ad

ad

NYUMA YA MACHOZI - 26


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
“Kiloleee! Mbona unakuwa na roho mbaya kama mnyama, yaani unamfunga mumeo kwa ajili ya penzi haramu?” Kinape alishtuka. “Kinape kulitafuta penzi lako nimepata dhambi kubwa, hili la Deus mbona dogo.” “Kubwa lipi?”
“Unajua ila ufahamu, kwa Mungu nina kesi ya kujibu juu ya roho za watu watatu niliowaua kwa ajili yako. Ukifanya mchezo wowote Kinape tutawafuata kina Happy.”
“Weweee! Unataka kuniambia wewe ndiye uliyemuua Happy?” “Ndiyo.”
SASA ENDELEA...
“Kwa nini?”
“Kwa ajili yako, ni wewe uliyesababisha nimuue nilikueleza muachane lakini ndiyo kwanza ulitaka kwenda kumtambulisha kwenu. Niliamini akifika kule sina nafasi ya kuwa na wewe tena.”
“Kiloleee! Kwanini umemuua Happy mtu asiye na hatia kama kosa nimefanya mimi, si ungeniua mimi Happy amekukosea nini?” Kinape alijikuta akitoneshwa donda lililokuwa bado bichi.
“Siwezi kuukata mti wangu wa kivuli, Kinape kumbuka ni wewe ndiye uliyenitoa usichana wangu na ndoto yetu kuwa mke na mume nina imani sasa ndiyo nafasi yetu ya kuwa mke na mume.”
“Lakini si kwa ukatiri na unyama kama huu, kwa nini Kilole umebadilika na kuwa na roho mbaya kiasi hiki!” “Kinape mimi na roho nzuri sana tena yenye huruma lakini nilitetea maumivu ya moyo wangu.
"Ni wewe ndiye uliyesababisha yote kwa kunipiga picha za aibu mimi nilifanya vile kwa ajili ya kuificha aibu ile kumbuka Deus angejua wewe ungekuwa katika hali mbaya tofauti na mimi. Kila ninachokifanya ni kwa ajili yako bado unaniona mpuuzi. ”
“Kwa hiyo unaniambiaje?”
“Wiki hii Deus anapandishwa kizimbani na kuhukumiwa kifungo kikubwa, baada ya kifungo chake kila kilicho chake tunataifisha kama tulivyokubaliana tunauza kila kitu tunahama mji.”
“Mmh! Sawa,” Kinape alikubali kwa shingo upande huku moyoni akiwa na maumivu makali ya kifo cha mpenzi wake Happy.
****
Kikao cha wauza dawa za kulevya kiliendelea chini ya Teddy aliyeoneka mwenye hasira kuliko wote waliokuwepo pale.
“Ehe! Vipi huko ulipokwenda?” Moppy aliyekuwa na uchungu wa mali yake iliyokamatwa jana yake.
“Sikilizeni watu wangu kuna tatizo limejitokeza ambalo ni dhalula ambayo ilikuwa ni vigumu kuiepuka.”
“Kuiepuka vipi Teddy? Usitufanye watoto wadogo,” Moppy alikuja juu kutaka maelezo kamili.
Teddy aliwaeleza kazi aliyoifanya kutwa nzima ya kumsaka Deus na majibu aliyoyapata juu ya Deus kukamatwa jana asubuhi muda mfupi baada ya kuwasiliana.
“Kwa hiyo unataka kutuambia nini?” “Nia yangu ilikuwa kumuua Deus, lakini nimeamini hana kosa hivyo basi mzeee..sijui nani,” alitoa simu yake kuangalia jina kwenye simu na kulikumbuka.
“Mzee Shamo, usiku wa leo anatakiwa kutekwa na kuja kutueleza mzigo wetu tutaupata vipi?” “Tusipoupata tutafanya nini?” Side aliuliza huku akifungua chupa ya Jacky Daniel.
“Hilo si swali, si mnakumbuka Mose shemeji yangu nilimfanya nini, pamoja na kumkosa bado namlia taimingi lazima nilibakishe jina. Na huyu mzee lazima afe kama hana maelezo ya kuridhisha.”
“Teddy una bahati sana, leo nilikuwa nakuulia hapohapo ulipokaa, niliamini kabisa umeniingiza choo cha kike. Niliamini kama wewe ulitaka kumuua shemeji yako niliona nawe ulistahili hukumu hiyo,” Tonny alisema huku akitoa bastora iliyokuwa kwenye jacket iliyokuwa tayari kukatisha maisha ya Teddy.
