ad

ad

NYUMA YA MACHOZI - 29


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
“Jamaa amesema anajua sijui upo Kenya sijui sehemu gani, ameniahidi ndani ya mwezi maiti yako itaokotwa barabarani kwanza atakubaka kabla ya kukuua kinyama.”
“Umesema amesema nipo Kenya?” Teddy alishtuka.
“Ndiyo.”
“Mmh! Mwache aje.”
“Kuwa makini sitajisikia vizuri nikisikia umeuawa na Mose.”
“Sawa Jimmy, nakuahidi nitammaliza yeye kabla hajanigusa.”
Baada ya kumaliza kuzungumza na Jimmy simu toka Dar toka kwa bosi wake Double D iliingia.
SASA ENDELEA...
“Haloo bosi,” Teddy alipokea.
“Vipi ulifika salama?”
“Nashukuru sana Bosi.”
“Basi kuwa makini.”
“Sawa Bosi.”
“Umezipata taarifa za Mose?”
“Kuhusu nini Bosi,” Teddy alijifanya hajui kitu.
“Leo amekusafisha kwa vyombo vya usalama ili alipe kisasi, sasa mama vita vya ndani sijui umejiandaa vipi?”
“Mkuu utanisaidia vipi?”
“Siwezi kuingilia ugomvi wa ndani, ni wewe kuwa makini kwa vile Mose ni mwenzetu.”
“Nimekuelewa Bosi kuanzia sasa hivi nitajua niishi vipi naweza nisionekane tena mpaka nitakapomtia mkononi Mose,” Teddy alijibu mapigo.
“Kwa hiyo na wewe unamtafuta?”
“Nimsubiri animalize, vita siku zote mfuate adui yako, nitatafuta nchi yoyote kuweka kambi ili nimsake hayawani yule wa kiume mbakaji mkubwa.”
“Na biashara?”
“Sasa hivi nasimamisha kwa ajili ya msako wa huyu hayawani anayetafuta vita na mimi.”
“Lakini Mose yupo sawa,” Double D alimtaadharisha Teddy.
“Namjua vizuri lakini siwezi kumkimbia akiniwahi basi lakini nitamfanya kitu kibaya zaidi ya kile cha mwanzo.”
“Basi kuwa makini, sipendi kukupoteza kwa vile wewe ni mtu muhimu sana.”
“Sasa bosi kwa nini usinisaidie kummaliza.”
“Msaada labba kukuelekeza sehemu salama, lakini zaidi ya huo siwezi kumbuka kumgeuka Mose sawa na kumsaliti kaka yake ambaye kwangu alikuwa zaidi ya ndugu, nafikiri unafahamu kitu hicho?”
“Nafahamu Bosi sina jinsi lakini sifi kikondoo patachimbika,” Teddy alijihami.
“Sasa ukihitaji msaada wowote utaniambia.”
“Sawa bosi.”
Baada ya kukata simu Teddy aliona kimenuka kwani hakukuwa na msaada wowote wa kumlinda kutokana na Mose kuwa ni mwana kikundi na kaka yake aliyekuwa bwana ya Teddy kuwa ndiye mwanzilishi wa kundi lile. Sifa ya kundi lile lilikuwa haliingilii mgomvi wowote wa ndani hata kuuana.
Ilikuwa lazima aondoke chimbo alilojificha baada ya kusikia Mose analifahamu, kwake ingekuwa rahisi kuwakimbia polisi wa Italia hata kwa kubadili sura lakini kwa Mose ingekuwa vigumu zaidi ya kutafutana.
Kilichokuwa kikimtisha zaidi ni uwezo wa hali ya juu wa Mose kundini katika mapigano, ndiye aliyekuwa akitumiwa kuwaua watu waliokuwa wakiweka kauzibe katika biashara zao. Hivyo suala la kuua kwake lilikuwa sawa na kuzima kibatari.
Aliamini kesi ya Deus haina nguvu alijipanga kuondoka mafichoni na kwenda nchi yoyote ambayo aliamini inamfaa kwa muda ule ili kujipanga kumsaka anayemsaka.
*****
Jiji Dar kesi iliyokuwa ikimkabiri Deus iliahilishwa kutokana na kifo cha mkuu wa kitengo cha madawa ya kulevya ambaye ndiye aliyekuwa shahidi wa mwisho. Baada ya mwezi mmoja hukumu ilitolewa na Deusi kufungwa miaka saba kutokana na kuonekana kuhusika kwa njia moja ama nyingine japo ushahidi haukumtia hatiani kwa asilimia mia.
