NYUMA YA MACHOZI- 27

MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
Baada ya mazungumzo walimtoa mzee Shamo wakiwa njiani kumrudisha walimvutisha dawa ya kulevya zilizomlevya na kulala, kwa vile ilikuwa usiku walimrudisha jirani na hoteli Sea Cliff kumuacha sehemu iliyo salama na kurudi kujipanga upya.
SASA ENDELEA...
*****
Mzee Shamo aliokotwa pembeni ya hoteli ya Sea Cliff akiwa hajitambui na kukimbizwa hospitali kupata huduma ya haraka. Alipata nafuu baada ya siku mbili, alijua wale ni jamaa zake Deus ambao alikuwa akifanya nao dili la kuvusha dawa za kulevya.
Lakini alipoulizwa juu ya kuokotwa hajifahamu ilitokana na nini. Alificha kuhofia onyo kali alilopewa na Double D kama ataitoa siri nje basi wangempoteza.
Aliamini kukaa kwake kimya ndiyo salama yake, hivyo kila alipoulizwa mara ya mwisho alikuwa wapi alidanganya alitekwa na watu asiowajua na kujikuta hosipitali. “Unasema walikuteka tu bila kueleza lolote?” Afisa mwenzake alimuuliza.
“Yaani wakati nakwenda kwenye gari langu walitokea vijana na kuniteka na kunitupia kwenye gari lao na kuondoka na mimi, baada ya hapo sikujua kilichoendelea mpaka nilipojikuta hospitalini.”
“Kwa hiyo hawakukusemesha chochote juu ya kukuteka kwako?”
“Hawakunisemesha chochote.” “Sasa kwa nini walikuteka na kukuachia bila kukufanyia lolote?”
“Inaonekana huenda waliniteka kimakosa na kuamua kuniachilia baada ya kugundua si mlengwa.”
“Lakini upo sawa?”
“Nipo sawa, kutokana na maelezo ya daktari nilinusishwa dawa za kulevya tu hakuna kitu kingine kibaya.”
“Hukumbuki hata namba za gari.”
“Kwa vile nilikuwa sijui nini kinaendelea hivyo sielewi chochote.”
Mzee Shamo aliamua kificha siri ile kwa upande wake aliamini ile ni kinga tosha ya wauza dawa za kulevya ya kutommaliza.
***
Deusi alipandishwa kizimbani akikabiliwa na kosa la kukutwa na dawa za kulevya. Upande wa msaada Kinape akiweka wakili wa siri baada ya mkewe Kilole kukataa kutumia fedha zake kumwekea wakili akiamini kabisa hawezi kupona katika kesi ile lazima atafungwa kwani ushahidi wote ulikuwepo. Kutokana na kukosa msaada kwa washirika wenzake kumsaidia Deus katika kesi yake Teddy alijitosa kumsaidia kwa kuongeza wakili mzoefu wa kesi nzito kama zile.
Kwanza alibadili mavazi na kuvaa ya heshima yenye kuuficha mwili wake kisha alijipaka piko kama mwanamke wa pwani vitu vile vilimfanya aonekane mwanamke mstaarabu mbele ya jamii.
“Nahitaji msaada wako Mr Mnyigu ili nimuokoe huyu baba, kesi imemkalia vibaya,” Teddy alimuomba msaada wa wakili wa kujitegemea.
“Kutokana na maelezo ya mtuhumiwa kesi imekaa vibaya hasa baada ya ushahidi kukutwa ndani mwake.” “Nina imani kesi kama hizi umekutana nazo sana, chonde msaidie baba wa watu.”
“Nitajitahidi lakini hii ni kesi nzito hasa kutokana na kushtakiana wenyewe kwa wenyewe kutokana na maelezo yake hii itakuwa mchezo umechezwa hivyo tusipokuwa makini tutaumbuka.”
“Huoni hapo kama unaweza kupata sababu ya kuona ni njama kwa vile kuna rekodi ya kukosana nyuma?”
“Teddy hapo utachekesha, wamekosana kwenye rushwa ya madawa ya kulevya, hilo ni kosa lingine ambalo halitakiwi kusemwa mbele ya mahakama.”
“Sasa tutafanyaje, kuhakikisha tunamwokoa.”
“Labda tuzungumze na mashahidi ambao nasikia ni mkewe na huyo mbaya wake aliyeapa lazima ampoteze.”
