YANGA YANYOOSHA DARUBINI YAKE KATIKA KUSAKA KIUNGO MWENYE KASI YA KUKABA
Sasa
kwa kipindi kirefu Yanga haipo vizuri katika nafasi ya kiungo mkabaji,
tunaweza kusema tangu kuondoka kwa Athuman Idd ‘Chuji’ na Frank Domayo,
hajapatikana mbadala wao.
Yanga
imepiga hesabu baada ya kumtazama kiungo Kenny Ally wa Mbeya City
katika mechi mbili dhidi yao na ile dhidi ya Simba na kujiridhisha
kwamba anafaa kuwemo kwenye kikosi chao.
Msimu
uliopita Yanga ilimsajili Thabani Kamusoko kutoka FC Platinum ya
Zimbabwe ili acheza kama kiungo mkabaji, hata hivyo Kamusoko raia wa
Zimbabwe ameonekana anamudu zaidi kucheza kama kiungo mshambuliaji.
Hesabu
za Yanga wakati huu zimelala kwa Kenny ambaye katika mchezo wa Ligi Kuu
Bara dhidi ya Mbeya City, Novemba 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa
Sokoine, Mbeya, Yanga ilifungwa mabao 2-1.
Mabao
ya Mbeya City yalifungwa na Hassan Mwasapili dakika ya sita na Kenny
akafunga la pili dakika ya 39 huku Donald Ngoma akiifungia Yanga bao
pekee dakika ya 45.
Yanga
imeona Kenny anaweza kuwasaidia katika kiungo cha ukabaji na tayari
baadhi ya viongozi wake wa Kamati ya Mashindano wameanza harakati za
siri kuhakikisha wanamsajili mchezaji huyo.
Kidogo
Yanga inaweza kukumbana na ugumu kwani Kenny mkataba wake na Mbeya City
umebakisha miezi mitatu kumalizika lakini hilo halijawazuia kuzungumza
naye kutazama uwezekano wa kumsajili.
“Ni
kweli kabisa tunamtaka Ally kwani tumeona kuwa anaweza kutusaidia
katika nafasi ya kiungo mkabaji ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitutesa,
tupo katika mazungumzo naye na mambo yakienda vizuri tutamsajili,”
alisema kiongozi mmoja wa Kamati ya Usajili ya Yanga.
Pia Yanga imehusishwa na harakati za kumtaka kiungo mshambuliaji wa Mbeya City, Raphael Alpha ili kukiongezea nguvu kikosi chao.
Gazeti
hili lilipowasiliana na Kenny alisema: “Taarifa hizo na mimi nazisikia
ila kama kweli wananitaka basi wafuate tu utaratibu, tukikubaliana mimi
nipo tayari kujiunga nao.”
Katibu
Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe hakupokea simu yake lakini ofisa
habari wa timu hiyo, Dismas Ten, yeye alisema: “Taarifa hizo tunazo
mezani kwetu, tumesikia kuwa Yanga wanamtaka Kenny Ally pamoja na
Raphael Alpha, kwa upande wetu sisi hatuna tatizo ila tunawaomba wafuate
utaratibu tu wa usajili.”
Alipotafutwa
Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit ili naye aweze kulizungumzia
suala hilo alisema: “Taratibu zote za usajili ni siri ya klabu, hivyo
kama kuna mchezaji tutamsajili basi tutawajulisha.”
Post a Comment