Baada ya hukumu mkewe Kilole alilia sana kuonesha kuumizwa sana na hukumu ile. Kinape alishangaa kilio cha Kilole, lakini moyoni alimshukuru sana Teddy kuweza kupunguza ukali wa kesi ile ambayo ungefanya Deus aozee gerezani.
Baada ya hukumu Deus alichukuliwa na kupelekwa gerezani kutumikia kifungo cha miaka saba. Aliondoka akijua kilio cha mkewe kilionesha jinsi gani ameiachia familia yake maumivu makali. Lakini haikuwa kama alivyofikiria, nyuma ya machozi ya mkewe kulikuwa na kicheko cha furaha cha kummaliza.
Mumewe akiwa gerezani Kilole alianza kupanga mipango ya kummaliza kabisa ili akimaliza kifungo chake asikute kitu. Cha kwanza alitaka kumuua mtoto aliyezaa na Deus kitu alichokikataa Kinape kwa nguvu zote.
“Sawa tumemfanyia unyama Deus unataka kumuua mtoto wake kwa kosa gani? Kwanza kumbuka hii ni damu yako.”
“Ni kweli, lakini anaweza kunigeuka akipata akili na kujua mimi ndiye niliyemfanyia yale baba yake.”
“Tafuta njia nyingine lakini si kumuua.”
“Sina njia nyingine zaidi ya kumua, nataka mimi na wewe tuanze upya maisha yetu yawe na mtoto wetu wenyewe.”
“Kwa hilo sikubaliani nalo.”
“Sasa tufanyeje?”
“Huyu atakaa hapahapa kama mtoto wako na tutampa matunzo yote na chochote kibaya utachokifanya sitakuwa na suruhu ya kuendelea kuwa na wewe.”
“Sawa nitafanyaje lakini simpendi hata kumuona,” Kilole alionesha jinsi gani alivyona roho mbaya hata kwa damu yake.
“Kama unaichukua damu yako mimi utanipenda vipi?”
“Hapana Kinape nakupenda kuliko nafsi yangu.”
“Basi kama unanipenda mpende huyu mtoto mara mbili yangu.”
“Nitafanya hivyo kwa ajili yako mpenzi.”
MIEZI SABA BAADAYE
Katika mapenzi yao haramu Kilole alishika ujauzito Kinape, hapo ndipo Kilole hakutaka kukubaliana na Kinape kuhusiana kuendelea kuwa na mtoto wa Deus. Lakini bado Kinape alikuwa na msimamo makali ikiwa pamoja na kumlazimisha kwenda kumuona Deus gerezani. Kilole kwa vile alikuwa akimpenda sana Kinape alikubaliana naye kwa shingo upande.
Mimba ilipoaanza kuonekana alimkataza lakini alikwenda nayo hivyohivyo na kushtua Deus ambaye hakuamini mkewe kumsarti.
“Mke wangu hii si mimba?” Deus alishtuka kumuona mkewe aliyemuacha akiwa hana kitu ana ujauzito mkubwa ambao si wake.
“Kweli gereza baya, kama kusoma hujui hata kuangalia picha huwezi,” Kilole alijibu kwa nyodo.
“Una maana gani mke wangu?”
“Hii ni mimba mume wangu.”
“Ya nani?”
“Ya kwako.”
“Si kweli, nimekuacha huna kitu na wala hukuwahi kuniambia una ujauzito.”
“Sasa unafikiri ni wa nani?”
“Mke wangu mwaka na nusu kuwa gerezani umenisarti?” Deus alisema kwa sauti ya kilio.
“Sijakusaliti bali nimempata msaidizi wa kukusaidia mpaka ukitoka gerezani unikute nipo nakusubiri.”
“Mke wangu sasa hayo ni maneno gani?’
“Kwani wewe ulikuwa unatakaje?”
“Kaitoe hiyo mimba.”
“Mume wangu niue kiumbe kisicho na hatia?”
“Sasa unafikiri utazaaje mtoto asiye na baba?”
“Mume wangu kitanda hakizai haramu, mtoto ni wako.”
“Hapana mke wangu pamoja na kufanya kosa la kunisaliti naomba uitoe hiyo mimba.”
“Yaani nikae nayo miezi nane niitoe kirahisi nikifa?”
