NYUMA YA MACHOZI - 25

MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
“Nilikueleza mapema kuwa huwezi kuwa msafi bila kujisafisha.” “Hiyo nini?”
Deus alitaka kunyanyuka kwa hasira lakini alitulizwa na siraha zilizokuwa zimemtazama.
“Deus umekwisha, nilikueleza toka zamani kuwa wewe mtoto mdogo huwezi kushindani na mimi, kwa hili utafia gerezani.”
“Muongo mkubwa huwezi kuja kuniwekea madawa ili kunitia hatiani, lakini nikitoka nitakuua nakuapia,” Deus alipagawa kuona ndani briefcase yake kuna madawa ya kulevya.
SASA ENDELEA...
“Jamani tuondoke naye kazi yetu tumemaliza, tunawaachia serikali watafanya nini sisi tena haituhusu.” Deus alitiwa pingu na kutolewa nje kama mhalifu huku Kilole akilia mpaka akagaagaa chini kwa ajili ya kumlilia mumewe, kitu kilichomshtua mzee Shamo na kujiuliza ndiye yule aliyeleta habari za mumewe au mwingine. Deus kabla ya kuondoka alimwambia mkewe. “Nenda kwa Mambo Twalipo mwambie habari hizi, sawa.”
“Sawa mume wangu lakini hizo dawa lazima wamekuwekea sisi hatuuzi dawa.” “Itajulikana wewe nenda asubuhi hii.”
“Sawa, Kinape yupo wapi?” “Ooh! Kweli alikwenda ofisini kwake, atarudi muda si mrefu, akirudi mweleze na yeye ashughulikie suala hili.”
Deus alipelekwa polisi na kufunguliwa mashtaka ya kujihusisha na kuuza dawa za kulevya.
Kilole pamoja na kupanga mpango ule alijikuta akijutia uamuzi ule wa kumfunga mumewe kwa ajili ya Kinape. Baada ya kuondoka mumewe alijikuta akilia mpaka macho yalivimba lakini bado aliamini alichokifanya kilikuwa sahihi upande wake.
****
Upande wa pili Teddy msichana hatari wa kuuza dawa za kulevya akiwa mafichoni Nairobi Kenya aliwasiliana na washirika wake waliokuwa tayari na mzigo wa kuingiza nchini Tanzania. Baada ya kupewa taarifa zile alimpigia simu Deus kuwa mzigo upo tayari, kwa vile alikuwa na uhakika na kazi yake, alimweleza awaeleze waje. Teddy naye aliwaeleza washirika wenzake wawili waliokuwa wamekuja na mzigo kidogo wa majaribio waingie nao. Hata asubuhi alimpigia kumweleza jamaa wapo njiani naye Deus alimtoa wasiwasi kuwa kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa. Lakini bahati mbaya kabla jioni haijaingia Deus aliangukia kwenye mikono ya polisi na kuwekwa mahabusu kusubiri kufikishwa mahakamani. Akiwa mahabusu alisubiri mtu aje amtume kwa vijana wake kuhusu mzigo utakaoingia jioni ya siku ile.
Haikuwa hivyo baada ya kukamatwa mkuu wao vijana wake wote walio chini yake walibadilishwa eneo la kazi, uwanja wa ndege waliwekwa askari wapya. Habari zile zilimkata maini Deus na kuona kama watu wake wakikamatwa atazidi kujiongezea matatizo kutoka kwa wauza dawa za kulevya ambao hawakuwa na dogo.
****
Majira ya saa moja jioni ndege ya shirika la Qatar iliwasili jijini, katika abiria waliotua siku hiyo walikuwemo washirika wawili wa Teddy. Wakati huo Teddy alikuwa ameishapiga simu zaidi ya mara kumi kumtafuta Deus. Mwanzo simu iliita bila kupokelewa na mwisho wake haikupatikana tena.
Pamoja na kumkosa hewani Deus, Teddy aliamini kutokana na makubaliano ya asubuhi lazima angekuwepo uwanjani. Baada ya ndege kufungua mlango. Tonny na Moppy walitoka taratibu wakiamini wapo kwenye mikono salama ya Deus.
Hata mizigo yake ilipowekwa pembeni hawakuwa na wasiwasi kwa kujua ndiyo njia ya kuwatoa kiwanjani salama. Kumbe siku hiyo kulikuwa na usimamizi mpya na mtu waliyekuwa wakimtegea alikuwa akinyea debe.
