ad

ad

SINGIDANI (A Story From My Heart) - 35



 

Chris alipokea funguo za gari kisha akanyanyua mkono juu na kuwaonesha wageni ukumbini. Ghafla akagonganisha macho na mtu ambaye hakutarajia kabisa kumuona!
Chris alishtuka sana!
SASA ENDELEA...
MSHTUKO ulikuwa mkubwa kwa hakika, kumuona mtu yule ambaye pia hakumwalika na alikuwa na uhakika kuwa Laura naye hakumwalika, kulimchanganya sana.
Akajitahidi kujikaza. Akaweka zile funguo za gari alizokabidhiwa na baba yake mfukoni. Baba yake akarudi kwenda kukaa sehemu yake. Chris alipomwangalia Laura akagundua kuwa, naye alikuwa amemuoana yule mtu.
Alikuwa ni Julius.
Jully, yule mwanafunzi aliyekuwa akisoma na Laura chuo Singida. Ni Jully ndiye aliyesaidia kuwaunganisha. Kwa maneno mengine kama si yeye, usiku ule pale club, kulikuwa na uwezekano mkubwa kwa Chris kumkosa kabisa Laura.
Zoezi la zawadi likaendelea ambapo Mzee Ngeleja alitangaza kutoa ekari 50 za mashamba ya mpunga, yaliyopo Mbarali, Mbeya. Ilipofika zamu ya wageni waalikwa, Jully naye alikwenda.
Alitoa bahasha ya kaki kwenye sehemu ya kuwekea zawadi kisha akamsogelea Chris na kumpatia karatasi ndogo.
“Hongera sana kaka, usijiulize ningekujaje hapa, ila naomba unitafute baada ya fungate, namba zangu zipo humu kwenye karatasi, kuna jambo lazima nikuambie.”
“Poa.”
Akatoka hapo na kwenda kwa Laura. Akamkumbatia na kumpongeza.
***
Tayari mipango yote ya fungate ilikuwa imefanyika. Wazazi wa bwana  na bibi harusi waliamua kuchangia fedha kwa ajili ya safari ya watoto wao.
Ulikuwa muunganiko mzuri sana wa familia hizo mbili. Wazazi waliwataka watoto wao wachague kisiwa chochote duniani, waende wakastarehe kwa wiki mbili katika kufurahia ndoa yao mpya.
Kitu cha kushangaza ni kwamba, wote kwa pamoja walikubaliana kwenda Zanzibar. Wazazi walishangaa.
“Kwa nini Zanzibar?” Mzee Ngeleja aliuliza.
“Kwanza ni hapahapa Tanzania, tunapenda kufanya utalii wa ndani baba. Lakini pia tuna mambo mengi sana ya kufanya kama wanandoa, hatutaki kwenda mbali wala kutumia muda mrefu kwa ajili ya fungate.
“Wiki moja itatosha sana mjini Zanzibar kwa mapumziko ya fungate yetu, wiki nyingine tutakwenda Singida, halafu tutarudi Dar kuendelea na mambo mengine.”
Hakuna aliyepinga, Mzee Ngeleja na Mzee Shila wakakubaliana kwa pamoja na watoto wao. Walilala The Atriums Hotel iliyopo Sinza–Afrika Sana ambapo asubuhi ya saa 4:00 waliondoka hadi uwanja wa ndege walipopanda ndege na kuelekea visiwani Zanzibar.
***
Wakiwa wamejipumzisha kwenye bustani ndani ya Hoteli ya Karafuu mjini Unguja wakicheza michezo ya kimapenzi, Chris akamkumbuka Jully.
“Mh! Lakini Jully anaonekana ana jambo muhimu la kuniambia, lakini sijajua ni nini. Ngoja nikachukue ile namba yake ya simu ndani,” akasema Chris.
“Hapana dear, ngoja nikachukue. Umeweka wapi?”
Chris akamwelekeza.
Laura akanyanyuka na kwenda ndani, baadaye aliporejea alikuwa na karatasi yenye namba ya simu, akampa mumewe. Chris palepale akampigia Jully.
“Kaka ulisema nikutafute baada ya fungate lakini naona kama nachelewa sana kujua, ndiyo maana nimekutafuta mapema,” akasema Chris mara baada ya Jully kupokea simu.
“Usijali kaka, uko wapi?”
“Zanzibar, tunaweza kuzungumza sasa?”
“Siyo ya kwenye simu kaka, halafu napenda nikizungumza uwe na Laura.”
“Njoo Zanzibar basi, kila kitu nitagharamia mimi.”
“Kweli?”
“Ndiyo, tena ikiwezekana leo. Sema nifanye mpango wa ndege ya jioni mara moja.”
“Nakubaliana na wewe.”
Ndivyo ilivyokuwa, mipango ikafanyika vyema, jioni yake Jully aliingia Zanzibar. Aliungana nao kwenye hoteli ileile waliyofikia. Jioni wakiwa wanapata chakula, Jully akaanzisha mazungumzo...
“Kwanza hongereni kwa kufanikisha kufunga ndoa. Nataka kuwahakikishia kuwa, kila mmoja ni muhimu na maalum kwa mwenzake. Muishi kwa upendo, amani na kusikilizana.
“Pia nimefurahi kwamba, mimi ni mtu pekee mliyeniamini na kunipa heshima ya kuwatembelea hadi kwenye fungate yenu, ahsanteni sana ndugu zangu,” akaanza kusema Jully.
“Usijali kaka, tupo pamoja. Wewe ni mtu muhimu, maana bila wewe ilikuwa vigumu sana kumpata Laura.”
“Ni kweli. Ila kuna jambo ambalo lazima niliseme kwa ukweli wa moyo wangu, maana nisipofanya hivyo nitabaki na mateso makubwa sana moyoni. Hiyo ndiyo sababu iliyonifanya nifunge safari kutoka  Moshi hadi Dar kufuatilia kuhusu harusi yenu na hatimaye nikahudhuria.
“Kuna jambo nimewafanyia, siyo zuri. Siyo la kiungwana hata kidogo, nataka kuwa mkweli kwenu, lakini nawaomba kabla sijaanza kusema, mkubali kunisamehe kwa nilichowafanyia kwanza,” akasema Jully, sasa akianza kutokwa machozi.
Wote wakamshangaa.
Jully akamgeukia Laura, akamwambia: “Laura tafadhali naomba unisamehe!”
Laura hakumjibu, akamgeukia mumewe na kumwangalia kwa makini, akamwonesha ishara kuwa, akubali kumsamehe ili wamsikilize mpaka mwisho.
Laura akatingisha kichwa.
“Ahsante. Je, Chris nawe utanisamehe?” Akauliza Jully.

Je, Jully amefanya jambo gani? Usikose
Powered by Blogger.