MALINZI AWE RAIS TFF, AWE MWENYEKITI WA MKOA KAGERA, KICHEKESHO KINGINE CHA KARNE!
Na Saleh Ally, Barcelona
TAARIFA
za Jamal Malinzi kufanikiwa kutetea nafasi yake ya uenyekiti wa Chama
cha Soka Mkoa wa Kagera (KRFA), nimezipokea kwa masikitiko makubwa na
imenishangaza sana.
Malinzi
ameamua kugombea kwa mara nyingine kuwa Mwenyekiti wa KRFA na
ameshinda. Sasa anaendelea kuwa na cheo hicho na rais wa TFF, hili ni
jambo la ajabu kabisa.
Malinzi amegombea nafasi hiyo na kushinda, ameamua kufanya hivyo kwa kuwa tu katiba haimkatazi, kwake ni sawa kufanya hivyo!
Ninachojua
katiba pia inatungwa na wanadamu na inawezekana ingetolewa mifano mingi
sana kulilinda hilo, ‘yaani si unajua hata nanihii, au hata Ulaya au
kule Fifa' na kadhalika.
Hata
iwe vipi, kwa mtazamo wangu mimi naona ni jambo ambalo haliwezekani na
hakuna kinachokwepeka kama utazungumzia suala la kubabaisha mambo kama
tutaruhusu hilo.
Rais wa TFF ambaye ni bosi wa mikoa yote, ndiye bosi wa Mkoa wa Kagera. Maana yake huyu Malinzi ni bosi hadi kwake mwenyewe!
Ukitaka kusahau machungu ya mchezo wa soka unavyosuasua, hili nalo ni sehemu ya kuchekesha.
Katika
soka nchini, kila siku vichekesho vipya. Kama ambavyo uliona, baada ya
Azam FC kuitwanga Yanga na kubeba Ngao ya Jamii, wakati wakikabidhiwa
pale uwanjani, dakika chache tu ikabanduka na kubaki kioo cha jamii.
Mambo ndani ya TFF yanakwenda tu, raha tu na hakuna matata!
Huenda
ndiyo maana jambo kama hilo la Malinzi kuwa rais na ‘mkuu wa mkoa’
linaonekana ni la kawaida sana. Binafsi naliona si sawa kwa mambo mengi
sana.
Moja
ninaamini Kagera kuna watu wengi sana wenye uwezo wa kuongoza, pili
naona Malinzi ana majukumu mengi unapozungumzia maendeleo ya kisoka
nchini, timu za taifa za watoto, vijana, wanawake na kubwa. Vipi anaweza
kukaa akatulia na kufanya vitu vya Kagera.
Utaniambia
vipi Malinzi anaweza kutenda haki kwa asilimia mia linapotokea suala la
kuchagua kupeleka nyasi bandia kati ya Bukoba na Songea, au Kaitaba na
Nangwanda Sijaona. Lazima atachagua sehemu ambayo yeye ni kiongozi mara
mbili.
Hii
si picha nzuri kwa kiongozi hasa ambaye yuko kwenye mpira kwa ajili ya
maendeleo. Sidhani pia kama ni sahihi kufanya hivyo eti kwa kigezo
kwamba katiba haikatazi au hata kule Fifa yupo nani hii anafanya kama
hivyo.
Soka
la Tanzania ni kimeo, viongozi wamekuwa chanzo. Kama kweli Malinzi
anaamua kuingia huko, bado ni vizuri akajipa muda na nafasi ya kufanya
mambo kuliko kujiongezea majukumu ambayo kuna watu wengi wangeweza
kuingia na kusaidiana naye.
Kwenye
uchaguzi mkuu inakuwaje, anajipigia kura? Lakini kwake faida ni ipi,
anabaki na hiyo ili kujihakikishia kura? Au ni kweli kwa ajili ya
maendeleo?
Soka
ya Tanzania ina mengi imefeli, kunatakiwa juhudi za dhati kuiinua. TFF
ya Malinzi nayo imeyumba, hata kuitetea inakuwa ni kazi kubwa kwa kuwa
haina mwendo balansi, inayumba kila kukicha na hakuna kauli dhabiti
kwenye mambo mengi ya msingi.
Ahadi
tele, hakuna utekelezaji. Mipango mingi iliyojaa hadithi, migogoro
isiyoisha na klabu utafikiri nayo inamiliki klabu. Sasa kiongozi wake
mkuu, kuwa pia kiongozi wa mkoa ni jambo jingine la kuchekesha.
Ninaamini
Malinzi ni mtu anayepapenda kwao Kagera kama ilivyo kwa wengine lakini
hili la kuwa kiongozi wa mkoa na rais wa Shirikisho, si sura sahihi
katika maendeleo ya mpira.
Binafsi
naona ni kama hakuna malengo ya dhati kimaendeleo zaidi ya kuangalia
upatikanaji wa sehemu au nafasi za uongozi na inawezekana isiwe kwa
maendeleo ya mpira nchini.
Naiachia
hapa, lakini ushauri wangu, ndugu yangu Malinzi aliangalie hili mara
mbili kama kweli ana nia ya kusaidia mpira nchini, la sivyo hofu yangu
kwake, itazidi hata mashaka kidogo niliyonayo.
Post a Comment