NYUMA YA MACHOZI - 28

MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
Teddy baada ya kutoka kwa Deus alibadili uamuzi wa kwenda kuonana na mzee Shamo kwa kuhofia kutego baada ya kutendo cha siku chache zilizopita japo hakukuwa na kitu chochote cha kuonesha wanatafutwa. Alipanga kusikiliza utetezi wa mke wa Deus aliyekuwa akipanda kizimbani kesho na kuhakikisha mzee Shamo hapandi kizimbani kutoa ushahidi siku ya mwisho.
SASA ENDELEA...
****
Siku ya pili Kilole alipopanda kizimbani alikana kuyaona yale madawa ya kusema ameyaona baada ya kuitwa chumbani kwake, lakini mume wake hajawahi kuuza madawa yale. Alipoulizwa inawezekana ni njama za watu za kumchafua mume wake, alijibu inawezekana japo hana uhakika.
Majibu ya mke wa Deus yalimshangaza sana mzee Shamo kutokana na yeye kupeleka mchongo ule na kuahidi msaada lakini mwisho wa siku aligeuka kama kinyonga. Kesi iliahilishwa mpaka siku ya pili utakapotolewa ushahidi wa mwisho na mkuu wa kitengo cha kuzuia madawa ya kulevya mzee Shamo. Teddy aliyekuwepo mahakamani alifurahi kuona mambo yamekwenda kama alivyopanga, kazi ilibakia kwake kumaliza kazi. Mzee Shamo alimfuata mke wa Deus na kumuuliza: “Sasa umefanya nini?” “Tutazungumza,” Kilole alijibu kwa sauti ya chini. “Tutazungumza nini, nani aliyeleta taarifa hizi?” “Mimi.” “Sasa kwa nini umenigeuka?” “Lakini wewe si kesho utammaliza.” “Nimmalize kivipi ikiwa umeishapunguza nguvu, wewe ndiye aliyekuwa na kisu kikali cha kumaliza kesi, huoni kama nitabanwa kuwa nimetengeneza kesi?” “Tutazungumza, naomba niondoke eneo hili si salama kwangu.” “Mmh! Nimejua, lakini naapa haponi nitakufa na mumeo.” Kilole aliachana na mzee Shamo aliyemshangaa Kilole kwa kauli yake ya kukana wakati aliapa kutoa ushirikiano wa kutosha na mara ya mwisho usiku kabla ya kukutana na Teddy alimuhakikishia atammaliza Deus. Lakini aliapa lazima ampoteze mbaya wake. Teddy naye alijipanga kuhakikisha mzee Shamo alioni jua la kesho ili kesi ikose nguvu na kumpa nafuu Deus. Baada ya mahakama Kilole na Kinape wakiwa wanajiandaa kuondoka alifika Teddy kwenye gari lao.
“Asante mdogo wangu umenifurahisha sana,” Teddy alimpongeza Kilole aliyekuwa akifunga mkanda wa gari.
“Lakini kazi bure kesho si anapanda mwenyewe hatujafanya lolote,” Kilole alimjibu kwa sauti ya chini.
“Kazi niliyokutuma umeifanya iliyobaki ni yangu, hata akifungwa mumeo hawezi kufungwa miaka mingi.”
“Mmh! Siamini.”
“Nilimuona anakufuata alikuwa anasemaje?”
“Alikuwa akinilaumu kumgeuka.”
“Akamjibu nini?“
“ Sikuwa na jibu.”
“Najua bado atataka kujua kwa nini umemgeuka.”
“Akiniuliza hivyo nimwambieje?”
“Mwambie vyovyote vile, lakini kazi itaisha usiku huu.”
“Umeishazungumza na hakimu?”
“Utajua kesho wakati wa kutolewa ushahidi wa mwisho.”
“Haya wacha niende nikapumzike.”
Kilole aliondoka huku moyo ukimuuma kushindwa kutoa ushahidi wa kumfunga mumewe. Lakini aliamini mzee Shamo anaweza kumfunga mumewe kwa vile ndiye shahidi namba moja.
Mzee Shamo naye alikaa pembeni ya mahakama na vijana wake wakijadiliana juu ya kugeukwa na mke wa Deus mtu aliyefanikisha kukamatwa mume wake.
“Sasa mzee tutafanyaje?”
“Kwa kweli yule mwanamke kanichanganya sana.”
“Sasa tutafanyaje, kesho na wewe ndiye utakayemaliza kutoa ushahidi?”
“Dawa iliyopo ni kumshika na kumtesa aseme ukweli ili kesho niweze kupata nguvu katika ushahidi wangu bila hivyo naweza kuonekana kweli nimeutengeneza. Unafikiri wakili wa Deus akisema kuwa nimetengeneza ushahidi ili nimfunge na mkewe amekataa itakuwaje?”
