wa Prosper kuishi gerezani na kila mwezi alipelekwa mahakamani ambako kesi yake ilitajwa tu!
Kila siku iliyokwenda kwa Mungu Prosper alikuwa na mawazo mengi juu ya maisha yake, lakini mawazo yaliyomsumbua zaidi ni juu ya msichana Belinda, alikaa na Belinda kwa muda mfupi shuleni na kumzoea na ni wazi alimpenda, kila alipoikumbuka siku waliyoachana shuleni baada ya Belinda kumpa nauli za kumpeleka likizo, roho ilimuuma sana Prosper!
Alikuwa na mapenzi makubwa sana kwa msichana huyo na aliamini hata yeye alimpenda na alimkubali pamoja na umasiki aliokuwa nao! Alishindwa kuelewa Belinda angepata vipi taarifa juu ya matatizo yaliyomkuta, kumbukumbu juu ya Belinda zilimtia simanzi zaidi.
********************
Belinda Dar es Salaam, Julai:
Siku chache kabla ya shule kufunguliwa kwa pesa aliyopewa na baba yake Belinda alimnunulia Prosper zawadi mbalimbali zikiwemo nguo, viatu na hata vitabu vizuri kwa ajili ya masomo yao.
“Prosper atafurahi sana kupokea zawadi hizi na ndio ataamini kuwa kweli ninampenda!” Aliwaza Belinda wakati akipakia mabegi yake katika gari tayari kwa kuondoka kwenda shule.
Belinda alikuwa na hamu kubwa ya kukutana na Prosper na aliona gari halifiki Moshi, alipofika shuleni hakumkuta na alikaa kwa mwezi mzima shule bila kumwona alianza kupata wasiwasi mkubwa moyoni mwake, alihisi pengine alikuwa amekosa pesa ya ada! Aliamua kumwandikia barua haraka na kumwomba aje shule na kama tatizo lilikuwa ada basi yeye angemlipia.
Kwa miezi miwili mfululizo haikujibiwa akaamua kuandika tena barua nyingine, lakini nayo pia haikupata majibu, Belinda akazidi kuchanganyikiwa hakuelewa ni kitu gani kilimpata Prosper!
Maisha ya shuleni yalikuwa magumu sana bila Prosper ! Kila siku alilia akiomba Prosper aje tena shule waendelee na maisha yao lakini haikuwa hivyo kwani hadi mwisho wa muhula Prosper alikuwa bado hajaripoti shuleni.
****************
Miaka mitatu baadaye:
Belinda alisoma kwa mateso bila kumwona Prosper tena, roho yake ilimuuma kila siku na mpaka anamaliza kidato cha sita alikuwa ni mtu wa kumlilia Prosper tu! Wanafunzi wenzake walimcheka, alipomaliza kidato cha sita alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa masomo ya sheria, mawazo yake yalikuwab bado kwa Prosper!
Likizo yake ya kwanza aliamua kusafiri bila kuwataarifu wazazi wake kwenda Tabora, Belinda alidandia treni lililompeleka hadi Tabora mjini ambako alipanda tena basi la Sabena lililokwenda hadi Mbeya, basi hilo lilimshusha kijijini kwao na Prosper Tutuo kilometa kama thelathini kutoka Tabora mjini.
Aliingia Tutuo saa saba mchana na kuulizia nyumbani kwa akina Prosper akaonyeshwa, kila mtu kijijini alimshangaa kwa mavazi aliyovaa! Alishangazwa na hali aliyoikuta nyumbani kwao na Prosper ilikuwa ni nyumba ndogo mno iliyokandikwa kwa udongo na ilianguka upande mmoja. Alipobisha hodi alipokelewa na mama mmoja aliyevaa nguo zilizochanika na alionekana kuwa mgonjwa alikohoa kila baada ya kuongea sentensi moja! Mama huyo alifanana sana na Prosper.
“Karibu binti!” Alisema mama huyo na kumpokea Belinda begi lake na mmoja wa wasichana alilipeleka ndani, akavuta kigoda kilichokuwa karibu na kumpa Belinda akikalie, ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Belinda aliyezaliwa katika familia ya kitajiri kuwa katika familia ya aina ile na alielewa ni kwanini Prosper aliishi maisha duni shuleni.
Baada ya salamu Belinda hakusita kueleza sababu ya safari yake! Wasichana wawili waliovaa magauni yaliyochakaa walikaa pembeni ya mwanamke huyo wakisikiliza.
“Mama mimi naitwa Belinda!”
“Wewe ndiye Belinda? Uliyeandika barua hapa miaka miwili na nusu iliyopita?” Uliyekuwa ukisoma na prosper Moshi?” Angelina mama yake Prosper alilipokea jina la Belinda kwa mshangao.