Walishangaa kuwekwa chini na kupewa kashikashi kisha kuchukuliwa na kupelekwa mahabusu. Walishangaa kutomuona mtu wa kuwasaidia. Washirika wenzao waliofika kuwapokea uwanjani pale hali ile iliwashtua na kumpigia simu Teddy. “Haloo Teddy, vipi mbona hatuelewi?’
”Hamuelewi nini?”
“Jamaa ameshikwa wapo chini ya ulinzi.”
“Msiwe na wasiwasi watatoka tu,” Teddy alijibu kwa kujiamini.
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“Nendeni nyumbani watakuja wenyewe,” Teddy aliamini kabisa Deus yupo.
Kila alipopiga simu ya ya Deus haikupatikana kitu kile kilimtia wasiwasi na kuwaomba waulizie kwa vijana wake mtu anayeitwa Deus. Walifanya vile, lakini jibu lilikuwa hawamfahamu mtu hiyo.
Majibu yale yalimfanya Teddy kichwa kifanye kazi kwa kuwaomba kuwafuatilia kwa mpaka mwisho ili wajue nini kinaendelea. Kutokana na uzoefu na kazi ile walifanikiwa kuwatoa kabla hakujapambazuka, lakini mzigo wao wa fedha nyingi ulipotea. Jamaa walijikuta wakimlaumu Teddy kwa kuwaingiza choo cha kike.
Teddy kitendo cha Deus kumgeuka kilimuumiza sana na kukumbuka kauli aliyomueleza Deus juu ya kwenda kinyume na makubaliano yao. Siku ya pili Teddy alipanda ndege mpaka Dar kumtafuta Deus, alipofika alijitahidi kumtafuta Deus kila kona lakini hakumpata wala habari zake hazikupatikana.
Sehemu zote ya uwanja alimtafuta bila mafanikio, wazo lililomujia ni kumteka sekretary wake ili ajue Deus yupo wapi. Kwa hasara waliyoingia aliapa kumuua kwa mkono wake. Majira ya saa kumi na mbili muda anaotoka secretary wa Deus, ambaye hakuwa mgeni machoni mwake alimuona akiingia kwenye gari na kuondoka.
Baada ya kuondoka waliamua kulifuatilia lile gari kwa nyuma. Kutokana na wingi wa magari ilikuwa vigumu kuweza kumteka kwa urahisi. Waliliacha gari lililombeba yule msichana aliyeoneka yupo na mpenzi wake kutokana na muonekano wao ndani ya gari. Japo vioo vyote walifunga lakini walionekana ndani. Gari lilipofika maeneo ya Mbezi beach iliacha barabara kubwa na kuingia njia iliyokuwa haina rami. Teddy aliliacha gari lile litembee kidogo sehemu iliyokuwa wazi.
Baada ya kuridhika na kile anachotaka kukifanya alikanyaga mafuta na kulipitisha gari kwenye majani kwa mwendo wa kasi kidogo ili kulipita gari alilokuwa amebebwa secretary na kusimama mbele yao kwa ghafla.
Kitu kilichofanya mpenzi wa secretary kuteremka kwa hasira baada ya kumuona aliyefanya mchezo wa kijinga ni mwanamke alimfokea huku akimtishia kumpiga. “Wee malaya unatafutwa bwana.”
“Nani malaya?” Teddy aliuliza akiwa anamsogelea bila wasiwasi wowote. “Wewe hapo,” mpenzi wa secretary alisema huku akimnyooshea kidole. “Bahati yako sina shida na wewe, ungejutia maneno yako ya shombo,” Teddy alisema bila hofu kitu kilichomshangaza Secretary na mpenzi wake na kujiuliza yule msichana ni nani. “Ungeniganya nini?”
“Nakwambia sina shida na wewe nashida na huyu dada, Deus yupo wapi?” Teddy aliyeoneka akijiamini kupita maelezo alimshtua secretary kwa swali lile.
“Deus gani?”
“Bosi wako.”
“Wewe nani unayemuuliza Deus?”
“Umenisahau?” Teddy alisema huku akitoa miwani usoni.
“Siwezi kuwakumbuka wote.” “Dear kwanza mambo ya ofini asubiri kesho,” mpenzi wa secretary aliingilia kati.
