ad

ad

NYUMA YA MACHOZI - 30


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
Usiku yalifanyika mauzo ya nyumba za Deus na magari yake tena mbele ya mwana sheria wa mnunuzi. Baada ya makabidhiano walikubaliana waondoke kesho yake, usiku wa siku ile walijiandaa kwa safari ya siku ya pili. Siku ya pili baada ya maandalizi muhimu walimchukua mtoto wa kwenda kumuacha nje ya gereza na kuelekea Mwanza kuanza maisha mapya.
SASA ENDELEA...
***
Ndani ya gereza Deusi Ndonga akiwa amejiegemeza kwenye ukuta huku maumivu ya moyo wake yalikuwa makubwa zaidi ya yale ya kufungwa gerezani miaka saba. Lakini kitendo cha usaliti wa mkewe Mwaka mmoja toka aingie gerezani kilimuuliza zaidi.
Akiwa bado kaegemea ukuta macho katazama juu alipata ujumbe anaitwa kwa mkuu wa gereza na kwenda kukutana na taarifa zilizozidi kumuumiza na kutamani ardhi ipasuke na kummeza.
Deus alimalizia simulizi ndefu sana iliyochukua zaidi ya saa mbili, baada ya simulizi ndefu kwa mkuu wa gereza ya sababu ya yeye kuingia gerezani na kusalitiwa na mkewe na rafiki yake kipenzi Kinape. Mkuu wa gereza aliyekuwa akimsikiliza kwa makini alijikuta akitokwa na machozi ya uchungu bila kujua.
(Kwa wasomaji wapya yote hii ni simulizi ya Deus aliyokuwa akimuhadithia Mkuu wa Gereza mwanzo wa hadithi hii baada ya mtoto wake aliyeambatana na barua kuletwa gerezani na mkewe Kilole aliyekuwa tayari ana ujauzito wa rafiki yake kipenzi Kinape.)
Mkuu wa gereza baada ya kumsiliza alishusha pumzi ndefu na kusema kwa sauti ya huruma:
“Pole sana Deus.”
“Sijapoa kila dakika maumivu moyoni mwangu yanazidi mara dufu.”
“Ni kweli, lakini wanaume tumeubwa kukabiliana nayo.”
“Ni kweli lakini inauma sana.”
“Nina imani hawa washenzi wapo nyumbani kwako?”
“Ndiyo mkuu.”
“Sasa hivi nitaomba msaada wa polisi wakamatwe mara moja.”
“Nitashukuru, japo sikupenda tufikie huko zaidi ya kutupatanisha.”
“Deus usiwe mjinga kwa hatua hii hakuna suruhu.”
“Sawa mkuu, utakachofanya chochote sawa.”
Mkuu wa gereza alipiga simu kwa mkuu wa jeshi la polisi na kumweleza kwa ufupi mkasa ule na kuomba msaada wake. Alimuhadi baada ya muda atampa jibu. Deus aliombwa arudi gerezani na mwanaye kwa kipindi kile atakuwa nyumbani kwa mkuu wa gereza.
Deus alirudi kichwa chini machozi na makamasi yakimtoka kama mtoto mdogo. Kila dakika kwake aliiona ni mateso mazito na kujiuliza baada ya yale kipi kinafuata. Alipofika alirudi sehemu yake na kuendelea kuegemea ukuta macho alitazama juu lakini hakuna alichokiona zaidi ya maumivu makali ya moyo aliohisi unavuja damu.
Mkuu wa gereza aliletewa majibu ambayo aliamini lilikuwa pigo lingine mujarabu kwa Deus. Taarifa zilizotoka polisi ni kwamba Kilole mke wa Deus aliuza nyumba na magari yote na kuondoka. Ila taarifa ilisema itafanya uchunguzi watu hao wapo wapi.
Mkuu wa gereza alijikuta akipata wakati mgumu wa kumweleza Deus unyama mwingine aliofanya mkewe. Lakini hakuwa na jinsi alimtuma mtu amwite ili ampe taarifa ambazo aliamini lazima awepo daktari la sivyo wangempoteza.
Kabla ya kumwita Deus kumpa taarifa za nyumbani kwake, mkuu wa gereza alimwita daktari mkuu wa gereza na kumwelezea taarifa zile na kumuomba awe karibu kama tukio lolote litatokea aweze kutoa huduma ya kwanza.
Baada ya kumwita daktari, mkuu wa gereza alimtuma mtu amfuate Deus gerezani.