“Ndiyo mama na madhumuni ya safari yangu ni kujua aliko Prosper kwa sasa, sababu ni miaka miwili na nusu sijamwona! Roho inaniuma sana kumpoteza kwani ninampenda!”
Badala ya kujibu ombi la Belinda mama yake Prosper aliangua kilio na hata wasichana waliokaa karibu yake nao walianza kulia machozi. Belinda alishindwa kujizuia na kujikuta nae akilia ingawa hakujua sababu ya wao kulia ilikuwa ni ipi!
“Niambieni basi ili nifahamu Prosper yupo wapi hasa?”
“Yupo gerezani!”
“Alifanya nini Prosper?”
“Alimuua baba yake!” Mama yake Prosper alishindwa kuueleza ukweli!
Belinda alianguka chini na kuanza kugalagala akilia kwa uchungu walijaribu kumbembeleza lakini hakusikia, alipotulia swali lake lilikuwa moja tu!
“Ni kwanini alimuua baba yake masikini Prosper?”
“Unaniona mimi nilivyo mwanangu?”
“Ndiyo!”
“Sikuzaliwa hivi unavyoniona yote hii ni kazi ya baba yake prosper, alinitesa sana kwa kunipiga kila siku na kunitoa viungo vyangu kwa kisu, Prosper alimuua baba yake kwa bahati mbaya akijaribu kunisidia mimi!” Alisema mama huku pia akilia machozi.
“Nahitaji kumwona Prosper mama hata huko gerezani mnipeleke!” Alisema Belinda.
“Prosper yupo gereza la Isanga lakini siku ya kumwona ni Jumapili pekee!”
Jumapili ilikuwa siku sita mbele yao, Belinda hakuwa na njia nyingine kumwona Prosper zaidi ya kusubiri mpaka siku hiyo ifike! Maisha yalikuwa magumu sana kwake kuendelea kusubiri lakini hakuwa na la kufanya aliishi nyumbani kwao Prosper akifanya kazi zote za nyumbani na alitumia pesa alizokuwa nazo kutatua baadhi ya matatizo katika familia hiyo.
Ni yeye alimpeleka mama yake Prosper hospitali ya Kitete mjini Tabora kupimwa, daktari aliamua kumpima makohozi, baada ya kuhisi alikuwa na kifua kikuu na alipigwa X-ray ya kifua na kuonekana mapafu yake yalikuwa yameharibika kabisa.
Makohozi yake yalipopimwa kwa muda wa siku tatu yaligungulika kuwa na wadudu wa kifua kikuu na kuanzishiwa matibabu!Angelina alimshukuru Belinda kupita kiasi.
Siku ya Jumapili ilipofika wote waliondoka kwenda gerezani Isanga, moyo wa Belinda ulikuwa ukidunda kwa nguvu na hakujua nini kingetokea baada ya kukutana na Prosper alishindwa kupata picha halisi ya Prosper kwa wakati huo lakini aliamini bado alikuwa ni kijana mwenye sura nzuri kama alivyokuwa awali. Walipofika gerezani waliandikisha majini yao na watu waliotaka kuwatembelea, taratibu zote hizo kwa Belinda zilikuwa ni kumchelewesha kumwona Prosper! Baada ya kujiandikisha walionyeshwa chumba maalum cha kumsubiri Prosper aje na kuongea naye!
Dakika kumi baadaye wakiwa wamekaa, Belinda alishuhudia kijana mmoja mwembamba mrefu akiingia chumbani humo, urefu wake ulikuwa sawa na Prosper lakini unene wa mwili na ngozi yake vilikuwa tofauti,alijaa ukurutu mwili mzima! Aliingia chumba akiongozana na mtu mmoja mwenye mwili mkubwa na ndevu nyingi.
Kijana huyo alipotupa macho chumbani akiwaangalia watu waliokuwepo, ghafla aliruka na kukimbia moja kwa moja kuelekea mahali alipokuwa amekaa Belinda! Alipomfikia ndipo Belinda aligundua kijana huyo alikuwa Prosper lakini katika hali mbaya.
“Belinda umefikaje huku?”
“Prosper ni wewe? Umekuwaje hivi mpenzi wangu?”
Waliangushana hadi chini na kuanza kulia, Angelina pamoja na binti zake Nyamizi na Kasanda walishindwa kujizuia na kujikuta wakiangua kilio, mwanaume aliyeambatana na Prosper alikwenda na kumvuta Prosper na kumtoa mikononi mwa Belinda.
“Ha! Hebu achianeni!” Alisema mwanaume huyo ambaye baadaye Belinda alimtambua kwa jina la Savimbi.
