NYUMA YA MACHOZI - 31

MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
“Kwa taarifa nilizozipata sasa hivi Mose na kundi lake wapo Ujerumani tena katika mji wa Humburg.”
“Muongo! Acha utani.”
“Sasa hivi anafanya msako wa Hotel zote za nyota tano.”
“Mungu wangu, sasa nifanyeje?” Teddy alichanganyikiwa.
“Fanya uwezavyo uondoke sasa hivi la sivyo mpaka kunapambazuka jina lako litabakia simulizi midomoni mwa watu.”
“Niende wapi?”
SASA ENDELEA...
“Fanya hivi, rudi nchi yoyote ya Afrika nina imani kwake akikukosa atakutafuta kwenye nchi za Ulaya au Marekani. Ukiwa Afrika hata kama msaada wangu utahitajika nitaweza kuja kukusaidia.”
“Sasa Afrika niende nchi gani? Maana sasa hivi nimeingia woga.”
“Sitaki kukueleza nenda nchi gani wala sitaki kujua atakuwa wapi la muhimu ondoka sasa hivi ukichelewa shauri yako.”
Teddy alipakia vitu vyake kwenye begi na kuondoka usiku uleule aliona heri aende moja kwa moja nchini Ghana. Aliamua kukaa palepale mjini Accra katika hotel ya nyota mbili ya East Gate iliyopo maeneo ya East Legon.
Taarifa za kusakwa kila kona ya dunia na Mose ilimchanganya sana na kuona muda si mrefu atamtia mikononi na kumuua.
Wazo lililomjia ni kwenda kubadili sura ili aweze kumkwepa Mose japo hakupenda katika maisha yake kuibadili sura yake. Kutokana na kuona vita ni kubwa pamoja na kumkimbia bado hakutakiwa kukubali kirahisi kushindwa zaidi ya kupambana.
Siku zote aliamini mwindaji hujiamini kuliko anayewindwa naye aliona ile ndiyo nafasi yake maye kuanza kumwinda taratibu. Akiwa chumbani kwake amepumzika kama ilivyokuwa kawaida yake kupenda kutoka usiku na mchana kutulia chumbani kwake.
Alipenda sana muda ambao hakuwa na kazi za kufanya kucheza game na alipochoka alilala. Kuhakutaka kufanya chochote kwa wiki mbili ili kupumzisha akili na kuchunguza Mose atakuwa wapi ili asikurupuke na kujiingiza katika mdomo wa mamba.
Baada ya wiki mbili kukatika akiwa amejipumzisha chumbani kwake alipatwa na mshtuko baada ya kuona taarifa za kushtusha za kifo cha bosi wake mtu aliyekuwa akimtegemea Double D aliyeuawa na baadhi ya washirika wenzake aliouawa kinyama habari na picha zilizorushwa na shirika la habari la CNN. Yalikuwa mauaji yalioutikisa jiji la Dar na nchi ya Tanzania.
Teddy alichanganyikiwa ilibidi ampigie simu Jimmy aliyekuwepo Italia kuhusiana na kifo cha Double D na baadhi ya washirika. Baada ya kuipokea kwanza Jimmy alionesha kushtuka na kuuliza:
“Ha! Teddy upo salama?”
“Jimmy nipo salama kwani vipi?”
“Hali ni mbaya Mose kawa mbogo anaua ovyo.”
“Unataka kuniambia yeye ndiye aliyemuua Double D na kina Tony?”
“Ndiyo.”
“Kwa sababu gani?”
“Kwa ajili yako.”
“Kwa ajili yangu ndiyo awaue?”
“Kwa taarifa zilizonifikia baada ya Mose kujua amejificha wapi nchini Kenya, alipofika na kukukosa. Inasemekana aliyekushtua ni Double D, nasikia walikoromeana sana kuhusiana na yeye kukushtua na kuweza kutoroka kiasi cha kutishiana maisha.
“Baada ya Mose kukufuatilia aligundua upo Ujerumani katika jiji la Humburg alifika mara moja na kundi lake, lakini hakufanikiwa kukuona. Kuna mtu katika kundi sijui nani alimweleza kuwa Double D ndiye aliyekubumburusha na kutoroka tena.
“Kitendo kile kilimkasirisha sana Mose na kumfuata Double D na kuchimbana mkwara katika kujitupiana maneno Double D alimpiga Mose kama mdogo wake. Mose hakukubali alimtolea bastora na kumlipua kila aliyetaka kumsaidia naye aliuawa kisha walitoroka.”
“Mmh! Kazi ipo sasa hivi Mose yupo wapi?”
“Amerudi Italia.”
“Na ana mpango gani na mimi?”
“Siwezi kujua nataka nikuambie kitu kama anataka kumkimbia Mose nenda Tanzania kwa sasa kwa vile hawezi kwenda kwa kuhofia kukamatwa.”
