Mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Februari 2016 wapungua kwa asilimia 5.6
Mfumuko
wa bei wa Taifa kwa Februari, umepungua kutoka asilimia 6.5 za Januari
hadi 5.6 kutokana na kupungua kwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa za
vyakula, matunda, mafuta ya dizeli, vinywaji na samaki.
Hata
hivyo, akitangaza takwimu hizo jana, Mkurugenzi wa Sensa za Jamii na
Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephraim Kwesigabo
alisema; “hii inamaanisha kwamba kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na
ununuzi kwa mwaka ulioishia Februari ndiyo imepungua wala siyo kushuka
kwa bei. Naomba lieleweke hapo. Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na
vinywaji baridi kwa Februari umepungua kutoka asilimia 10.7 ya Januari
hadi 9.5 Februari,” alisema.
Kwesigabo
alisema kupungua kwa mfumuko huo kumechagizwa na kupungua zaidi kwa bei
za baadhi ya bidhaa ya vyakula na zisizo za vyakula kwa kipindi
kilichoishia Februari.
Alitaja
mwenendo wa baadhi ya bei za bidhaa zilizoonyesha kupungua kuwa ni gesi
asilimia 10.3, dizeli asilimia 4.5 na matunda asilimia 7.2.

Post a Comment