“Sikiliza kaka, nakuheshimu hunijui sikujui, naweza kumchukua sijui mkeo na usinifanye lolote na zaidi ya hapo ni kukupoteza kwa sekunde chache. Mimi si mwendawazimu kuja huku,” Teddy alisema kwa sauti ya kukoroma.
“Kwani wewe shida yako nini?” secretary alikuwa mpole kutaka kumsililiza kwani alijua yule dada alikuwa na jambo la msingi. “Shida yangu Deus.”
“Nina imani unajua kazi zetu, hebu nieleze shida yako kwa Deus, naweza kukusaidia.”
“Shida yangu kuonana na Deus.”
“Wewe ni nani kwake?”
“Nina imani unanikumbuka niliisha wahi kuletwa ofisini kwa kosa la kukamatwa na dawa za kulevya na tatizo langu lilichukua muda lakini mwisho wa siku Deus alilimalizia.”
“Ooh! Nimekukumbuka, kwa sasa huwezi kumuona.”
“Kwa nini?”
“Taarifa za Deus nilipata juujuu kuwa ana matatizo makubwa sana ambayo yanaweza kumpotezea kazi na kufungwa.”
“Tatizo! tatizo gani hilo?” Teddy aliuliza huku macho yamemtoka pima.
“Japo si sheria sina budi kukueleza ukweli, Deus jana asubuhi amekamatwa kwake na dawa za kulevya.”
“Muongo mkubwa! Mmeamua kupindisha ili kumkinga kwa kitendo alichonitendea?” Teddy alikuja juu hakukubaliana na taarifa ile.
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Juzi nimewasiliana naye na asubuhi ya jana, halafu uniambie eti ana matatizo, usalama wako ni kunipeleka alipo bosi wako la sivyo nitageuka mtoa roho sasa hivi,” Teddy alibadilika na kuwa mwekundu baada ya kuona Secretary akileta ujanja.
“Dada hunijui wala sikujui, lakini Deus yupo kwenye matatizo makubwa sana na sijui kama atatoka salama, majuzi alikesha uwanja wa ndege kikazi na asubuhi aliporudi nyumbani kwake hakutulia alikamatwa kwa kukutwa na dawa za kulevya kwenye briefcase yake.”
“Kwa sasa yupo wapi?”
“Yupo ndani na kesho anapandishwa kizimbani kama unaona nakudanganya njoo kesho mahakamani.”
“Kwa nini alinieleza niingine mzigo?”
“Tatizo hilo lazima nimtetee ilikuwa ghafla, halafu pigo kubwa lilikuwa kubadili askari wote wa uwanja wa ndege. Kwa tatizo lile bado kuna mabadiliko makubwa yanakuja hata mimi sina maisha marefu kwa vile ndiye niliyekuwa mtu wake wa karibu muda wote aliokuwa kazini.
“Hata taarifa za kuingia watu wawili wenye mzigo mimi nilikuwa najua, lakini yaliyotokea walitutisha, kama wangekuwa vijana wake wapo hata mimi ningesimamia kusingeharibika kitu.”
“Una uhakika Deus hafanyi kazi ya kuuza unga?”
“Afanye ile biashara iwe vipi, wakati kila siku anaingiza fedha nyingi kwa hao wauza unga.”
“Unafikiri ni kwa nini amekamatwa na dawa za kulevya?”
“Kuna bosi mmoja haelewani naye ndiye aliyemkamata, watu wote tunajua amembambikia ili kumharibia maisha yake.”
“Huyo bosi wake anaitwa nani?”
“Mzee Shamo.”
“Ni mkubwa wake?”
“Ndiyo.”
“Kwa nini alimfanyia vile?” “Kuna fedha za rushwa ziliingia yule mzee akamzika Deus alipodai ikawa tatizo na kufikia kutishiana maisha. Lakini walimaliza tatizo lao, lakini nashangaa mzee yule alivyommaliza vibaya Deus. Yaani bosi wangu alikuwa mzungu hana tamaa za kijinga kama wazee tunaofanya nao kazi kila kitu wanataka wao.” “Mzee Shamo anakaa wapi?”
“Nasikia yupo Kinondoni lakini sijui ni sehemu gani.”
“Una namba yake ya simu?” “Ninayo.” “Naomba.”
Secretary alimpa namba ya simu, Teddy aliisevu kwenye simu yake na kusema:
“Asante, pia samahani kwa kuwasimamisha kijeshi na kuwapotezeeni muda.”