Deus alikuwa amejiegemeza kwenye ukuta wa chumba cha gereza akiwaza na kuwazua aliyofanyiwa na mkewe Kilole na rafiki yake kipenzi Kinape. Maumivu aliyokuwa akiyapata alitamani dunia imfukie akiwa mzima baada ya kuamini hana thamani yoyote.
Alirudisha kumbukumbu jinsi alivyomsaidia Kinape na pia familia ya mkewe Kilole, hakutegemea kama wangemtendea unyama kama ule. Alishtuliwa na sauti ya kuitwa, alinyanyuka na kusogea mlangoni alikukutana na askari:
“Mheshimiwa unaitwa na mkuu.”
“Sawa,” alijibu kwa sauti ya chini.
“Nifuate,” Deus alimfuata bila kusema kitu akiamini Kilole na Kinape watakuwa wamekamatwa. Moyoni hakupenda Kilole akamatwe kwa ajili yake kwa kuamini bado ana nafasi nyingine kwake.
Aliongozana na askari mpaka nje ya ofisi ya mkuu wa gereza, kutokana na maelezo ya mkuu kwa secretary wake, walipofika aliruhusiwa kuingia ofisini.
“Deus unaweza kuingia,” secretary alimwambia Deus.
Deus aliingia ofisini kwa mkuu na kumkuta akimsubiri.
“Karibu Deus.”
“Asante mkuu,” Deus alijibu kwa sauti ya chini.
“Kaa kwenye kiti,” Deus alikaa na kutulia kumsikiliza mkuu wa gereza.
Kabla ya kusema mkuu wa gereza alimtazama Deus na kumuonea huruma kwa kuamini moyoni mwake kuna mateso mazito, lakini hakuwa na jinsi zaidi ya kumwambia ukweli.
“Deus,” mkuu alimwita kwa sauti ya upole.
“Naam mkuu.”
“Najua moyoni mwako upo katika hali gani, lakini kama mwanaume unatakiwa kupambana nayo.”
“Ni kweli, lakini nimeshtukizwa sana.”
“Ukiwa mwanaume unatakiwa kukabiliana na yote, siku zote mwanaume ni mpambanaji na kutatua matatizo mazito.”
“Ni kweli kabisa mkuu, lakini nitawezaje kukabiliana nayo wakati nipo gerezani?”
“Unatakiwa kuachana na mambo ya nje ya gereza ili utumikie kifungo chako ukitoka utakuwa na nafasi ya kukabiliana nayo. Lakini ukiwa humu ndani na kufikiria ya nje yatakuchanganya.”
“Najitahidi kufanya hivyo lakini kila dakika linazuka zito kuliko la mwanzo.”
“Yote hiyo ni mitiani ya maisha unayotakiwa kuikabili hakuna maumivu unayoweza kupokewa na mtu.”
“Nimekuelewa mkuu, vipi wamepatikana?”
“Kuna taarifa zisizo nzuri, lakini unatakiwa nazo kuzipokea kama mwanaume.”
“Taarifa gani?” Deus aliuliza huku moyo ukimlipuka.
“Mkeo ameuza kila kitu.”
“Ameuza kila kitu una maana gani sijakuelewa?”
“Mkeo ameuza nyumba na magari yote.”
“Sasa yeye kakaa wapi?” Deus aliuliza swali la kizuzu.
“Siwezi kujua.”
“Mkuu unasema kweli au unatania?”
”Ni kweli kabisa kutokana na taarifa za kipolisi kuwa zilizofika nyumbani kwako kumekutwa mtu mwingine ambaye amenunua kila kitu jana usiku. Kwa maana hiyo mkeo hajulikani hayupo ila kauza kila kitu.”
“Ooh! Mungu,” Deus alisema na kujilaza nyuma ya kiti na kuseleleka mpaka chni alipotua kama mzigo.
Mkuu alijitahidi kumuwahi lakini alichelewa Deus alikuwa amekwishafika chini, alipomuangalia alikuta amepoteza fahamu. Haraka alimwita mganga mkuu ambaye hakuwa mbali na kuja kumpa huduma ya kwanza Deus aliyekuwa hajitambui.
Walimpatia huduma ya kwanza lakini haikuweza kumsaidia Deus ambaye viungo vya upande mmoja vilionesha kupoteza mawasiliano.
“Mkuu hali ni mbaya,” dakta Fukwa alisema huku akijifuta jasho kutokana na kujitahidi kwa muda mrefu kuokoa hali ya Deus bila mafanikio.
“Sasa tutafanyaje?”
“Hatuna ujanja, tumuwahishe Muhimbili.”
“Basi tufanye haraka.”
Mkuu wa gereza aliiita gari la wagonjwa lililofika na kumchukua Deus kumuwahisha Muhimbili kupata huduma kubwa. Gari lilimchukua haraka na kumkimbiza hospitali. Walipofika Muhimbili bado Deus alikuwa hajitambui alichuliwa haraka na kukimbizwa chumba cha wagonjwa mahututi.
