UKISIKIA KAMBI MPYA, HAPA NDIYO CAMP NOU, NI MTAJI WA MAISHA YA BARCELONA
| SALEHJEMBE, AKIWA NJE YA UWANJA WA CAMP NOU JIJINI BARCELONA, JANA. |
Na Saleh Ally, Barcelona
UWANJA
wa Camp Nou ni mali ya Klabu ya Barcelona ambayo inamilikiwa na
wanachama lakini una miongozo kadhaa yenye utamaduni wa aina yake.
Neno
Camp Nou ni katika lugha ya wenyeji wa hapa, yaani Kihispania. Kwa
lugha yetu adhimu ya Kiswahili, neno hilo maana yake ni Kambi Mpya.
Nakukumbusha
tu kuwa ni uwanja wenye uwezo wa kuchukua watu 99,354 waliokaa vitini.
Hii inaufanya kuwa wa pili kwa ukubwa kwa maana ya kuingiza watu wengi,
duniani. Unaoongoza ni Uwanja wa Rangrado May Day wa Korea Kaskazini.
Idadi
hiyo ya kuchukua watu 99,354 inaufanya Uwanja wa Camp Nou kuwa wa
kwanza kwa ukubwa nchini Hispania na barani Ulaya kote ambako unafuatiwa
na Wembley wa England unaochukua watu 90,000.
Kweli
ni “Kambi Mpya”, lakini ni jina lililoanza mwaka 1957 tangu
walipohamia. Umeendelea kuwa mpya kutokana na marekebisho kadhaa na kama
hiyo haitoshi, uwanja huo ni mtaji mkubwa kwa Barcelona.
Wakati
nikifanya ziara kadhaa maeneo ya karibu ya uwanja huo, ndani pia,
kilichonivutia ni mpangilio na namna unavyotoa ajira kwa Wahispania
zaidi ya 150.
Watu
wanaofanya kazi hapo ni wale wanaohusika na matengenezo kwa maana ya
mafundi, wanaoutunza uwanja, watunza majani ya uwanja na wale ambao
wanakuwa katika baadhi ya ofisi za Barcelona.
Hawa
wote wanalipwa na uwanja huo kwa kuwa umeendelea kufanya kazi hata siku
ambazo si za mechi kwa kuwa watu mbalimbali wanafika kuutembelea, hivyo
kuufanya kuingiza zaidi ya euro milioni 1.5 (zaidi ya Sh bilioni 3.6)
kwa mwezi kwa shughuli za kawaida tu, nje ya mechi ambazo hutumiwa na
Barcelona.
Kwa
Barcelona, Camp Nou ni mtaji mkubwa ambao huenda Yanga na Simba
wanaweza wakajifunza mengi na kujiona wamechelewa kujenga viwanja vyao
kwa kuwa bado tunaweza kuona uwanja hauna maana ya sehemu ya kuchezea
pekee, badala yake, uwanja ni mtaji au biashara kubwa.
Klabu
ya Barcelona inautegemea kwa asilimia 61 uwanja huo ili kujipatia
matangazo zaidi, asilimia 39 iliyobaki inaweza kuwekwa sehemu nyingine,
ikiwemo kwenye jezi za klabu hiyo.
Wakati
nafika hapa, nilikuta ule mjadala wa uwekezaji wa uwanja huo umefumuka
upya, Barcelona wakiamini unaweza kuwaingizia fedha nyingi zaidi kama
watafanya kama ilivyokuwa kwa Arsenal na jina la Emirates au Man City na
Etihad kwa kuwa klabu hulipwa fedha nyingi mwekezaji kuwekeza jina lake
kwenye uwanja ambao tayari ulikuwa maarufu.
Uwekezaji
huo unaonekana kupingwa na wengi, kamwe hawataki kuona jina Camp Nou
linapotea. Wanaona ni utamaduni, sifa au kitu cha kujivunia na wanapenda
kubaki jina hilo ili wajisikie raha kufika hapo na wanachama wengi
ambao ni wamiliki wa klabu wanaona bora kuendelea kubaki na jina hilo.