“Kwanini?” Prosper aliuliza.
“Kwani huyu msichana ni nani?”
“Huyu ni mpenzi wangu!”
“Nani amekuambia unatakiwa uwe na mpenzi?”
“Savimbi mimi sitakii,niachie bwana niongee na Belinda wangu!”
Sura ya Savimbi ilibadilika na ghafla bila hata kuuliza alimnyanyua Prosper na kuanza kumvuta kumrudisha ndani ya gereza, Belinda alilia na kushindwa kabisa kuelewa kilichokuwepo kati ya Savimbi na Prosper wote walibaki wameangaliana bila kujua la kufanya!
Belinda hakuamini alichokiona alishangaa ni kwanini mwanaume huyo amchukue Prosper kabla hajamaliza kiu ya maongezi naye, alifikiria sana na kujikuta akilia.
Alishindwa kuelewa ni kitu gani kiliendelea kati ya Prosper na mwanaume aliyemchukua kwa nguvu ukumbini na Prosper alionekana kutokuwa na sauti kabisa mbele ya mwanaume huyo.
Kichwa cha Belinda kilihisi kitu fulani lakini hakuwa na uhakika nacho sana na alishindwa kupitisha moja kwa moja kuwa kulikuwa na uhusiano wa kishoga kati ya Prosper na mwanaume huyo!
“Haiwezekani Prosper ninavyomfahamu hawezi kufanya hivyo!” Aliwaza Belinda!
Hapakuwa na sababu ya wao kuendelea kubaki gerezani siku hiyo, walilazimika kuondoka kwenda hadi stendi ambako walipanda basi na kurudi tena kijijini Tutuo!
Njiani Belinda aliwaza mambo mengi sana juu ya kifo cha baba yake Prosper na alishindwa kuelewa ilikuwaje mpaka Prosper akafikia uamuzi huo wa kikatili, mama yake Prosper ilibidi aeleze kila kitu kuhusu ukatili aliofanyiwa na mumewe na hatua aliyoichukua prosper kumkingia mama yake.
“kwanini hamkwenda mahakamani mama?”
“Mwanamke wa Kinyamwezi hatakiwi kumshtaki mume wake hata kama akipigwa mwanangu!”
“Hivi mama yule mwanaume aliyekuja na Prosper pale gerezani ni nani?”
“Ni rafiki mkubwa wa Prosper anaitwa Savimbi kila mara tukienda gerezani huwa anakuja naye!”
“Mh! Mbona jina lake linatisha?”
“Hivyo ndivyo anavyoitwa!”
Walifika kijijini saa tisa mchana na Belinda aliendelea kuishi kijijini kwa wiki nyingine zaidi akisubiri Jumapili ifike ili aende gerezani kumwona tena Prosper, siku ilipofika walikwenda tena gerezani siku hiyo mama yake Prosper hakwenda kwa sababu hali yake haikuwa nzuri kifua kilimbana sana na alikuwa ameshindwa hata kuhema.
Walikwenda Belinda na dada zake Prosper peke yao na walifanikiwa kuonana na Prosper lakini siku hiyo alikuja peke yake bila Savimbi na kusalimiana nao, dada zake walionekana kushangaa.
“Leo Savimbi yupo wapi?” Nyamizi alimuuliza Prosper.
“Alipigana na Mnyapara jana!”
“Kwanini?”
“Kwa sababu Mnyapara alinipa ugali mkubwa na mboga yenye mafuta!”
“Ndio wakapigana?”
“Ndiyo!”
Belinda alizidi kuyaamini mawazo yake, ilikuwa si rahisi watu wapigane sababu ya Prosper kupewa ugali!Roho ya Belinda iliumia sana na kujikuta akilia alitaka kusema kitu lakini alishindwa sababu dada zake walikuwa pale.
“Wifi zangu mnaweza kunipa nafasi kidogo tu niongee na kaka yenu faragha?”
“hakuna shida wifi!” Walijibu na wote wakatoka nje wakiwaacha prosper na Belinda peke yao chumbani, kilikuwa ni chumba chenye mwanga mdogo.
“Prosper pamoja na matatizo yote yaliyokupata bado nakupenda!”
“Hata mimi nakupenda pia Belinda na sasa ninaamini hunidanganyi penzi lako kwangu ni kweli tupu ingawa nasikitika kuwa nitafia gerezani,bila hivyo tungeoana na kuzaa watoto wetu Belinda!”
“Usiwe na wasiwasi Prosper bado nina uhakika tutaoana!”
“Tutaoanaje wakati mimi tayari nilishahukumiwa kunyongwa?”
“Usijali muujiza wa Mungu utatokea na nikirudi nyumbani nitamshawishi baba yangu anipe pesa ili nikutafutie wakili ajaribu kukutoa gerezani!”
