TUNAENDELEA KUWALILIA WAZALENDO, LAKINI WAO WANAPIGANIA BANGI NA MAMBO KIBAO YA KIJINGA!
Na Saleh Ally
UKWELI
ni jambo jema sana katika maisha hata kama utakuwa umeamua kuwatetea
watu ambao unaamini ni wako au wale ambao unapaswa kuwatetea katika
jambo lolote lile.
Kila
Mtanzania ana haki ya kuwatetea wazawa kwa kuwa naye kama mzawa
atatetewa na wengine. Hilo ni jukumu la msingi na linaingia katika
kipengele cha uzalendo katika maisha ya kawaida.
Mimi
ni muumini wa wazalendo, natamani kuona kijana kutoka hapa nchini
akifanikiwa kuliko yule anayetokea nje ya nchi hii, acha niwe wazi tu
ili nieleweke.
Lakini
siwezi kuingia kwenye vita ya kumzuia kijana wa nje asifanikiwe kama
namuona ana juhudi na maarifa, anajituma pia ni mtu ambaye amepania
kufikia ndoto zake. Nitakachofanya nitamuunga mkono.
Nitakueleza
kwa nini nitamuunga mkono, mimi ni muumini wa watu wanaojituma, watu
wanaotaka kufanikiwa na wanapambana kwa vitendo badala ya maneno mengi
na kulalamika kila kukicha. Hapo, uzalendo nauweka kando.
Kupitia
Metodo, leo nimeona vizuri kujadili suala la wachezaji au wanasoka
wazalendo katika nchi yetu ambao wamekuwa wakisonga kwa mwendo wa kusua
na wengine wanalia kuwa wanavunjwa moyo au nguvu na viongozi wa klabu
mbalimbali ambao wanaonyesha kuweka nguvu nyingi kwa wageni.
Kuacha
viongozi waweke nguvu nyingi kwa wageni bila sababu zozote za msingi
hasa kama wanaona wana uwezo mdogo, kweli haliwezi kuwa jambo la
kuachiwa lipite hivihivi, tutalivaa na kupambana nalo na mara nyingi
nimekuwa nikifanya hivyo. Napinga wachezaji wa kigeni kulipwa fedha
nyingi kwenye Ligi Kuu Bara, huku wakipewa nyumba na marupurupu zaidi
lakini uwezo wao unafanana na wazawa au kuwa chini kabisa. Hilo siwezi
kukaa kimya hata kidogo.
Kinachoniudhi
ni kwamba wakati wazalendo tunapambana kwa ajili ya kuwarekebisha
viongozi ili watupe nguvu kwa vijana wazawa, vijana hao wanaendelea na
mambo ya kijinga kabisa ambayo wao wanataka kuyegeuza ni sehemu ya
maisha yao huku wakijua kweli ni ya kijinga.
Wachezaji
au wanasoka wengi wazalendo wanaamini bangi ni sehemu ya mafanikio,
wapo wanaoona mvuta bangi ndiye anayeweza kufanya vizuri katika soka,
hili ni jambo la kijinga kabisa.
Wako
ambao hawana nidhamu katika kazi yao, hawalali mapema, hawana muda wa
kupumzika, hawajitumi mazoezini, hawawasikilizi walimu wao lakini ajabu
wana ndoto za kufika mbali kwa maana ya mafanikio, huu ni ujinga
mwingine wa juu kabisa.
Kulitetea
taifa letu ni sehemu ya jukumu letu, lakini haitakuwa sahihi kuendelea
kuwatetea wanaofanya mambo ya kijinga ambayo wanajua ni tatizo kwao na
wakaendelea kufanya tena bila ya kuchoka, halafu tuendelee kuwalilia
kwamba wanapunjwa au kuonewa, utakuwa ujinga zaidi.
Kuna
kila sababu ya vijana wa Kitanzania ambao mnaamini soka ni ajira yenu
kuanza kutengeneza nidhamu ya juu kabisa kuhusiana na kazi na lazima
mjue, mnalipwa mishahara hadi Sh milioni moja na zaidi huku wale
wanaofanya kwenye makampuni makubwa kama benki, makampuni ya simu
hawawafikii mishahara yenu.
Lakini
kwa kuwa wengi wenu hamjui thamani ya kazi yenu, mnaendelea kuichezea
kazi huku mkiwa na nyimbo nyingi za kulalamika kuwa mnaonewa. Huenda ni
kwa kuwa na sisi tunaendelea kuwatetea, acheni mambo hayo ya kijinga ili
muweze kupiga hatua.
Vijana
wengi wa Kitanzania wana vipaji vya juu kabisa michezoni. Lakini
wamekuwa waoga kwenda kucheza nje ya Tanzania kwa kuwa wana hofu ya juu
kuhusiana na nidhamu yao na aina ya maisha wanayoishi.
Acheni
kulalama hovyo, fanyeni kazi kwa kujituma, kwa juhudi na maarifa. Pia
lazima mjue, hata kama una kipaji kikubwa kumpita Lionel Messi na
Cristiano Ronaldo halafu hauna nidhamu wala juhudi, utafeli tu. Hata
tukutetee vipi, utafeli tu.

Post a Comment