“Kwa hiyo kazi tuifanye mara moja kabla hajatoka eneo la mahakamani?”
“Hapana anatakiwa akachukuliwe usiku na kupata mateso mazito na kesho atakuja mahakamani akitokea mahabusu.”
“Huoni kama anaweza kusema tumemlazimisha?”
“Kwa hiyo mnanishauri tufanye nini?”
“Mzee inatakiwa tusitumie nguvu tunatakiwa kwanza tujue nini kilichomfanya akugeuke kisha tujue tufanye nini,” kijana mmoja wake mmoja alimpa ushauri.
“Halafu kuna kitu alinieleza kuwa usalama wake ni mdogo pale mahakamani.”
“Inawezekana kuna watu wanashindana na sisi ambao ni miongoni mwetu.”
“Lakini ni yeye aliyeleta taarifa za mumewe kuuza unga sasa anageuka nini kwani tulimfuata?”
“Kwa hiyo mzee wangu tunatakiwa kufanya jambo kisomi kuliko kutumia nguvu. Inawezekana kuna kitu kimeingia katikati si umesema jana usiku uliwasiliana naye na kusema kila kitu kipo sawa.”
“Hata mimi nashangaa.”
“Ukiona hivyo ujue kuna kitu.”
“Basi usiku tutakwenda kujua sababu kipi kilichomfanya ageuke kama kinyonga.”
****
Majira ya saa kumi na mbili Teddy alikuwa amesimamisha gari lake karibu kabisa na ofisi za kupambana na madawa ya kulevya. Aliwahi makusudi ili aweze kumuona mzee Shamo na kumfuatilia. Baada ya kukaa kwa muda majira ya saa moja kasoro aliliona gari la mzee Shamo likitoka ofisini. Aliliacha lipite kisha alilifuatilia nyuma bila mwenyewe kujua.
Mzee Shamo kama kawaida yake alielekea Sea Cliff hoteli, alimfuatilia mpaka alipoingia hotelini. Hakusumbuka sana kumfuata alipaki gari lake pembeni ya gari la mzee Shamo na kumfuata ndani ya baa.
Teddy aliagiza wine na kunywa taratibu huku akifuatilia nyendo za mzee Shamo, majira ya saa mbili walitokea vijana wawili na kuondoka naye. Japo alijua ana kazi nzito lakini hakufanya papara. Aliwahi kwenye gari lake walipoondoka aliwafuata taratibu bila wao kujua wanafuatwa na mtu. Waliondoka eneo lililokuwa na taa na kuingia sehemu ya giza aliamini ile ndiyo nafasi aliyokuwa akiitaka.
Aliongeza kasi kidogo na kuwapita kisha alilisimamisha gari kwa mbele ghafla iliyosababisha gari la mzee Shamo kulikwangua kwa nyuma. Kilole hakuteremka haraka kwenye gari alitulia bila kufungua vioo. Vijana wa mzee Shamo waliteremka kwa hasira ili wamuadabishe mwenye gari ya mbele.
Teddy wakati huo alikuwa amekwisha jiandaa kwa mapigano, bastora yake ilikuwa tayari kufanya kazi.
Walifika na kuanza kutukana huku wakigonga kioo kwa ngumi ili afunge. Wakati huo mzee Shamo naye aliteremka na kusogea. Kwa vile ndani ya gari kulikuwa kiza Teddy aliteremsha kioo kidogo na kuachia risasi zilizowapata wote.
Hakuondoka haraka aliteremka na kuwaongeza risasi ili kupata uhakika kama kweli wamekufa. Baada ya kumaliza zoezi lake alikimbilia kwenye gari ili aondoke kabla ya kuondoka alisikia king’ora cha polisi kilichomshtua.
Alipowasha gari aondoke liligoma kuwaka, aliteremka na kukimbilia sehemu za baharini. Akimbilia na kwenda kujificha nyuma ya mti mkubwa uliokuwa karibu na bahari. Baada ya kujicha alichungulia na kuona gari la doria likisimama eneo la tukio, aliwaona wakiteremka na kuwanza kufanya uchunguzi.
“Aisee kuna watu watatu wamelala chini, tuweni makini,” askari mmoja alitoa taadhali baada ya kuona watu wamelala chini.
“Tena hii gari kama ya Afande Shamo?” askari mwingine alisema huku akimulika na tochi.
“Si huyu!” Teddy alimsikia mmoja akisema kwa mshtuko.
“Nani?”
“Afande Shamo.”
“My God ameuawa?”
“Pigeni simu haraka kuongeza ulinzi hali ni mbaya.”
“Afande wakati tunakaribia hapa niliona kama mtu anakimbilia baharini.”
“Hatuwezi kupambana naye hatujui uwezo wake huenda wapo wengi.”
