MSISITIZO, SERIKALI IMECHEMSHA SUALA LA KUSITISHA UMMITASHUMTA, UMISETA, WANAOTETEA, KUNA CHAO WANAKITAKA
![]() |
| WAZIRI SIMBACHAWENE |
Na Saleh Ally
Kati ya wadau ambao nimekuwa nikiwaona wakipambana kwa ajili ya michezo hasa mchezo wa riadha ni Gida Budayi.
Lakini
leo amenishangaza alipokuwa akizungumzia msimamo wake kuhusiana na
kusimamishwa kwa michezo ya Shule za Msingi na ile ya Sekondari maarufu
kama Ummitashumta na Umiseta.
Siku tatu zilizopita, Waziri wa Ofisi ya Rais ,Tamisemi, ,utumishi na Utawala bora,George Simbachawene
alitangazwa kusitishwa kwa michezo hiyo kwa madai ya kutaka kutimiza
agizo la Rais John Pombe Magufuli, kwamba hadi mwisho wa mwezi huu,
kusiwe na mtoto anayekaa chini.
Gida
Budayi alisema angependa kutofautiana na wadau waliolaumu kuhusiana na
suala hilo. Akidai yeye anaona tofauti kwa kuwa kuna haja gani ya
kulazimika kuwa na mbegu wakati huna shamba. Kwamba wale watoto
wanaoshiriki michezo, wanapofanikiwa wanakwenda wapi wakati hakuna
sehemu kama vile vituo vya michezo.
Mdau
huyo katika mahojiano na Radio One alionekana kabisa alikuwa akilenga
kuhusiana na mchezo wa raidha ambao yeye ni mdau mkubwa.
Msisitizo
wake ni kwamba, hata kama watoto wakifanya vizuri, basi hakuna pa wa
kuwapeleka. Mwisho akahoji hata soka vipi hawashiriki Olimpiki kama
ilivyokuwa Nigeria iliyokuwa ya kwanza kushiriki enzi za kina Kanu.
Lakini
Gida Budayi akaenda mbali zaidi kwa kusema kuna maofisa elimu ambao
wanakaa tu maofisini na ndiyo wamekuwa wakizitumia fedha hizo kujenga
nyumba zao.
Nami
niwe wazi, nionyeshe ninampinga mdau huyo kwa kusema hivi, nimekuwa
nikiunga kwa nguvu zote mapambano yake ya kuinua mchezo wa riadha,
lakini safari hii anaonekana alinuia kujipatia sifa au kutaka kusikika
au kuona raha akiwa mtu mwenye upande usio na wengi bila ya kujali
alizungumza mambo mengi sana ya kubahatisha, hakika sikutarajia.
Nianzie
na alipoishia, lini amewahi kueleza uozo wa maofisa elimu kutumia fedha
za michezo kama Umiseta au Ummitashumta kwa ajili ya kujenga nyumba
zao?
Ajabu
zaidi, anaanza kuzungumzia Olimpiki akiamini katika soka ndicho pekee
kinachotafutwa! Hajui michezo hiyo imetoa wachezaji wangapi ambao leo
wanaishi maisha mazuri maradufu!
Hajui
kuna wachezaji waliopitia katika michezo hiyo, leo wanamiliki majumba
na usafiri kwa kuwa walitafutwa. Hajui kulikuwa na shule kama Makongo
ambayo ilijitolea kuwaendeleza na wengine wakawa shujaa wa taifa letu
katika ngazi za klabu au taifa letu?
Najua
Gida Budayi alipata elimu yake nje, huenda aliporejea hakujifunza mambo
mengi sana aliyoyaacha nyuma na hakutaka kujua ndiyo maana hana uchungu
na michezo hiyo ya shule za msingi na sekondari.
Wakati
mwingine nilianza kufikiria Gida Budayi atakuwepo kwa ajili ya kupinga
chochote atakachokitetea Filbert Bayi kwa kuwa tu amekuwa akitofautiana
naye katika masuala ya riadha.
Nimekuwa
nikimuunga kwa pointi nyingi za msingi kuhusiana na riadha wakati
akimueleza Bayi. Lakini katika hili, kama kweli kwa kuwa Bayi amepinga
kusimamishwa kwa michezo hiyo, basi lazima yeye aibuke na kusema anaunga
mkono, itakuwa ni kitu cha ajabu kabisa kuingia masikioni mwa wadau wa
soka.
Angalia
hapa, wakati yeye anasema anaunga mkono, mwisho anapishana na
ilichokifanya serikali iliyoamua kununua madawati fedha za michezo hiyo.
Yeye anasema anaunga mkono, huku akitaja kujengwa kwa vituo vya
michezo. Sasa serikali kwani imejenga vituo vya michezo.
Lakini
je, baada ya kusimamishwa mwaka huu, kama mwakani itakuwepo, vituo vya
michezo vitakuwa vimekamilika? Naona ni maneno yasiyo na faida, sawa na
mbegu zisizoweza kuzalisha mazao zilizopandwa shambani.
Vizuri
wadau wa michezo tuangalie hili kwa jicho la tatu badala ya kila mmoja
kutaka kujipatia sifa kwa kuzungumza tu ili mradi asikike. Kweli kila
mmoja ana haki ya kutoa mawazo yake, lakini vizuri kutafakari kabla ya
kuyatoa kwenye jamii.
Wamesema
serikali imeokoa bilioni 1.5 kutoka kwenye Ummitashumta na Umiseta.
Inaumiza sana kusikia kutofanyika kwa michezo ya wanafunzi wa shule za
msingi na sekondari ni kuokoa fedha!
Vipi
mbona hawakusitiza Mwenge wa Uhuru, Vipi Hawakusitiza sherehe zote
zinazohusiana na kuadhimisha ukiachana na il ya Uhuru. Kwani zile
mwendelezo wake kwa maana ya maendeleo ni nini.
Serikali
haina urafiki wala ukaribu na michezo, hata Sh bilioni 1.5 inayotoa kwa
ajili ya wanafunzi hao nayo inaonekana inapotea? Kama inashindwa
kufanya fainali tu za wanafunzi, itaweza vipi kutenga kiasi cha fedha
kusaidia michezo nchini.
Michezo ni ajira, inaingiza kipato kwa taifa kupitia kodi. Lakini leo inaonekana eti kutofanyika kwake ni kuokoa fedha.
Angalia
katika soka, fedha zinaingia serikalini kupitia Kodi ya Mapato,
inaingia kupitia viwanja, maana mapato yake yanakatwa na kadhalika. Vipi
serikali inaona kutofanyika kwa michezo ni kuokoa fedha. Tena michezo
ya wanafunzi ambao kila siku wanahimizwa kushiriki michezo.
Wangapi
watakuwa wamekata tamaa na kuamua kuachana na michezo baada ya kuona
serikali haithamini? Hakika huu ndiyo wakati wa kutafakari na
wanaochangia wawe makini kuliko kutaka “kujionyesha” au kuzungumza kwa
manufaa yao binafsi badala ya taifa letu.
Mimi
naendelea kusisitiza, suala la vituo vya michezo ni zuri, suala la
madawati ni zuri lakini hakukuwa na ulazima wa kuisimamisha michezo eti
kuokoa fedha.
Kwangu
naona ndani yake kuna uoga, waziri hakuwa mtulivu ili aweze kuhakikisha
michezo hiyo inaendelea na madawati yanapatika. Hakutulia kufanya
ubunifu au hakuwa tayari kufanya ubunifu na kilichofanyika sasa si sawa
hata kidogo.

Post a Comment