“Nitajua mwenyewe niishi wapi lakini wapi nitakuwepo itabakia siri yangu ila nashukuru kwa ushauri wako.”
“Take care, Mose kapagawa kawa kama mbwa mwenye kichaa anamuua kila ajae mbele yako sijui akikushika itakuwaje anaweza kukula nyama mbichi.”
“Nimekuelewa Jimmy.”
Baada ya kukata simu Teddy alijitupa kitandani na kuamini yupo kwenye wakati mgumu na Mose. Pamoja na kuua na kukimbia bado alijua atazidi kumtafuta huenda kamtumia Jimmy ili aweze kumtia mikononi. Lakini bado hakutaka kuitoa siri nje atakufa nayo.
Akiwa amejilaza kitandani macho akitazama juu alijikuta akiingiwa na hofu kubwa ya kifo cha Double D na kina Tony kilimchanganya sana na kuamini kama wale watu aliowategemea wameuawa na Mose yeye asingekuwa kitu kwake.
Alijilaumu sana kumbakiza duniani na kujiuliza alikosea sehemu gani iliyomfanya Mose aendelee kuwa hai. Aliona kuna umuhimu wa kutafuta jeshi la kumuongezea nguvu kuweza kukabiliana na Mose na kundi lake lililomtishia maisha.
Hakutaka kuendelea kumkimbia zaidi ya kujibu mapigo kwa yeye naye kuanza kumwinda adui yake. Wazo la haraka lilimjia lilikuwa kurudi Tanzania kumtafuta Deus kufanya kila awezalo kumtoa gerezani aweze kumsaidia kwa vile alionekana ni mtu mwenye uwezo mkubwa sana wa kutumia siraha kutoka na historia yake aliyoipata toka kwa aliyekuwa sekretary wake.
Deus alichaguliwa kujiunga na kitengo cha kupambana na madawa ya kulevya kutokana na utukutu wake na uwezo wa kutumia siraha za moto na mikono kwa ufasaha mkubwa.
Teddy aliona kuna haja ya kutumia kiasi chochote cha fedha kumtoa Deus gerezani. Wakati akiwaza hayo muda huo ndiyo Deus alikuwa akitoka hospitali baada ya kupata nafuu kubwa ya kumwezesha kuendelea na kifungo kilichobakia.
Pamoja na kurudi gerezani bado kazi ngumu hakuweza kuzifanya, mkuu wa gereza alipanga katika watu watakaopata msamaha wa rais basi mmoja wapo atakuwa Deus. Aliapa kumsaidia Deus mpaka atakapomtoa gerezani kwa kumpa upendeleo wa pekee kwa kula chakula kizuri hata sehemu yake ya kulala ilikuwa nzuri.
*****
Teddy aliteremka kwenye gari ka kifahari nje ya gereza la segerea na kwenda moja kwa moja kwenye ofisi za gereza na kuomba kuonana na mkuu wa gereza. Baada ya kujulishwa alimruhusu apelekwe ofisini.
“Karibu bibie,” Mkuu wa gereza alimkaribisha msichana mrembo.
“Asante mzee wangu, shikamoo.”
“Marahaba.”
Baada ya Teddy kukaa ulipita ukimya mfupi huku akiwa ameinama kuonesha mwingi wa aibu akichezea vidole, mkuu wa gereza alivunja ukimya.
“Ndiyo mama nikusaidia nini?”
“Nilikuwa na shida na Deus.”
“Deusiii...Deus ...yupi?” alimuuliza huku akimkazia macho.
“Mfungwa wako aliyefungwa kwa tuhuma za dawa za kulevya miaka zaidi ya miwili iliyopita.”
“Sasa mwanangu si ungekwenda gerezani tu ukamuone, huku ni sehemu ya utawala tu mama yangu,” mkuu wa gereza alimjibu kwa ustaarabu.
“Kuja huku nina sababu yangu mzee wangu.”
“Sababu gani?”
“Nataka kuzungumza naye faragha.”
“Kuhusu nini?”
“Mzee wangu ungenikutanisha naye ningefurahi sana.”
“Una muda gani hujaonana naye?”
“Mmh! Muda mrefu sana nimeondoka bado hajahukumiwa, taarifa za kufungwa nilizipata nikiwa nje ya nchi. Jana nimefika nataka kumuona na kesho naondoka haitakuwa vizuri kuondoka bila kumuona.”
“Sheria za gereza haziruhusu mtu kutembelea katikati ya siku zaidi ya kusubiri siku ya kutembelea wafungwa jumapili.”
“Naomba msaada wako nina imani utafurahi mimi kuonana na Deus pia nina mazungumzo mrefu na wewe ambayo pia nina imani tutaelewana na hutanisahau maishani mwako.”
