HAKIKA DIEGO SIMEONEHANA BAHATI LAKINI KAZI YAKE ANAIJUA KWELI
Na Saleh Ally
KWANZA
anza kwa kujiuliza kama ungekuwa wewe ndiye Kocha wa Atletico Madrid,
Diego Simeone ungejisikiaje? Hakika ni maumivu makali ya moyo.
Lazima
ungehisi au kuamini hauna bahati hata kidogo na hasa linapofikia suala
la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ndani ya miaka mitatu, Simeone amekiongoza
kikosi chake kucheza fainali mara mbili dhidi ya timu moja.
Fainali
ya kwanza msimu wa 2013/14 ilikuwa dhidi ya Real Madrid kama ile ya
2015/16. Zote mbili wamepoteza, moja wakianza kufunga Madrid
wakasawazisha, ya usiku wa kuamkia jana wakaanza kufungwa, wakasawazisha
na kung’olewa kwa mikwaju ya penalti 5-3.
Mtu
asiye na bahati kwa Lugha ya Kihispania anaitwa sin suerte. Unaweza
ukampa jina hili Simeone raia wa Argentina anayeonekana ni mtu asiyekata
tamaa na kila kitu.
Simeone
ni kocha aliyeshinda makombe kadhaa makubwa na muhimu akiwa na Atletico
Madrid. Amechukua ubingwa wa La Liga, Copa del Rey, Super Cup Hispania,
Europa Cup na Uefa Super Cup pia.
Si
mgeni wa makombe tokea akiwa mchezaji hadi kocha. Lakini kombe pekee
ambalo linaonekana kumteleza kila anapojaribu ni lile la Ligi ya
Mabingwa Ulaya.
Rekodi
yake na kikosi cha Atletico Madrid inamfanya aonekane mmoja wa makocha
bora kabisa kuwahi kuifundisha timu hiyo aliyowahi kuichezea pia.
Tokea
ajiunge nayo mwaka 2011, ameiongoza katika mechi 260. Ameshinda 164,
sare 52 na kapoteza 44, hii inamfanya awe na wastani wa juu kabisa wa
63.1% ya ushindi. Huu ni wastani wa juu kwa kocha anayefundisha timu
kubwa zinazoshiriki michuano yenye ushindani wa juu.
Ukiachana
na rekodi za mafanikio yanayopatikana baada ya mchezo, angalia mchezo
wenyewe. Mfano, fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Madrid pale
jijini Milan, Italia.
Kikosi
chake kilicheza vema zaidi, ingawa mwenyewe mwisho alisisitiza kwamba
kuna mambo walizidiwa ambayo ndiyo yalifanya wapinzani wao mwisho wabebe
ubingwa huo mbele yao.
Simeone
anakubali kuwa ana maumivu ya moyo, huenda maumivu hayo yametambaa kwa
mashabiki wengi wa soka duniani kote wakiwemo wale ambao si mashabiki wa
Atletico Madrid, lakini wanaumia kwa kuwa wanajua kocha huyo
Muargentina anaifanya kazi yake kwa ufasaha.
Wanajua
kikosi chake kufikia kucheza namna hiyo ni mtu anayejituma, anayefanya
jambo kwa juhudi kubwa lakini inaonekana mafanikio yanamkimbia hasa
katika Ligi ya Mabingwa.
Kabla
ya mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa jijini Milan, Ronaldo de Lima
alipata nafasi ya kumzumngumzia Simeone ambaye alicheza naye timu moja
wakiwa Inter Milan ya Italia pia.
Ronaldo
alianza kwa kupinga tabia ya Simeone kupandikiza hasira za Kiargentina
kwa wachezaji wake, akisema wanakuwa wajeuri na wakatili. Lakini mwisho,
akasema ni wagumu kushindika na kocha huyo ni kati ya makocha bora
kabisa duniani.
Kwenye
kutengeneza jambo mengi yanatokea, lakini mwisho ni matokeo bora.
Simeone amekuwa akiyapata lakini tatizo kubwa ni Ligi ya Mabingwa.
Kinachovutia kwa huyu jamaa ni maneno yake ya mwisho kuhusiana na kuonekana hana bahati ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
“Sitaki
kuonyesha machungu yangu kwenu, lakini najua naumia kiasi gani kufika
hapa mara mbili lakini sijarudi nyumbani na kombe. Hakuna ambaye
angeweza kufurahia.
“Utaona,
wachezaji wamepambana hadi mwisho, wamecheza mechi nyingi sana ndiyo
maana dakika 15 za dakika 30 za nyongeza, kila mmoja alionekana ameisha
kabisa.
“Najua
hatukufika hapa kwa bahati hata kama kweli tuna bahati mbaya. Hatuwezi
kuishia hapa, niwaahidi ninabaki Atletico na kwa mara nyingine tunataka
kufika fainali ili tuiondoe bahati mbaya,” anasema.
Wengi
wanaamini Atletico au Simeone wana bahati mbaya na kombe hilo. Kutokana
na wanavyojituma watu wanawaonea huruma, vyote viwili anavikataa.
Utagundua
kuwa Simeone si mpiganaji wa muda mfupi, si muoga, si anayetaka kuonewa
huruma na anachoamini ni kurejea na kupigana tena ili wafike fainali
kumaliza makosa ya fainali mbili zilizopita.
Hakuna
ubishi, siku wakifanikiwa kuingia fainali tena, kutwaa kombe hilo
halitakuwa na mjadala. Lakini utaona namna kamanda anavyopaswa kuwa,
hata kama kaumia anaonyesha bado mapambano yanaendelea.
Simeone
anaficha maumivu yake ili kuinua mioyo ya wachezaji wake lakini pia
anafuta hisia za wao hawana bahati na Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kama yeye akikubali, maana yake vijana wake wakati mwingine watakuwa hawana sababu ya kulipigania.
Hii ni
falsafa ya kiongozi sahihi ambaye maisha yake yote hachoki kupambana na
hakati tamaa kwa kuwa hataki kuonewa huruma. Kuhurumiwa ni falsafa ya
kusaidiwa au kubebwa, Simeone hataki na tayari amerejea tena kwenye
mapambano.
MAFANIKIO YA SIMEONE
AKIWA MCHEZAJI
Atletico Madrid
La Liga (1): 1995–96
Copa del Rey (1): 1995–96
Inter Milan
Uefa Cup (1): 1997–98
Lazio (4)
Serie A (1): 1999–2000
Coppa Italia (1): 1999–2000
Supercoppa Italiana (1): 2000
UEFA Super Cup (1): 1999
TIMU YA TAIFA
Argentina (4)
Kombe la Mabara Fifa (1): 1992
Copa America (2): 1991, 1993
Artemio Franchi (1): 1993
Medali ya Fedha Olimpiki (1): 1996
KAMA KOCHA
Estudiantes de La Plata (1)
Ubingwa Argentina (1): Torneo Apertura 2006
River Plate (1)
Ubingwa Argentina (1): Torneo Clausura 2008
Atletico Madrid (5)
La Liga (1): 2013–14
Copa del Rey (1): 2012–13
Supercopa de Espana (1): 2014
UEFA Europa League (1): 2011–12
UEFA Super Cup (1): 2012
BINAFSI
Kocha Bora wa Mwaka La Liga (2): 2012–13, 2013–14
Tuzo ya Miguel Munoz (1): 2013–14
Kocha Bora wa Mwezi La Liga (2): Oktoba 2013, Novemba 2015



Post a Comment