ad

ad

NILIUA KUMLINDA MAMA YANGU - 16 (MWISHOOO)



 
Hapo, mambo yakaanza upya, kesi ikaanza kusikilizwa mahakamani huku waandishi wa habari wakiifuatilia kwa umakini kabisa. Madai ya Anita yaliwashangaza watu wengi, wengi wakashtuka kwani hawakutegemea kama kuna siku kungekuwa na mwanamke angeibuka na kudai kwamba mali zote alizokuwa nazo bwana Kambani ambazo kwa wakati huo zilikuwa chini ya familia yake zilikuwa zake.
“Una uhakika nitashinda kesi hii?” aliuliza Anita, alikuwa akimuuliza mumewe.
“Utashinda tu, wala usihofu.”
“Nashukuru kwa kunitia moyo!”
“Tupo pamoja.”
Kesi iliendelea kuunguruma, walichokifanya mahakimu ni kupitia mafaili ya kipindi cha nyuma kabisa, jinsi mafaili yalivyoonyesha, kulionekana kuwa na mianya mingi ya rushwa hivyo kuanza kuisimamia tena kesi ile.
Mawakili kutoka pande zote mbili wakawasilisha hati za umiliki wa nyumba na biashara mbalimbali, hati hizo zikafikishwa kwa hakimu ambaye alitaka kuangalia pamoja na baraza lake la wazee.
Siku hiyo, kesi ikaahirishwa tena na kutakiwa kusomwa tena baada ya wiki mbili. Kila siku ilikuwa ni kuahirisha kesi hiyo ila baada ya miezi miwili, hukumu ikatolewa kwamba zile hati ambazo familia ya bwana Kambani iliziwakilisha mahakamani, zilionekana kuwa na kasoro nyingi na hazikuwa halali kabisa, ila hizi ambazo alizipeleka Anita, zilikuwa ni za halali na zilionyesha kwamba yeye ndiye alikuwa mmiliki halali wa mali hizo.
“Mmiliki halali wa mali hizo ni bi Anita Philip..” alisema hakimu, bi Anita akashindwa kuvumilia, hapohapo akaanza kurukaruka kwa furaha.
Maisha yakaanza upya, mali hizo aliachiwa Anita aziendeleze kama kawaida huku mume wake, bwana Philip akiendelea kuwa nchini Madagaska. Hakutaka kurudi tena nchini Tanzania, kila kitu, hasa maisha yake yangeendelea kuwa hukohuko nchini Madagaska.
*****
“Kweli duniani wawiliwawili...”
“Kwa nini?”
“Mmh! Nilikutana na msichana kama wewe!”
“Wapi?”
“Kwa bosi wangu! Yaani kama wewe...”
“Yupo wapi?”
“Sikumfuatilia sana mara baada ya bosi mwenye kuuawa, nilichanganyikiwa ati mpaka nikawa namuita kwa jina lako...” Joshua alimwambia Cynthia.
Muda wote waliokuwa Joshua alionekana kuwa na furaha, kila alipomwangalia msichana wake, Cynthia, kumbukumbu za msichana aliyekutana naye kwa bwana Kambani zilimjia kichwani mwake.
Alikuwa Cynthia huyohuyo lakini hakuweza kuligundua hilo kwa kuwa mpenzi wake huyo aliamua kumficha. Kilichotokea baada ya kukaa kwenye uhusiano kwa muda wa mwaka mzima, hapo ndipo wawili hao walipopanga kuoana kama walivyopanga kipindi cha nyuma.
Hilo halikuwa tatizo, kila mmoja alikuwa tayari na baada ya kutambulishana kwa wazazi, wawili hao wakafunga ndoa kwenye kanisa la St. Patrick lililokuwa Masaki jijini Dar es Salaam.
Siri ya kuwa mpelelezi kutoka nchini Madagaska iliendelea kubaki moyoni mwake, hakutaka kumwambia mumewe. Kwa upande wa pili, mpelelezi Cosmas aliendelea kupeleleza lakini kila alipokuwa akifikia, hakuweza kuendelea, hakupata ushahidi wowote ule, kila sehemu aliyokuta mwili wa marehemu, hasa wale mabilionea, hakukuwa hata na alama za vidole.
Alichanganyikiwa, baada ya miaka miwili ndipo akapokea barua pepe iliyomwambia kwamba alitakiwa kuachana na kila kitu kwani kuuawa kwa watu hao kulikuwa na mpango kabambe nyuma, hasa kuua mizizi ya biashara ya madawa ya kulevya.
Hakujua barua pepe hiyo ilitoka wapi ila alipoifuatilia sana, aliona ikiwa imetoka katika shirika kubwa la kijasusi nchini Marekani, CIA hivyo akaamua kufunga mafaili yake na kusafiri tena kwenda nchini Marekani kula bata kama kawaida yake.
Huku nyuma, kila kitu kilichotokea kilisahaulika, mapenzi motomoto kati ya Philip na Anita yalirudi tena, binti yao aliwafanya kuwa na furaha siku zote, kazi kubwa aliyokuwa amepewa, aliifanya kwa kiasi kikubwa na hakutaka kujishughulisha na bwana Marimba ambaye alikuwa nyumba ya nondo.
Yote hayo, mauaji aliyofanya, alifanya kwa kuwa alimlinda mama yake ili hapo baadaye asije kuuawa na watu hao walioonekana kuwa na roho mbaya.
Cynthia na mumewe waliishi nchini Tanzania kwa miaka miwili kabla ya kuamua kuhama na kuhamia nchini Madagaska ambapo wanaishi huko mpaka leo hii.

MWISHOOO

No comments

Powered by Blogger.