“Kama ningekuwa nimefanya kwa makusudi ruksa kufanya mtakalo, hata mimi sipo tayari kumsamehe adui yangu,” Teddy alitia nguvu maneno ya Tonny.
Walikubaliana usiku wa siku ile kumtafuta mzee Shamo ili wajue wataupataje Mzigo wao. Baada ya kikao Teddy alimpigia simu mzee Shamo baada ya simu kuita ilipokelewa upande wa pili.
“Haloo.”
“Haloo mzee Shamo, shikamoo,” Teddy alijifanya anamfahamu.
“Marahaba, nani mwenzangu?” mzee Shamo aliuliza. “Najua hunijui ila tukikutana utanifahamu vizuri.”
“Una shida gani?”
“Mzee Shamo haraka ya nini? Tukikutana unajua kila kitu, upo wapi sasa hivi?”
“Sasa hivi nipo Sea Cliff Hotel.”
“Okay, baada ya dakika ishirini nitakuwa hapo.”
“Hakuna tatizo.”
Baada ya kukata simu aliwageukia wenzake waliokuwa wakimfuatilia apokuwa akizungumza.
“Nakuja sasa hivi.”
“Una kwenda wapi?”
“Namfuata yule mzee.”
“Teddy utamuweza peke yako?”
“Akinishinda namtwanga risasi na kutokomea zangu.”
“Noo, usifanye hivyo usitumie hasira kila wakati, nenda na Tonny nina imani mtaweza kumfikisha hapa bila kumwaga damu,” Double D alimtuliza Teddy aliyeoneka amepandwa na mzuka baada ya kuona kifo chake kilikuwa usoni kwake kwa kuoneshwa bastora na Tonny iliyotakiwa kuchukua uhai wake.
Teddy aliongozana na Tonny kumfuata mzee Shamo, moyoni aliapa lazima atampoteza Tonny baada ya kutaka kumuua yeye alipanga kummaliza siku yoyote bila mtu kujua. Waliondoka katika gari moja kila mmoja akiwa na mawazo yake Tonny akiamini kabisa aliyoyasema yameishia palepale, lakini kumbe mwenzake alikuwa na kisasi kikali moyoni mwake. Walipofika nje ya Hoteli ya Sea Cliff, Teddy alimpigia simu mzee Shamo.
“Mzee wangu nimefika.”
“Nipo jirani na mlango wa kuelekea baharini.”
“Sawa nakuja.”
Baada ya kukata simu alimgeukia Tonny aliyekuwa bado yumo ndani ya gari akisubiri maelekezo. “
Tonny mzee anasema yupo karibu na mlango wa kuelekea baharini, sasa fanya hivi.. nenda mpaka eneo lile kisha nibip mimi nitampigia angalia nani anayepokea ili tufanye kazi kwa uhakika.”
“Hakuna tatizo.”
Tonny aliteremka kwenye gari na kuelekea ndani ya hoteli na kumwacha Teddy akigeuza gari na kuliweka vizuri kusubiri kutaarifiwa. Haikuchukua muda simu yake iliita, alipoangalia ilijua tayari Tonny amefika eneo husika. Alipiga simu moja kwa moja kwa mzee Shamo, baada ya kuita kwa muda ilipokelewa.
“Haloo upo wapi mbona sikuoni?” mzee Shamo aliuliza.
“Umesimama wapi?”
“Nipo hapa mbona unaonekana wewe upo wapi?”
“Nipo kwenye mlango wa kuelekea baharini.”
“Mbona mimi nimesimama hapa tena nipo wazi.”
“Okay nimekuona.”
Teddy alikata simu na kumpigia Tonny.
“Tonny umemuona?” “Nimemuona.”
“Msemeshe na muombe utoke naye huku nje.”
“Poa.” Baada ya kukata simu Tonny alimsogelea mzee Shamo na kumsemesha.
“Shikamoo mzee.”
“Marahaba kijana.”
“Nina imani wewe ndiye mwenyeji wetu.”
“Una maana gani?”
“Sasa hivi sister alikuwa akiwasiliana wewe.”
“Eeh! Yupo wapi?” Yupo nje kanituma nikufuate ana mazungumzo na wewe ya dakika tano kisha utaendelea na starehe zako.”
“Hakuna tatizo.”
