MAAMUZI YA SIMBACHEWENE KUSIMAMISHA MICHEZO NI KUIUA, PIA YANA UOGA NDANI YAKE
Na Saleh Ally
WAZIRI
wa Ofisi ya Rais Tamisemi, Geroge Simbachawene ametangaza rasmi kuzuiwa
kufanyika kwa Umoja wa Michezo ya Shule za Msingi (Umitashumta) na ule
wa shule za sekondari (Umisseta).
Michezo
ya Umisseta ilipangwa kufanyia kuanzia jana hadi Juni 22 jijini Mwanza,
ni siku tisa. Halafu ile ya Umitashumta ingefanyika kuanzia Juni 25
hadi Julai 5, jumla ni siku 10.
Simbachawene
amesema wameamua kusitisha michuano hiyo ili kuweza kusimamia kwa
ukamilifu utekelezaji wa agizo la Rais John Pombe Magufuli kuhusiana na
suala la madawati mashuleni. Wanataka kutekeleza kwa wakati agizo lake
la kila mwanafunzi kuwa ameketi kwenye dawati ifikapo nwishoni mwa mwezi
huu.
Waziri
Simbachawene hajui kama wachezaji nyota wa Tanzania walipatikana katika
Umitashumta na Umisseta. Iliposimamishwa na Waziri wa Elimu, Joseph
Mungai wakati huo, ilikuwa ni kuiua michezo na madhara yake tumeyaona
miaka nenda rudi. Serikali ya awamu ya nne ilielewa kosa lililofanyika
katika awamu ya tatu, ikairejesha michezo mashuleni.
Simbachawene,
ameizika rasmi. Yeye anasema itafanyika itakapotajwa tena, huenda
mwakani lakini alichokifanya ni kuonyesha ni kiasi gani michezo imewekwa
kama ‘spea tairi’ katika nchi hii, kila kitu kinakuwa wazi, haitakuwa
na maendeleo.
Nawakumbusha
Dua Said aliyeng’ara Simba, leo ana miradi yake na anaendesha maisha
lakini hakuwahi kufika chuo kikuu. Soka ilimtoa kimaisha leo anaweza
kuishi vizuri kuliko wahitimu wa chuo kikuu.
Tunawajua
wachezaji wengi Watanzania ambao wana ajira zao kwa sasa, wanalipwa
mishahara ya Sh milioni moja na zaidi kwa mwezi na serikali inaingiza
kodi, lakini walianzia kwenye mashindano hayo ya mashule.
Nyota
wa taifa hili, mfano Edibily Lunyamila, kwenye kikapu Ramadhani Dullah,
Nteze John Rungu aliyeng’aa baadaye Pamba na Simba, hawa wote ni zao la
Umisseta na Waziri Simbachawene halijui hili, ameamua kwa kuwa anataka
kutimiza agizo la rais la madawati.
Sitaki
kusema agizo la madawati ni baya, lakini ninaona ni uamuzi wa hofu, kwa
kuwa Waziri Simbachawene haujui umuhimu wa michezo, hajui
tulivyoipigania irudishwe na huenda hajui michezo ni somo jingine muhimu
na nyenzo muhimu ya afya bora.
Ninaamini
anaona michezo ni michezo kwa ajili ya kucheza. Anasahau ni ajira na
chanzo kikubwa cha ajira, ndiyo maana wachezaji ambao hawajafika chuo
kikuu hapa nyumbani, wanalipwa fedha nyingi kuliko wafanyakazi
waliohitimu vyuo vikuu.
Serikali
nayo inafaidika na kodi kupitia michezo kwa kuwa mishahara mikubwa na
kodi inayopatikana ni nyingi. Sasa vipi uue michezo ili ufanikishe
kutengeneza madawati?
Kwani
Simbachawene haumizwi na hili? Kama angekuwa ameagizwa ningeanza kuwaza
ameshindwa vipi kumshauri rais kwamba michezo ni ajira, michezo ni
chanzo cha kodi na tunapaswa kuanza kuwakuza na kuwalea au kuwaona
vijana wengi wakiwa shuleni kwa kuwa haitatokea siku mchezaji akakua
kama mbuyu, lazima apitie hatua hizo.
Niwe
mkweli, nimeumizwa sana kuona kwa mara nyingi michezo inarudishwa
shimoni na serikali ambayo imekuwa haiko tayari kuisaidia michezo na
huku viongozi wake wakiwa ni sehemu ya wanaofurahia kwa kiasi kikubwa
inapotokea wanamichezo wakapata mafanikio kiduchu kabisa.
Serikali
itafakari, ilichofanya imekurupuka. Huenda wako wanaohofia kusema kwa
visingizio vingi tu. Lakini mimi siwezi kuwa mwoga kwa kuwa hii ndiyo
nchi yetu sote, tunapaswa kupigania kila kilicho sahihi.
Alichofanya
Waziri Simbachawene si sahihi hata kidogo na inaonyesha ni uamuzi
uliojaa uoga. Na kama itakuwa ni uamuzi kutoka juu serikalini, pia si
sahihi kwa kuwa ni kuidharau na kuirudisha nyuma michezo huku
mkidhoofisha vipaji vya vijana.
Msitake
kutushawishi kuwa kila mtoto atakayetokea shule ya msingi na baadaye
sekondari atakwenda chuo kikuu. Wengine wataishi kwa vipaji vyao baada
ya hapo, hivyo ni vizuri kuviheshimu vipaji. Kwa kuwa serikali
haionyeshi mapenzi navyo katika kuvilea, basi vizuri ikaheshimu
mashindano machache kama hayo iliyoyasimamisha.
Serikali
haina mpango mkakati wowote wa kuendeleza michezo kwa maana ya kujenga
vituo vya michezo. Kuendeleza vipaji na vitu vingi vinaendeshwa na
taasisi tu.
Kama
nilivyoeleza awali, kwenye mafanikio serikali kwa kuwa ndiyo baba
inajumuika. Sasa imeamua kuziba mfereji tena wa ukuzaji na endelezaji wa
vipaji vya michezo ambavyo baadaye vinaweza kujitegemea katika suala la
ajira na kuipunguzia serikali kazi. Sidhani kama kulikuwa na upembuzi
yakinifu katika hili au kwa kuwa ile ‘watasema watachoka’ linaonekana ni
jambo la kawaida tu kwa kipindi hiki. Nasisitiza, kilichofanyika si
sawa hata kidogo.



Post a Comment