“Basi hiyo kazi niachie mimi nitakupa jibu leo usiku au kesho asubuhi.”
Teddy baada ya kuagana na wakili wa kujitegemea Mr Mnyigu alipanga jioni ya siku ile akasikilize mkewe amejipanga vipi kumuokoa mumewe.
*****
Majira ya saa mbili usiku alikuwa nje ya nyumba ya Deus kutokana na maelezo aliyoelezwa hakumpotea nyumba. Ndani ya nyumba kulikuwa na muziki wa rusha roho wa sauti ya juu, ulionesha kama ndani kuna sherehe. Aligonga mlango kwa muda mlango ulifunguliwa na kutoka Kilole ambaye hakuonesha uso wa majonzi.
“Karibu,” Kilole alimkaribisha.
“Asante,” Teddy alijibu huku akiingia ndani. Baada ya kutulia kwa muda akisoma mandhali ya ndani Kilole alimuuliza:
“Ndiyo dada yangu, nikusaidie nini?”
“Nina imani wewe ni mke wa Deus?”
“Mmh! Kwani vipi?”
“Dada nijibu wewe ndiye mkewe au vipi?” “Ndiyo mimi.”
“Mpaka sasa kuna juhudi gani za kumuokoa mumeo?” “Kwa kweli hakuna kwa vile amekutwa na ushahidi kabisa, tunasuburi mahakama itaamua nini.”
“Hata kama amekutwa na ushahidi bado unaweza kumsaidia.”
“Haiwezekani lazima atafungwa mtu kashikwa na ushahidi utamsaidia vipi?”
“Naomba ushirikiano wako, nina sikia wewe ulikuwepo mumewe akikamatwa na hayo madawa?”
“Unaomba ushirikiano gani?”
“Kuhakikisha tunamtoa.”
“Ni vigumu kumsaidia hasa kesi yenyewe ipo mikononi mwa serikali, kama una fedha heri unipe ili nimlee mtoto wake.” “Sikiliza, naomba ukane mahakamani kuwa mumeo hauzi madawa ya kulevya nami nitakuwa nyuma yako.”
“Siwezi kusema uongo, nitafungwa.”
“Huwezi mdogo wangu, wee siku ukipanda kizimbani kutoa ushahidi mteteee mumeo kwa nguvu zote ukisema alikuwa anauza na wewe utakuwemo.”
”Na ule ushahidi?”
“Nitashughulika nao mimi.”
“Kwanza wewe ni nani?”
“Utanijua baada ya kesi.”
“Lakini dada kwa vile nami nilikuwa shahidi namba moja kuona dawa za kulevya kwenye brifcase ya mume wangu siwezi kugeuka lazima nitafungwa.” “Huwezi kufungwa.”
“Nitafungwa, itanibidi niseme ukweli.”
“Hebu kuwa muelewa huwezi kufungwa kwa kutoa ushahidi wa kweli.” “Ukweli si ndio huo wa kuyaona madawa kwenye brifcase ya mume wangu.”
“Mume wako anauza dawa za kulevya?”
“Mmh! Sijui.”
“Hujui nini na wewe ni mke wake?”
“Labda alifanya kwa siri.” “Sasa sikiliza ninachokizungumza sasa hivi si ombo bali amri, ukifika mahakamani kana huyajui madawa yaliyokutwa ndani ya brifcase ya mumeo. Wewe hujui kuwa mumeo na mzee Shamo wana ugomvi?”
“Najua.”
“Sasa kwa nini unakubali mambo kirahisirahisi tu, huoni hizo ni njama za kumpoteza mumeo?” “Sasa mimi akifungwa ananihusu nini?”
“Ni kweli mumeo?”
“Kweli mume wangu, lakini kilanga haliliwi wala hawekewi matanga kila mtu atazikwa kaburi lake.”
“Una ugomvi na mumeo kabla ya tukio hili?” “Hakuna,” wakati huo alikuwa akiingia Kinape ambaye alimsahau Teddy kutokana na mavazi aliyokuwa amevaa.
“Kuna mgeni?” Kinape aliuliza baada ya kuingia.
“Ndiyo, sijui wakili wa Deus,” Kilole alijibu. “Karibu dada yangu.”
“Asante, nina imani wewe ni ndugu yake Deus?”
“Ndiyo.”
“Unanikumbuka?”