“Bila samahani kwetu kawaida,” Secretary alijibu.
“Inaonekane kwa shemeji ni ngeni, samahani shemu,” Teddy alimuomba msamaha mpenzi wa secretary. “Kawaida dada yangu.”
“Niwaache mkapumzike, lakini hasira zangu kwa Deus zitaishia kwa huyo mzee sijui Shamo lazima atalipa mzigo uliopotea na ziada sitaki mchezo kwenye kazi yangu.”
“Haya dada siku njema.”
Teddy aliagana na Secretary kwa kuliondoa gari mbele yao na kisha kuligeuza kurudi mjini. Njia nzima alikuwa na hamu ya kuonana na mzee Shamo ili ajue atalipa vipi hasara za kumweka ndani Deus na kuwasabishia usumbufu hasara kubwa. ****
Juhudi za kumtoa ndani zilikuwa tofauti kati Kilole na Kinape, Kilole alimweleza Kinape asipoteze muda kwani kesi ya Deus yenye ushahidi kuweka wakili ni kupoteza muda.
“Sikiliza Kinape fedha tunayotaka kupoteza kumwekea wakili Deus heri tuiweke kwa ajili ya kumsomeshe mwanaye.”
“Japo ameshikwa na dawa ambazo bado siamini kama ni zake, lakini wakili anaweza kupunguza adhabu na kufungwa miaka michache.”
“Kinapeee, acha ujinga dawa zimekutwa ndani kwetu tena ndani ya biefcase yake bado unaona atapona?”
“Anaweza kupona inawezekana zile zilikuwa za ushahidi na si za kuuza.”
“Kinape hata Yesu arudi mara ya pili Deus haponi tena bahati yake ingekuwa Uarabuni angenyongwa.”
“Mbona sikuelewi nakuona kama vile una furahia tukio la Deus kufungwa?”
“Lazima nifurahie kama angesafiri na mzigo ule kukutwa ndani mimi si ndiye ningenyea debe.”
“Lakini hiyo biashara kaianza lini?”
“Muda mrefu ila aliifanya kwa siri hakupenda mtu yeyote ajue hata mimi mwanzo alinificha.”
“Sasa Deus kwa nini anajiingiza kwenye biashara kama ile wakati alikuwa kwenye mradi mzuri wa kuingiza mabilioni bila fedha.” “Ndio hivyo mshika mawili.”
“Lakini bado sikubali nitapigania kuhakikisha Deus anatoka kwa gharama yoyote,” Kinape bado alikuwa na huruma na rafiki yake.
“Kinape usiwe mjinga kwa taarifa yako Deus hatoki, hii ni nafasi ya mimi na wewe kuishi pamoja.”
“Hapana Kilole haiwezekani lazima nimpiganie Deus, mambo yangu yote haya ni kwa ajili yake sitakuwa mwizi wa fadhira.” “Kinape tulizungumza nini?” Kilole alimshangaa Kinape.
”Kuhusu nini?”
“Deus.”
“Kuhusu Deus nini?”
“Si ulinikataza nisimuue tutafute njia ya kumfanya ili tu atupishe tuwe pamoja, nafasi imepatikana unaleta kiswahili kirefu mbona sikuelewi?” Kilole alizungumza kwa lugha ya ukali.
“Pamoja na hivyo lakini tulitakiwa kumsaidia na si kumwacha aangamie, lazima tuoneshe utu katika hili.”
“Lakini kwa nini hutaki kuwa mwelewa, kila kilichotokea nimekifanya kwa ajili yako.”
“Mmh! Una maana huu mpango wa kukamatwa Deus umeufanya wewe?”
“Ndiyo, si ulinikataza nisimuue sasa huu nao unauona mbaya?”
“Kiloleee! Mbona unakuwa na roho mbaya kama mnyama, yaani unamfunga mumeo kwa ajili ya penzi haramu?” Kinape alishtuka. “Kinape kulitafuta penzi lako nimepata dhambi kubwa, hili la Deus mbona dogo.” “Kubwa lipi?”
“Unajua ila ufahamu, kwa Mungu nina kesi ya kujibu juu ya roho za watu watatu niliowaua kwa ajili yako. Ukifanya mchezo wowote Kinape tutawafuata kina Happy.” “Weweee! Unataka kuniambia wewe ndiye uliyemuua Happy?” “Ndiyo.” “Kwa nini?”
Itaendelea
Post a Comment