Aliyetumbuliwa na JPM anunua benzi la mil.75
DAR ES SALAAM: Kigogo mmoja wa
bandari aliyetumbuliwa na Rais Dk. John Magufuli ‘JPM’ hivi karibuni
amejinunulia gari la kifahari aina ya Benz lenye thamani ya shilingi
milioni 75.
Akizungumza na gazeti hili
ofisini kwake hivi karibuni katika mahojiano maalum, Mwenyekiti wa Taifa
wa Umma Party ambaye pia ni mfanyabiashara wa kuuza magari, Wakili
Hashim Rungwe alisema kigogo huyo alinunua Benz hilo kwa ajili ya
matumizi yake binafsi licha ya kudhaniwa kuwa, kwa sasa angekuwa hana
kitu.
“Kiujumla utumbuaji wa majipu sioni
faida yake kwa wananchi wa kawaida kwa sababu wote waliotumbuliwa
wanapata mishahara yao kama kawaida na hivi karibuni kigogo mmoja wa
bandari alikuja kwangu kwenye yadi na kununua Benz la thamani ya
shilingi milioni 75,” alisema Wakili Rungwe bila kumtaja jina kigogo
huyo.
Aliongeza kuwa, utumbuaji majipu bado
haujasaidia kuondoa njaa kwa wananchi wa kawaida badala yake ameshuhudia
waliotumbuliwa wakiendelea ‘kutanua’ mitaani na kula mishahara yao bila
kuifanyia kazi.
Alisema kuwa, wakati wa kufanya manunuzi
ya gari hilo, kigogo huyo alimwambia kuwa, kwa sasa kila akiamka
anafikiria kwenda kutumbua maisha wapi.
“Alisema yeye na familia yake ni bata tu
siku hizi, maana wakati mwingine anakwenda ufukweni na mkewe na watoto
wote. Kifupi aliniambia hajapata athari zozote kwa kutumbuliwa,” alisema
Rungwe kwa mshangao mkubwa.
Hivi karibuni serikali imewatumbua
vigogo wengi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania na wale kutoka Kodi ya
Mapatao TRA kwa kuwasimamisha kazi kwa madai kwamba waliwasaidia
wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi hivyo kuikosesha serikali mabilioni
ya shilingi.
Hata hivyo, vigogo wote waliosimamishwa
kazi kwa agizo la JPM, wamepisha uchunguzi na wengine wako mahakamani
ambapo itakapothibitika kuhusika katika ufisadi, kutanua huko kutageuka
kuwa uchungu.
Post a Comment