Askofu aipinga tume ya Pinda
ASKOFU wa Kanisa la PAG, Charles Kanyika, ameikosoa serikali kwa
kusema kuwa kuundwa kwa tume ya kuchunguza chanzo cha wanafunzi wa
kidato cha nne kushindwa kufaulu mitihani si dawa ya kutatua tatizo la
elimu nchini.
Akizungumza ofisini kwake juzi, aliongeza kuwa
kitendo cha wanafunzi kufeli ni hatua mbaya zaidi kwa serikali na
kutengeneza taifa la watu ambao hawajui la kufanya hapo baadaye.
Alisema makosa hayo si ya walimu bali ni ya serikali, kwani imekuwa
ikipuuzia maoni ya wadau wa elimu ambao huishauri serikali kwa nia njema
ya maendeleo.
Alisema tume zinazoundwa na serikali mara nyingi hazina majibu ya
kuridhisha na badala yake hutumia fedha nyingi za walipa kodi bila
kupatiwa faida wala majibu ya kina.
Askofu Kanyika alisema kuundwa kwa tume kulikotangzwa na Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, hakuwezi kutoa majibu sahihi ya tatizo lililopo.
Akizungumzia masuala ya udini ambao unaonekana kushamili kwa kasi,
Askofu Kanyika alisema vuguvugu hizo ni mbegu ya serikali kwani mara kwa
mara walikuwa wakieneza chachu ya udini kama sehemu ya propaganda za
kisiasa.

Post a Comment