“Hataa.” “Naitwa Teddy, najua hujawahi kuniona lakini uliwahi kuisikia sauti hii, uliwahi kutumwa na Deus milioni 75,” Teddy alisema huku akitoa nikabu kichwani na kuweza kuonekana vizuri, Kinape alimkumbuka.
“Ooh! Nimekumbuka, karibu sana.”
“Ndiyo za siku?”
“Nzuri, kama ulivyosikia kaka yupo kwenye matatizo.”
“Najua ndiyo maana nipo hapa.”
“Lakini hali ni mbaya kila sehemu niliyohangaika imeonekana lazima atafungwa.” “Sasa sikilizeni, humu ndani wangapi wameshuhudia yale madawa?”
“Shemeji,” alijibu Kinape.
“Nimemueleza msaada mkubwa katika ile kesi ni kukana hayajui yale madawa ile itasaidia kupunguza ukali wa ile kesi.”
“Lakini kumbuka kuna mkuu wake ndiye shahidi namba moja,” Kinape alisema.
“Hiyo haisumbui, kama ukikana mahakamani kazi nyingine nitajua jinsi ya kuifanya,” Teddy alisema kwa kujiamini.
“Mimi siwezi, nitasema kweli,” Kilole alishikilia msimamo wake baada ya kumuona Kinape.
“Narudia hili si ombi, kaka unajua kazi yangu, kama mkienda kinyume nitawaua wote kwa mkono wangu,” Teddy alitoa onyo kali.
“Uniue mimi?” Kilole alishtuka.
“Ndiyo.”
“Kwa kosa gani?”
“La kumfunga mumeo.” “Sasa mimi nitafanya nini wakati kashikwa na ushahidi?”
“Nakuhakikishieni ushahidi utakuwa wa mtu mmoja, mzee Shamo hata panda kizimbani.” “Kwa sababu gani?”
“Sitaki maswali ila kesho ukipanda kizimbani toa ushahidi huo.”
“Lakin...”
“Sitaki maswali, naondoka ila mkienda kinyume mtageuka adui zangu namba moja, kwa herini.”
Teddy alisema huku akinyanyuka na kuondoka na kuwaacha Kilole na Kinape wakitazamana. Baada ya kuondoka Teddy, Kilole alimuuliza Kinape.
“Yule ni nani?”
“Ni yule msichana muuza dawa za kulevya aliyekamatwa na kutoa milioni 75 na ndiye aliyetaka kututajilisha lakini nashangaa papara yako umetukosesha kila kitu.”
“Hayo si muda wake sasa.”
“Sawa.”
“Sasa huyu mwanamke kesi hii inamuhusu nini?”
“Sijui.”
“Au mwanamke wake?”
“Hapana.” “Nakuhakikishia lazima nimfunge Deus kesi hii hatoki nitasema ukweli na aje aniue.”
“Kilole yaani nakuomba umsikilize yule dada, usimuone vile ni mafia mbaya anaweza kukuua hata palepale mahakamani baada ya kutoa ushahidi wa kumfunga Deus.”
“Sasa tutafanya nini?”
“Kwa nini tusimsaidie Deus?” “Deus tayari amenaswa na ndoano hawezi kuruka.”
“Sasa sikiliza, hata wewe ukikana bado atafungwa, huenda Deus ana wasiwasi na wewe, ukipanda kizimbani kutoa ushahidi ukane ule ushahidi kuwa huujui lakini akija mzee Shamo atamaliza kazi.” “Mmh! Yule mzee atanielewa kweli ikiwa mimi ndiye niliyetengeneza mpango mzima.”
“Fanya hivyo kwa uhai wako yule dada hatanii huenda na mzee Shamo sipande kizimbani.” “Kwa sababu gani.”
“Huenda atapewa fedha au auawe.”
“Mmh! Inatisha itanibidi nifanya hivyo.”
Teddy baada ya kutoka kwa Deus alibadili uamuzi wa kwenda kuonana na mzee Shamo kwa kuhofia kutego baada ya kutendo cha siku chache zilizopita japo hakukuwa na kitu chochote cha kuonesha wanatafutwa.
Alipanga kusikiliza utetezi wa mke wa Deus aliyekuwa akipanda kizimbani kesho na kuhakikisha mzee Shamo hapandi kizimbani kutoa ushahidi siku ya mwisho.
Itaendelea
Post a Comment