SUALA LA MO DEWJI KUINUNUA SIMBA, UTANI UKAE PEMBENI KWANZA
Na Saleh Ally
AZAM
FC ni kati ya timu zilizofanikiwa kubeba ubingwa zikiwa na umri mdogo
sana. Inawezekana hazikuwa zimemaliza hata shule ya msingi.
Hata
kama haina wanachama lakini inajivunia mengi na hasa suala la
maendeleo, ndiyo inayomiliki miundombinu bora kwa ajili ya soka,
ikiwezekana kuliko timu zote kongwe za Afrika Mashariki.
Azam
FC haina mashabiki wengi sana, lakini wachache walioipenda, lazima
watakuwa wamevutiwa na mwenendo bora wa mpangilio wa maendeleo.
Yanga
na Simba, ndizo zinazoongoza kwa mashabiki wengi zaidi ikiwezekana
Afrika Mashariki na Kati. Lakini zina ugonjwa mkubwa unaohusiana na neno
maendeleo. Hazina na huenda si jambo la hivi karibuni.
Wazee
walioanzisha Yanga mwaka 1935 na Simba 1936, walikwenda wanabadilika
hadi kuziwezesha timu hizo kumiliki majengo katikati ya Jiji la Dar es
Salaam. Lakini sasa ni zaidi ya miaka 40 tokea zimekuwa na majengo kwa
mara ya kwanza, hakuna jingine jipya.
Mohammed
Dewji ametangaza kuwekeza Simba, akitaka kupata hisa asilimia 51 ili
amwage Sh bilioni 20. Tayari ametangaza kutoa nafasi kwa kipindi cha
mpito na ameuomba uongozi kufanya kwa miezi mitatu, hii ikiwa ni baada
ya mabadiliko kupitishwa na wanachama.
Lakini
kinachoendelea sasa ni wanachama au mashabiki wa Simba na wale wa
wapinzani wao kuendelea kulumbana na wanachoangalia ni bei ya uuzwaji wa
klabu yao kama ni sawa au si sawa.
Ukweli
wa faida, hakuna anayejadili kwa kuwa kwa zaidi ya miaka 75, Simba na
Yanga zimeendelea kujivunia ubingwa pekee lakini si vinginevyo.
Inawezekana
kabisa yako masuala ya msingi ya kujadili hasa faida kwa kuwa suala la
umiliki wa mtu mmoja au kampuni lipo tena wazi kama ambavyo tumeona
England na kwingineko.
Lakini
kikubwa ambacho kinapaswa kujadiliwa ni suala la faida zake ni zipi,
klabu itapata nini, wapi mipaka, upi ni mwisho wa kuhoji na kadhalika.
Nafikiri
mjadala kama huu ambao unahusisha kipindi cha mabadiliko ya mpira
nchini haupaswi kumalizwa kishabiki na watu kujadili kuwa “mmenunuliwa”
au “mmekodiwa” huku vicheko vikifuatia.
Huu
ni wakati wa utulivu, Wanasimba kwa kuwa wamepitisha, basi watoe nafasi
kwa uongozi wao na kama kuna kamati nayo ipewe ifanye kazi yake kwa
usahihi.
Kama
nilivyowahi kueleza, litakuwa jambo la msingi kupitisha jambo baada ya
kugusa kila sehemu husika badala ya haraka. Ninaamini miezi mitatu
aliyoomba Mo, inatosha kwa Simba kufanya hivyo.
Miezi
hiyo mitatu itatosha kama utaratibu utakwenda na watu wanaofanya mambo
yao kitaalamu au kwa kuhoji lakini si kugeuza ni mambo ya kawaida au
malumbano ya furahisha genge. Ukiwa na chuki na Mo, basi hutaki
mabadiliko, ukiwa unafurahishwa naye sana, basi mabadiliko yapite hata
bila kuhoji. Haiwezi kuwa sahihi.
Kuzuia
mabadiliko haya ambayo yameanza kujitokeza ni kujidanganya. Asilimia
kubwa kisoka duniani ambako kuna maendeleo makubwa, masuala ya hisa au
umilikishaji kwa matajiri upo na mafanikio yanaonekana. Inawezekana bado
kuna sehemu kama Hispania kama Real Madrid na Barcelona, wanatumia
wanachama na wanafanikiwa.
Lakini
hapa Tanzania, tumetumia wanachama kwa zaidi ya miaka 80, wote mnajua
tumefeli. Hivyo wawekezaji, wakiwa na sapoti ya wanachama au mashabiki,
basi wanaweza kuleta mabadiliko.
Kweli
soka ni ushindi na ndiyo furaha yenyewe, lakini dunia imebadilika. Sasa
ni ushindi na maendeleo na hayo hayapatikani kwa “kuuza” maneno kwenye
vijiwe pekee, badala yake kubungua bongo na kufanya matendo yanayolenga
kuleta maendeleo.
Dunia inapaa kwa kasi ya kimondo, lazima tukubali kwamba tumeachwa sana,
tena siku nyingi. Hivyo tuangalie, suala hili na lilipofikia, si
ushabiki wa uwanjani ni uhai wa klabu yenu na uhai wa mapenzi ya mioyo
yenu, msiiache ikafa nyie mikitaniana.

Post a Comment