TAREHE YA KUTOLEWA KWA ZAWADI ZA LIGI KUU BARA HII HAPA
Mabingwa
wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Young Africans SC na timu
nyingine zilizoshiriki katika msimu ulioisha wa 2015/2016 zitakabidhiwa
zawadi zao mapema mwezi ujao na Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom
Tanzania ambayo ni mdhamini mkuu wa ligi hiyo.
Meneja
Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu amesema kuwa ucheleweshaji
wa kutoa zawadi hizo baada ya kumalizika, umetokana na baadhi ya timu
zinazoshiriki kwenye mechi za mashindano ya kimataifa kama vile
mashindano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika na kuingia kwa mfungo wa
Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
“Tunaomba
radhi kwa timu husika, wachezaji na wadau wa soka kwa zoezi hili
kuchelewa ila tunawahakikishia kuwa zawadi ziko tayari na
zitakabidhiwa mwezi ujao,” alisema Nkurlu.
Pia
alishukuru wadau wote waliofanikisha ligi hiyo hadi kufikia mwisho
ambapo Young Africans ya jijini Dar es Salaam iliibuka tena bingwa kwa
mwaka huu.
“Licha
ya changamoto zinazoendeleza kujitokeza katika ligi yapo mafanikio
makubwa na ligi hii inazidi kuwa na msisimko mkubwa nchini tunawashukuru
wadau wote na tuna imani kuwa itazidi kuwa bora katika siku za usoni,”
alisisitiza Nkurlu.
Alisema
kuwa Vodacom Tanzania itaendelea kutoa udhamini wa ligi hii hata katika
msimu ujao kwa mujibu wa mkataba wake na TFF na aliwataka wadhamini
wengine kujitokeza ili kuboresha zaidi ligi hii ikiwemo kuwawezesha
wachezaji kunufaika zaidi katika ushiriki wake.
Post a Comment