Mzee Shamo aliongozana na Tonny nje kuelekea upande wa gari lilipokuwa, Teddy alipowaona wanasogea alilisogeza gari, wakati huo Tonny alikuwa ameisha toa bastora na kumuwekea ubavuni mzee Shamo. “Samahani mzee naomba uwe mpole ingia kwenye gari hilo hapo mbele la sivyo nakumwaga utumbo.”
“Jamani kuna tatizo gani?” mzee Shamo alishtuka. “Hakuna tatizo ila tuna mazungumzo ya kirafiki.”
Kwa vile gari lilikuwa limekwisha simama na kufunguliwa mlango mzee Shamo aliingia ndani kisha alifuatia Tonny baada ya kufungwa mlango Teddy aliondoa gari kwa kasi. Baada ya kwendo mfupi walimfunga kitambaa cheusi na gari kupelekwa moja kwa moja ndani ya ngome ya wauza dawa za kulevya. Walipofikisha ndani alifunguliwa kitambaa na kujiona yupo mbele ya watu zaidi ya nane.
“Karibu mzee Shamo,” Double D alimkaribisha kistaabu.
“Asante,” alijibu huku akijenga ujasiri. “Unatumia kinywaji gani?”
“Asante, kwa sasa sihitaji zaidi ya kujua sababu ya kuletwa hapa kama gaidi.”
“Utajua tu mzee wetu, shida yetu kupata mzigo uliokamatwa juzi.”
“Mzigo! Mzigo gani?”
“Juzi kuna vijana wawili walikamatwa uwanja wa ndege na dawa za kulevya, na sababu kubwa ni wewe..”
“Mimi?” Shamo alimkata kauli kupiga tuhuma zile.
“Ndiyo, kumbuka tukio ulilofanya asubuhi ya siku hiyo ndiyo lililoharibu kila kitu, tunajua wewe ni mtu mkubwa tunaomba ule mzigo uurudishe mara moja.”
“Usipoteze muda wenu sijui lolote kuhusiana na hicho mnachosema.”
“Mzee hatutaki tutumie nguvu, tutakuachia usiku huu kabla hakujapambazuka tunataka mzigo uliokamatwa.”
“Sasa mimi nitaupata wapi?” “Utajua mwenyewe la sivyo jina lako litabakia historia.”
“Hata mnipe mwaka mzima siwezi kuwapa kitu kilichokamatwa siku zote uharibiwa pia mimi si mtunza stoo.”
“Kwa hiyo?”
“Sina msaada wowote.”
“Teddy nina imani mzee hana jibu, mrudisheni akaendelee na starehe zake.”
“Hakuna tatizo, kwa hiyo tunamuacha hivihivi tu?” Teddy alihoji.
“Mwacheni tu.”
“Siri yetu si itatoka nje?”
“Haiwezi, kwanza hapa hajui yupo wapi.” Mzee Shamo alifungwa kitambaa usoni na kupelekwa nje kwenye gari, Double D aliwafahamisha washirika wake kwa nini amemuacha huru mzee Shamo.
“Mnajua kwa sababu gani nimeamua kumwacha hai, tukimuua leo lazima tutamuongezea matatizo yule jamaa yetu aliye mahabusu kwa kuamini kifo chake kinatokana na kukamatwa kwake.”
“Aisee, sikuwaza vile ingekuwa mimi ningemuua palepale kwenye kochi,” Teddy alisema. “Yule kifo kipo palepale kutokana na maelezo yote inaoneka kabisa jamaa yetu haponi, kwa vile hana msaada wowote kwetu hatuwezi kumsaidia kwa lolote.”
“Lakini tunaweza kucheza na hakimu.”
“Teddy hata tukimtoa hakuna faida yoyote tutayopata, tusubiri tu akifungwa tumlipie kisasi kwa kuua mbaya wake siamini tuna msaada mwingine zaidi ya huo.”
“Mmh! Sawa.”
Teddy alikubali shingo upande kwa kuamini alitakiwa aonesha naye ubinaadamu kama alivyofanyiwa na Deus alipokamatwa na mzigo. Kwa upande wake asingeweza kumsaidia kutokana na hofu ya kutafutwa baada ya kushindwa kuua shemeji yake.
Baada ya mazungumzo walimtoa mzee Shamo wakiwa njiani kumrudisha walimvutisha dawa ya kulevya zilizomlevya na kulala, kwa vile ilikuwa usiku walimrudisha jirani na hoteli Sea Cliff kumuacha sehemu iliyo salama na kurudi kujipanga upya.
Itaendelea

No comments

Powered by Blogger.