ad

ad

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yawavaa waangalizi wa uchaguzi...Baada ya waangalizi wa ndani na nje kugoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema haina muda wa kuwabebeleza waangalizi wa kimataifa waliosusia uchaguzi wa marudio utakaofanyika Machi 20, mwaka huu, wakiwamo wa Umoja wa Ulaya (EU).

Tamko hilo lilitolewa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ofisini kwake, Vuga mjini hapa, kuhusu uchaguzi huo.

Alisema uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, ulifutwa na matokeo yake baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC)  kujiridhisha kuwa haukuwa huru na haki.

Waziri Aboud alisema kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, uamuzi wa tume ni mwisho na haitakiwi kuingiliwa na mamlaka au mtu katika utekelezaji wa majukumu yake.

"Hatuna sababu ya kuwabebeleza waangalizi wa kimataifa kuja Zanzibar kuangalia uchaguzi wa marudio,'' alisema.
Msimamo wa SMZ umetolewa baada ya EU,  Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Marekani na Uingereza, kususia uchaguzi wa marudio kwa madai ule wa Oktoba ulikuwa huru na wa haki.

Wakati waangalizi kutoka jumuiya na nchi hizo wakisusia, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wameomba kupewa mwongozo Tume wa kushiriki uchaguzi huo.

Aidha alisema kuwa suala la uchaguzi ni mambo ya ndani ya nchi na yanasimamiwa na katiba na sheria, ndiyo maana Tanzania haikutoa msimamo wake baada ya utata wa matokeo ya uchaguzi wa Marekani wa mwaka 2000 katika jimbo la California.
 

CHANZO: NIPASHE

No comments

Powered by Blogger.