“Baba yako atakubali kweli?”
“Nina uhakika baba atakubali wala usiwe na wasiwasi mpenzi!”
Wote wawili waliangaliana na kujikuta wakitokwa na machozi ya uchungu! Kumbukumbu kubwa sana juu ya maisha yao ilikuja vichwani mwao, mambo mengi waliyoyafanya shuleni na kufurahia maisha yalirejea akilini mwao, Belinda alihisi mapenzi makali sana yakiutwaa tena moyoni mwake! Kweli alimpenda Prosper kuliko kitu kingine chochote, ni wanaume wengi walishamfuata kumtaka mapenzi lakini hakuwakubali moyo wake ulimpenda Prosper kijana masikini tena aliyekuwa gerezani wakati huo.
Kitu kama sumaku kilijitokeza katikati yao na kujikuta wamekumbatiana na kuanza kupapasana miili yao! Kwa mara ya kwanza katika maisha yao tangu wafahamiane walijikuta wakitamaniana kimwili na mambo yaliyofuata katika muda wa dakika tano ndani ya chumba hicho hayaandikiki wala kuelezeka ila ilikuwa ni raha ambayo wote wawili waliipata kwa mara ya kwanza maishani mwao.
“Proper ahsante! Ninakupenda sana Prosper na sijui nitaishije bila wewe!” Alisema Belinda huku akilia machozi.
“Nakupenda pia Belinda na kama nilivyokueleza bila haya matatizo tungeoana na kuwa mke na mume!”
“Usiwe na wasiwasi Prosper tutaoana tu!” Belinda aliendelea kusisitiza alichokisema awali.
“Hivi sasa unasoma wapi?’
“Mimi?”
“Ndiyo!”
“Baada ya kumaliza kidato cha sita nilijiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam ambako ninasoma Sheria!”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Unataka kuwa mwanasheria Belinda?”
“Ndiyo!”
“Soma sana uje utusaidie!”
Dakika tano baadaye kengele ililia ndani ya gereza na Prosper alinyanyuka na kumkumbatia Belinda walipigana mabusu na kuagana! Mwili wa Prosper ulikuwa mchafu kupita kiasi alihisi Belinda angemwonea kinyaa lakini haikuwa hivyo, Belinda hakujali wala kuonyesha kushangazwa na hali hiyo alizidi kumkumbatia.
“Belinda ni lazima niende sasa muda wa kuongea na wewe umekwisha!”
“Sawa darling lakini jaribu kuwa mwangalifu sana na Savimbi siipendi tabia yake!”
Prosper hakujibu kitu alizidi kuinamisha kichwa chake chini kwa aibu jambo lililomfanya Belinda aendelee kupata uhakika kuwa kulikuwa na jambo kati yao!
Baada ya kuagana Belinda alitoka nje ya gereza na kuungana na wifi zake na safari ya kwenda stendi kupanda basi la kuwarudisha nyumbani ilianza, njia nzima Belinda alikuwa ni mwenye mawazo alifika akiwa amechoka na kujitupa kitandani ambako aliendelea kumlilia Prosper!
***************
Alikaa Tabora kwa wiki tatu bila wazazi wake kufahamu mahali alikokuwa, baba mzazi yake alishamtafuta kila mahali bila kumpata mpaka kukata tamaa! Alitangaza katika vyombo mbalimbali vya habari lakini bado hakufanikiwa kumpata binti yake, wengi walihisi Belinda alikufa lakini baba yake hakuliamini hilo.
Hatimaye mzee Thomson Komba baba yake Belinda aliamua kutangaza zawadi nono ya shilingi milioni kumi kwa mtu yeyote ambaye angefanikisha kupatikana kwa Belinda, wanakijiji wawili wa kijiji cha Tutuo walijitokeza na kwenda kutoa taarifa moja kwa moja kituo cha polisi Belinda akawa amekamatwa.
Siku aliyokamatwa aliiacha familia ya akina Prosper katika majonzi makubwa kwa sababu kwao mkombozi alikuwa ameondoka! Kukaa kwa Belinda katika familia hiyo kulipunguza sana shida zao za maisha, pesa yote aliyokuwa nayo aliitumia katika matumizi ya nyumbani na ni yeye pia aliyenunua dawa za mama yake Prosper.
Alichokifanya Belinda wakati wa kuondoka ni kumtupia Nyamizi dada yake Prosper shilingi elfu hamsini alizokuwa nazo katika mfuko wa suruali ili ziwasaidie.
“Wifi!Pesa hizo zitawasaidia!”
ITAENDELEA KESHO NA MAPEMA

Post a Comment