NAWAPA POLE TFF KWA YANGA KUWAKOSESHA MAPAT LAKINI MUWE MAKINI NA MNACHOTAKA KUAMUA
| RAIS WA TFF, JAMAL MALINZI |
Na Saleh Ally
MASHABIKI
wa soka bado wanabaki na kumbukumbu ya kuingia bure katika pambano la
Yanga dhidi ya TP Mazembe katika mechi ya Kombe la Shirikisho iliyopigwa
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Ulikuwa
ni uamuzi wa uongozi wa Yanga kuamua kuwaingiza mashabiki bure kwa
lengo la kupata mchezaji wa 12, yaani mashabiki ambao wangeiunga Yanga
mkono kwa nguvu ili kuwamaliza mabingwa hao wa Afrika.
Kweli
mashabiki wengi walijitokeza na mechi ikachezwa na kuisha salama ingawa
kulikuwa na vurugu nje ya uwanja mashabiki wakitaka kuingia. Kizuri
zaidi, hakukuwa na vurugu zozote za kuhatarisha usalama ndani ya uwanja.
Baada
ya mechi hiyo ambayo Yanga ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya mabingwa hao
wa Afrika. Tumerejea katika maisha ya kawaida na mjadala mkubwa ni kwa
nini ilikuwa bure na inaonekana kabisa wako ambao hawakufurahishwa!
Walioamua
watu waingie bure ni Yanga ambao wanaihudumia timu yao. Walisema
wanafanya hivyo ili kupata sapoti kubwa ya mashabiki kwa kuwa walizitaka
sana pointi tatu za Mazembe kwa kuwa walipanga kushinda mechi zote tatu
za nyumbani ili kujiweka sawa baada ya kuwa wamepoteza mechi ya kwanza
ugenini dhidi ya Mo Bejaia kule Algeria.
Wakati
mechi hiyo imebaki historia, inaonekana kuna ugomvi unakuja. Kwani
Tayari TFF imetangaza ndiyo itakuwa ikisimamia masuala ya mechi zote za
Yanga likiwemo suala la ukataji wa tiketi, kitu ambacho ninaona ni kama
kichekesho.
Leo
TFF wamekumbuka shuka alfajiri, kwamba watakuwa wakiangalia wageni
wanapotua nchini kuja kucheza na Yanga, wao wanaangalia kila kitu.
Jiulize vipi hawakufanya hivyo kabla? Kama wanajua ni jukumu lao vipi
waliacha, ni uzembe na kwa nini?
Pia
wanasema wanasubiri ripoti ya kamisaa kuona kama kulikuwa na shida.
Hizi inanipa hofu, kwamba kuna uwezekano hata wao wakafurahia kuona
Yanga inalimwa faini ili kuthibitisha kwamba watu walioingia bure
haikuwa sahihi.
Ukiangalia
TFF wana kila sababu ya kukasirika kwa kuwa hawakupata mapato ambayo
walitegemea kuingiza mlangoni na hili hawawezi kumdanganya mtu kama
kweli walilifurahia.
Ndiyo
maana hata wakati wa mechi hiyo, viongozi wengi wa TFF si kama
tulivyozoea kuwaona uwanjani wakiingia kwa wingi hasa katika mechi
kubwa. Siku hiyo, wengi wakawa na majukumu mengine.
Nafikiri
hawapaswi kuonyesha wamekerwa sana na hiyo bure. Au hawana sababu ya
kuanzisha au kufikiri kuanzisha uadui au kutaka kukomoana na Yanga ambao
leo ndiyo wanaifanya TFF iendelee kujadili haya kwa kuwa imefikia
ilipo.
Kama
TFF itakuwa inatunishiana misuli na Yanga, hii itakuwa ni sehemu
nyingine ya kuonyesha kuna tatizo kubwa kwa mzazi ambaye ni shirikisho
hilo, kwamba anapenda sifa na hajali kuona wanaye wanaharibikiwa.
Kanuni
ipi inasema Yanga ilikosea kuwapeleka watu waingie bure? Kama haipo na
TFF iliona kuna tatizo kutokana na idadi kubwa iliyoingia, TFF ikae na
Yanga na kuwaeleza ambacho wanaona hakikuwa sawa.
Vizuri
ni kuepusha kuijaza Caf pumzi ili ione Yanga ilikosea sana. Fujo za nje
ya uwanja, hakuna taarifa za matatizo makubwa. Na kama yalikuwepo
kidogo, basi nini kifanyike kitu kuyamaliza ili wakati mwingine
yasitokee.
Hii
si mara ya kwanza Yanga kuamua mashabiki wake waingie bure katika mechi
ya kimataifa. Kipindi uongozi wao haukuwa na misuli kama hii ya sasa.
Hili
suala halihitaji hasira wadau, mashabiki walioingia bure ni Watanzania.
Tushukuru walitoka salama, kama linaonekana lina makosa ndani yake,
basi lijadiliwe kwa kiwango cha kujenga na si kulenga au kufikiri
kukomoa au kuonyeshana. Onyesheni mnalenga kuendeleza mpira.
Kama
Yanga wamekosea kutofanya biashara, basi vizuri muwashauri kibiashara
na athari zake ni zipi na si “mimi ndiye mwenyewe”, haya yamepitwa na
wakati sasa!
Post a Comment