“Wewe ni nani wake?”
“Ni mtu wake wa karibu sana.”
“Unajua yaliyomtokea?”
“Zaidi ya kufungwa sijui kingine.”
“Ni mengi yamemkuta akiwa gerezani, amekaa hospitali zaidi ya miezi sita.”
“Mungu wangu nini tena?” Teddy alishtuka.
“Alipooza mwili upande mmoja.”
“Ooh! Jesus,” Teddy alisema sauti ya kukata tamaa.
“Lakini sasa hajambo japo hawezi kufanya kazi nzito.”
Teddy aliinama na kujikuta akipoteza tumaini alilolitegemea bila kutarajia machozi yalimtoka. Hali ile alioona mkuu wa gereza na kuamini kweli yule mtu wake wa karibu aliyeguswa na tatizo la Deus.
“Pole sana binti.”
“Asante, inauma sana kwani nini kilimsibu mpaka kuwa hivyo?”
“Ni historia ndefu ya kusikitisha ya kutoa machozi kwa vile mwenyewe yupo atazungumza naye.”
Mkuu wa gereza alimtuma mtu kwenda kumwita Deus gerezani, Deus alikuja akiwa na maswali mengi kwani kila alipoitwa alikutana na kitu kilichouumiza moyo wake. Alipoingia ofisi ya mkuu wa gereza hakuamini kumuona mtu alimpigania kwa nguvu zote lakini alivyopotea hakujua.
“Ha! Teddy?”
“Ni mimi Deus pole sana.”
“Asante, za siku?”
“Mmh! Wee acha tu.”
“Ukisema hivyo sisi tutasemaje?”
Mkuu wa gereza aliwapa nafasi ya kuzungumza, Teddy alitaka kujua nini kilichomsibu Deus kiasi cha kupooza mwili na kulazwa hospitali kwa miezi mingi. Deus hakumficha alimweleza yote baada ya kuondoka jinsi mkewe na rafiki yake kipenzi walivyomtenda.
Simulizi ile ilimtoa machozi Teddy na kujikuta akijifuta kamasi nyembamba na mishipa ya kichwa kumsimama.
“Amini Deus kwa maelezo yako hata zile dawa za kulevya zimewekwa na mkeo na rafiki yako nina uhakika huo kuna siku nilikwenda kwa mkeo kutafuta njia ya kukutoa gerezani. Nilimkuta mkeo anafuraha amefungulia muziki kwa sauti kubwa, nilishtuka lakini leo nimepata jibu.”
“Hata mimi naanza kuamini hivyo.”
“Kuna kitu kilinileta na kuwa tayari kutoa kiasi chochote cha fedha ili utoke tuifanye kazi moja ambayo imeniweka katika maisha ya wasiwasi. Lakini hali yako imenikatisha tamaa.”
“Kazi gani?” Deus alimuuliza akimtazama usoni
Teddy naye ilibidi aeleze mkasa toka alipokamatwa mara ya kwanza uwanja wa ndege na vijana wa Deus na kisasi achokilipa na bahati mbaya adui yake alipona kifo na kuanza kumsaka mpaka kufikia kuua sehemu kubwa la kundi lao akiwemo bosi wao Double D.
“Utani huo unataka kuniambia kikosi chote kile kimepukutika?”
“Wee acha, nimebakia mimi tu.”
“Kweli mwanaume kapania, sasa ulikuwa unahitaji msaada gani toka kwangu?”
“Msaada niliokuwa nataka tuunde jeshi la watu wawili wa kumsaka Mose na kummaliza. Lakini hali yako nina imani huwezi kutoa msaada wowote, nitakuwa nimechemka sina jinsi. Mkeo nikimuona nitamuua kwani kama nitakufa mimi sababu ni yeye.”
“Kuhusu hali yangu sasa hivi nipo sawa, ila mkuu amenieleza msamaha wa rais utakaotoka mimi nitakuwa mmoja wapo, hivyo kanieleza niendelee kuigiza bado mgonjwa ili watu waamini naumwa hata nikiachiwa wasiwe na wasi na kuachiwa kwangu.”
“Mnategemea kuachiwa lini?”
“Baada ya sherehe ya uhuru mwezi ujao.”
“Kumbe siyo mbali.”
“Siyo mbali japo sijui maisha yangu nikitoka yatakuwaje?”
“Kuhusu maisha usiwe na wasiwasi kila kitu utapata kwangu na tukifanikiwa kumtokomeza yule nduli nitakupa utajiri mara tatu ya ulioupoteza.”
“Japo najua ni kazi lakini nina imani nitamtuliza.”
“Mbona unajiamini hivyo?” Teddy alimshangaa Deus.
Itaendelea
Post a Comment