Teddy alitumia nafasi ile kutembea pembezoni mwa bahari mpaka maeneo ya Daraja la Salenda, alichepua mwendo kufuata barabara ya Ali Hasani Mwinyi kuelekea Mwenge. Mbele kidogo gari dogo lilisimama na kushangaa kuitwa jina lake.
“Teddy.”
“Nani?”
“Ingia haraka.”
Bila kuuliza aliingia ndani ya gari, haikupita muda gari la polisi lilitokea, lakini halikushughulika nao lilipita huku likipiga king’ora cha hatari. Teddy alishtuka kumuona mbaya wake Tony ndiye aliyekuja kumuokoa.
“Vipi Tony unatoka wapi?”
“Huwezi kujua, nimetumwa na bosi nikusaidie ameona kila kitu.”
“Alikuwa wapi?”
“Hiyo haikuhusu ila safari hii moja kwa moja Air Port unatakiwa uondoke na ndege ya saa sita usiku.”
“Booking?”
“Kila kitu kipo tayari mengine utayajua ukifika chimbo.”
Tonny aliendesha gari kwa kasi hadi uwanja wa ndege na kumpatia Teddy tiketi ya kusafiri. Muda ilionesha ni saa tano kasoro sita. Tonny hakuondoka mpaka ndege ilipoondoka kuhofia Teddy kuendelea kuwepo Dar na kuleta tafrani baada ya kukosa uvumilivu wa kutenda mambo.
Walihofia huenda akafanya mauaji zaidi kwa vile alikuwa akitumia nguvu bila akili. Teddy aliwasili uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyata saa kumi alfajiri na kwenda moja kwa moja chimbo.
***
Siku ya pili Teddy akiwa sehemu yake ya maficho alishtuka kumuona shemeji yake aliyetaka kumuua akiwa mzima wa afya na akikanusha vikali kwamba Teddy ndiye aliyetaka kumuua katika televisheni ya Italy News. Maelezo yake yalimsafisha Teddy aliyekuwa amewekewa WANTED na polisi wa Italia.
Maelezo ya shemeji yake yalimchanganya sana Teddy na kujiuliza kwa nini ameamua kumsafisha vile ikiwa amemfanyia kitu kibaya cha kutaka kumuuua lakini alimsafisha mbele ya vyombo vya usalama vya Italia hata kutoka picha za kumuomba radhi Teddy kutokana na kushukiwa na njama za kumuua Moses.
Hakiwa bado haamini alipokea simu toka kwa washirika wenzake toka Italia.
“Haloo Teddy.”
“Ndiyo Jimmy.”
“Umepata taarifa za Mose?”
“Hapana,” alijifanya hajui kitu.
“Mose amekusafisha katika vyombo vya usalama, lakini...”
”Lakini nini tena Jimmy?”
“Jamaa amesema yale kwa vile ana uchungu na wewe na amesema atakusaka popote ili alipe kisasi.”
“Achana naye hawezi kitu,” Teddy alisema kwa kujiamini.
“Teddy humjui Mose! Sisi ndiyo tunamjua, amesema ndani ya mwezi mmoja atakuwa ametia mikononi. Anajua kuna watu wanakukingia kifua eti wanaume zako ataanza kudili na hao na mwisho atakumalizia na hivi ninavyosema anajiandaa kuanza kukusaka.”
“Kwani yeye anajua nipo wapi?”
“Siwezijua lakini kaa ukijua jamaa kaingia msitari wa mbele kukusaka.”
“Poa tutaona mimi na yeye nani atammaliza mwenzake.”
“Nataka pia kukueleza Moses ana jamaa zake wanapenda kuua kama hawana akili nzuri, hivyo wakati wowote wataanza kukusaka.”
“We mwache aje wala hanitishi kwa jeuri yangu nitamfuata hukohuko.”
“Wewe!”
“Jimmy hunijui hivi ninavyozungumza nimemlaza mtu mzito serikalini na vijana wake usiku wa kuamkia leo jiji Dar.”
“Na sasa upo wapi?”
“Jimmy kama umetumwa siwezi kukueleza ila mweleze wala asisumbuke kunitafuta namfuata huko huko,” Teddy alionesha jinsi gani anavyojiamini.
“Jamaa amesema anajua sijui upo Kenya sijui sehemu gani, ameniahidi ndani ya mwezi maiti yako itaokotwa barabarani kwanza atakubaka kabla ya kukuua kinyama.”
“Umesema amesema nipo Kenya?” Teddy alishtuka.
“Ndiyo.”
“Mmh! Mwache aje.”
“Kuwa makini sitajisikia vizuri nikisikia umeuawa na Mose.”
“Sawa Jimmy, nakuahidi nitammaliza yeye kabla hajanigusa.”
Baada ya kumaliza kuzungumza na Jimmy simu toka Dar toka kwa bosi wake Double D iliingia.
Itaendelea
Post a Comment