Wameelezwa,
kwamba maisha yanabadilika na utaona Barcelona ilikuwa ikilipa euro
milioni 1.5 kwa Unicef ili itumie jina lake kwenye jezi zake. Ilikuwa
klabu pekee inayomlipa mdhamini halafu inamtangaza lakini baadaye mambo
yakawa magumu ikalazimika kuchukua mamilioni ya Qatar Airways ambayo ni
Shirika la Ndege la Qatar.
Sasa
suala la fedha linahitajika, mtaji mkubwa Barcelona kibiashara ni
wachezaji watatu, Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar ambao Barcelona
inaona angalau ni vizuri kukaa nao kwa miaka mitano mingine ijayo,
lakini bila fedha ndoto zao hazitatimia.
Barcelona
wanajua wapinzani wao wakubwa Real Madrid katika suala la fedha,
wamewahi kuwanunua wachezaji kadhaa nyota kama Ronaldo di Lima, Luis
Figo na wengine. Kwa sasa kumuuza mmoja kati ya Suarez, Neymar au Messi
kwenda Madrid itakuwa ni faida ya muda mfupi lakini kibiashara,
itachukua muda mrefu.
Hivyo,
Barcelona inahitaji uwekezaji na mwekezaji akaribishwe Camp Nou na
hakuna ubishi, atakayewekeza lazima atakuwa anahitaji kujitangaza na
lazima atataka kubadili jina.
Hili
linaonekana kuwakera wengi, mmoja wa manahodha waliokuwa na mafanikio
ndani ya Barcelona, Cares Puyol naye ameamua kufungua mdomo na kusema,
kuvunja jina la Camp Nou, ni kuiondoa Barcelona kwenye ramani ya soka
duniani kwa kuwa inaonekana ndiyo maarufu zaidi kwa klabu za Bara la
Ulaya.
Anaamini
na kukubali klabu inahitaji fedha ili kujilinda na mawimbi ya kifedha
yanayotarajiwa japokuwa anaona kuna mbinu zaidi za kuweza kuikomboa
Barcelona na soka la vijana ndiyo njia pekee.
Puyol amesema kupitia kituo cha kukuza vijana cha La Masia, au kushikilia suala la vijana, itakuwa ni msaada mkubwa sana.
Kibiashara,
Barcelona imebadilika kwa kuwa ilitaka kupambana na masoko. Neymar
alichukuliwa kwa ajili ya Brazil maana ilionekana wengi kutoka katika
nchi hiyo kama wanataka kuiweka kando Barcelona na kuonekana ni kama ya
watu wa Argentina anakotokea Messi, jambo ambalo halikuwa zuri kwao.
Suarez
alichukuliwa kwa biashara ya Uruguay lakini kuongeza ushindi kwa kuwa
anaaminika bora katika ufungaji mabao. Kawaida biashara hukua au kupaa
timu inapofunga mabao mengi au kushinda mechi nyingi. Hivyo biashara
yote ya soka, inategemea zaidi ya kufanya vizuri kwa timu.
Jina
la Camp Nou linaendelea kuwa utatanishi wa kipi sahihi cha kufanya
kulingana na muda. Tayari Barcelona wameonekana kuingia hofu kwamba kuna
hatari inakuja mbele na wanaweza kujikutana wanawauza kati ya nyota wao
hao watatu, jambo ambalo linaonekana halikubaliki kuanzia utosini mwa
Barcelona hadi kwenye unyayo wake.
Nitakuwa
zaidi Barcelona kwa siku moja, ninaamini nitapata nafasi nyingine ya
kukuletea taarifa kuhusiana na Barcelona inavyokwenda kiuchumi na
inavyoweza kuwatumia wachezaji kama mtaji wake, jambo ambalo klabu za
nyumbani zinapaswa kujifunza hili, kwani ni jambo muhimu na katika soka,
suala la furaha pekee, limepitwa na wakati.
SOURCE: CHAMPIONI





Post a Comment