Baada ya kupokelewa alipatiwa huduma ya haraka ili kuokoa maisha yake, walifanikiwa kuyashtua mapigo ya moyo yaliyokuwa yakipungua kila dakika na kuweza kumwekea mashine za kupumulia.
Deus alipata ufahamu wa mbali baada ya siku mbili sehemu moja ilikuwa na mawasiliano lakini upande wa pili imepoteza mawasiliano. Hali ile ilimfanya akae hospitali zaidi ya miezi mitano kutokana na kujaribu kuutibu ugonjwa wa kupoteza mawasiliano mwilini.
****
Kilole na Kinape baada ya kufika jiji Mwanza na kukaa kwenye nyumba ya wageni huku wakijipanga kutafuta kununua nyumba ya kuishi. Kwa vile walikuwa na fedha waliweza kupata nyumba nzuri maeneo ya shule Isamilo. Haikuchukua muda mrefu walifungua maduka makubwa ya kuuza vitu vya jumla na rejareja mtaa wa Liberty.
Kwa muda mfupi maisha yao yalibadilika kutokana na kufahamika haraka kutokana na uwezo wao wa kifedha. Gari walilosafiri nalo toka Dar waliliuza na kununua lingine. Wakati huo Kilole alikuwa amejifungua mtoto wa kike waliyempa jina la Gift.
Pamoja na kufanyiwa yote yale Kinape bado alikuwa na kisasi kizito moyoni mwake cha kuuawa mpenzi wake Happy bila sababu. Kila dakika aliyokuwa peke yake alimkumbuka mpenzi wake na kupanga kumfanyia kitu kibaya Kilole ambacho hata sahau maishani mwake.
Kilole upande wake aliamini Kinape anampenda sana na ndiye mwanaume wake sahihi maishani mwake. Alipanga kumpigania kwa nguvu zote kuhakikisha hampotezi alikuwa radhi kuendelea kutoa roho ya kiumbe yeyote wa kike atakayemsogelea karibu mpenzi wake.
*****
Teddy baada ya kutoka Kenya alikwenda kujificha nchini Ujerumani katika jiji la Hamburg katika hotel ya nyota nne ya Senator. Lakini pale alikaa wiki tatu na kupewa taarifa za tahadhari kubwa. Akiwa amejipumzisha chumbani kwake alipata simu toka kwa bosi wa kikundi Double D.
“Haloo Teddy upo wapi?”
“Kwa sasa sitaki kumjulisha mtu nipo wapi wacha nipumzike.”
“Teddy kuwa serious kuna kitu kibaya kinakukabiri.”
“Kitu gani? Acha kunitisha?” Teddy aliamini ni utani.
“Mose anakutafuta ile mbaya amefika Kenya kwenye chimbo lako na kukukosa alikuja Dar na kuniuliza juu yako lakini nilisema sijui chochote. Inaonesha kuna mtu katika kundi letu anawasiliana na Mose na kumwambia mimi nafahamu kila kitu kuhusiana na wewe pamoja na kumkatalia lakini alinihakikishia lazima akutie mikononi.”
“Hawezi kujua nipo wapi,” Teddy alisema kwa kujiamini.
“Kuna taarifa kuwa upo Ujerumani.”
“Nani kawaambia?” Teddy alishtuka.
“Mtu akitaka kumkamata mtu hashindwi, nimekueleza toka awali kuwa mtu yule anajiamini sana kuna kitu anakitegemea ndiyo maana alifuta ushahidi wa kukutia hatiani ili alipe kisasi kwa mkono wake.”
“Kwa hiyo Mose anajua nipo huku?”
“Ndiyo.”
“Mmh! Nani kamwambia nini nipo huku?” Teddy hakuamini kusikia vile.
“Wewe si unaona unafanya siri lakini mambo yako mengi yapo nje, kuwa makini badili mfumo wako wa maisha la sivyo utapotea.”
“Kwa hiyo Mose sasa hivi yupo wapi?”
“Kwa taarifa nilizozipata sasa hivi Mose na kundi lake wapo Ujerumani tena katika mji wa Humburg.”
“Muongo! Acha utani.”
“Sasa hivi anafanya msako wa Hotel zote za nyota tano.”
“Mungu wangu, sasa nifanyeje?” Teddy alichanganyikiwa.
“Fanya uwezavyo uondoke sasa hivi la sivyo mpaka kunapambazuka jina lako litabakia simulizi midomoni mwa watu.”
“Niende wapi?”
Itaendelea

No comments

Powered by Blogger.