“Huwezi kufa mke wangu.”
“Hivi huyo mwanaume akisema na yeye amuue mwanao utakubali?”
“Nikubali vipi wakati wewe ni mke wangu wa halali.”
“Sikuja kwa hayo ila kukufahamisha nimepata msaidizi wa kukutunzia mkeo na mtoto nawe utumikie kifungo kwa amani na mguu huu ni wa mwisho kuja hapa.”
“Nooo, usifanye hivyo mke wangu.”
“Siwezi kutumikia mabwana wawili.”
“Huyo msaidizi ni Kinape?” Deus aliuliza huku amepiga magoti.
“Mbona umemtaja yeye ndiye uliyempa kazi ya kukulindia mkeo?”
“Hapana mke wangu, mbona unazidi kuniumiza?”
“Umejiumiza mwenyewe kwa kufanya biashara haramu kwa siri ningejua si ningeweza kuficha. Nimekutetea mahakamani bado tu unaniona sina maana.”
“Nashukuru mke wangu, lakini miaka saba siyo mingi.”
“Najua, lakini imetokea hivi unatakiwa ukubali matokeo.”
“Nimekubali lakini usiniache bado nakupenda,” Deus alizidi kuumizwa na mkewe.
“Basi habari ndiyo hiyo nikitoka leo sitarudi tena labda mwanao,” Kilole alisema huku akiondoka na kumwacha Deus amepiga magoti huku akiendelea kubembeza na machozi kumtoka.
Askari magereza alimchukua Deus na kumrudisha ndani, Deus baada ya kurudishwa ndani alijikuta kwenye wakati mgumu maishani mwake. Tokea siku ile aliishia katika maisha magumu huku akiamini yeye ni kiumbe mwenye nuksi. maumivu ya kusalitiwa yalikuwa makubwa zaidi ya yale ya kufungwa gerezani miaka saba.
Kitendo cha usaliti wa mkewe kilimuumiza sana kiasi cha kila siku kuonekana mgonjwa mpaka siku alipoitwa na mkuu wa gereza kumkuta mwanaye ofisini na barua yake nzito toka kwa mkewe.
****
Kupelekwa kwa mtoto wa Deus gerezani kulifikiwa baada ya mvutano mkali kati ya Kilole na Kinape juu ya kauli ya Deus ya kumlazimisha kuutoa ujauzito wa Kinape uliokuwa na miezi minane.
“Hata kama alitaka kuutoa ujauzito huo bado alikuwa na haki ya kusema vile kwa vile wewe ni mkewe.”
“Komea hapohapo toka alipofungwa mume wangu ni wewe hivyo na mtoto wake naye hafai kuendelea kuishi.”
“Kwa hilo sitakuelewa.”
“Sasa nasema hivi kama hutaki tumuue huyu mtoto nitamuua kisha nitajiua na mimi.”
“Kwanini umuue, basi tumpeleke wa wazazi wake kijijini?”
“Siwezi.”
“Basi mpeleke gerezani kwa baba yake.”
“Nitampelekaje?”
“Mpeleke na kumuacha nje ya gereza na barua mkononi askari wakiumuona watamchukua na kuisoma lazima taarifa zitamfikia.”
“Huo si ujinga wakija hapa si nitafungwa.”
“Ule mpango umekamilika, nimepata mununuzi wa nyumba na magari.”
“Mbona hukuniambia?”
“Nilikuwa nikuambie leo.”
“Kwa hiyo nitampeleka baada ya kuuza kila kitu.”
“Tutabakia na Toyota Land Cruiser tutayoitumia kuuhama mji.”
“Tunakwenda wapi?”
“Mwanza.”
“Ushawahi kufika?”
“Sijawahi, lakini nasikia ni mji unakaribiana na Dar kwa ukubwa na mzunguko wa fedha.”
“Hakuna tatizo, mauzo saa ngapi?”
“Usiku wa leo.”
Usiku yalifanyika mauzo ya nyumba za Deus na magari yake tena mbele ya mwana sheria wa mnunuzi. Baada ya makabidhiano walikubaliana waondoke kesho yake, usiku wa siku ile walijiandaa kwa safari ya siku ya pili. Siku ya pili baada ya maandalizi muhimu walimchukua mtoto wa kwenda kumuacha nje ya gereza na kuelekea Mwanza kuanza maisha mapya.
Itaendelea

No comments

Powered by Blogger.