ad

ad

NYUMA YA MACHOZI - 23


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
“Kinape tuwahi nipo tayari,” Deus alisema huku akimtoa Kilole kifuani kwa Kinape.
“Okay twende.”
“Mbona hujabadili nguo?”
“Mbona nipo sawa.”
“Sasa utakwenda na taulo?” Kinape alipojiangalia akijikuta amejifunga taulo, alikimbilia ndani kubadili kisha walitoka kuwahi hospitali.
SASA ENDELEA...
****
Walipofika walikuta mwili wa Happy ndiyo umefikishwa muda mfupi ukiwa bado upo katika gari la polisi, dada yake Happy alipomuona Kinape alimkimbilia na kujitupa kifuani kwake na kuangua kilio cha sauti.
“Ooh! Shemeji mdogo wangu wamemuua.”
“Hapana si kweli Happy hawezi kufa kirahisi namna hiyo,” Kinape alisema kwa sauti ya juu huku akimkumbatia shemeji yake.
“Kweli mdogo wangu amekufa, yaani wamemuua kama jambaziii...amewakosea nini mdogo wangu mimiii,” dada yake Happy aliendelea kulia akiwa bado amejilaza kifuani.
Wakati huo kitanda cha kuuchukulia mwili wa Happy uliokuwa umefunikwa shuka kilikuwa kimesogezwa karibu kabisa na gari la polisi.
Kinape alijitoa kwenye mikono ya dada yake Happy na kwenda kwenye gari la polisi wakati huo askari walikuwa wakiushusha mwili wa Happy uliokuwa ulifunikwa na shuka jeupe lililojaa damu.
Baada ya kuulaza mwili juu ya kitanda cha magurudumu, Kinape alisogea karibu kabisa akiwa bado haamini kama kweli mpenzi wake Happy amekufa. Aliishika shuka upande wa kichwani na kuanza kuifunua huku mikono ikimtetemeka. Macho yake yalikutana na uso wa Happy aliyeonekana kama umelala.
“Happy mpenzi wangu amka,” alimwita kwa sauti huku akimtikisa taratibu.
“Shemeji amekufa mdogo wangu,” dada Happy ambaye alikuwa akilia kuliko watu wote waliokuwa pale alikwenda kuungana na shemeji yake ambaye alikuwa bado akiona kama kiini macho kilichokuwa mbele yake.
“Happy mpenzi wangu amka huwezi kufa kirahisi mpenzi wangu, huwezi kuniacha peke yangu, leo asubuhi tunakwenda kwa wazazi wangu wakakutambue. Hata kaka Deus yupo hapa ametoa gari ili lake la kifahari ili nikupeleke kijijini...Amka mpenzi amka ni wewe peke yako niliyekuchagua... Hapiiiiiiiiii,” Kinape alimtikisa kwa nguvu ili aamke lakini mwili ule haukuwa na uhai. Kinape alilia kwa uchungu, Deus alimchukua na kumuondoa kwenye kitanda na kumpeleka pembeni kumbembeleza.
“Deus niache huu ni unyama wa hali ya juu, inaniuma kwa nini wamuue mpenzi wangu nimewakosea nini?” alisema huku akipiga chini. “Pole rafiki yangu, kazi ya Mungu haina makosa.” “Noooo, hapana hii si kazi ya Mungu ni mashetani wasiopenda kuona Kinape na Happy wanaoana.”
“Basi...basi, wewe mwanaume unatakiwa kuyashinda maumivu ya moyo wako,” Deus aliendelea kumbembeleza. “Yaani Happy...hata siamini haiwezekani Happy hajafa,” Kinape alimponyoka Deus na kukifuata kitanda kilichokuwa kikielekea chumba cha uchunguzi kabla ya kupelekwa Mochwali. Alichepua mwendo huku akimwita kwa sauti kama anamsikia, lilikuwa pigo mujalabu ambalo hakulitegemea kipindi kile.
“Jamani mnampeleka wapi mpenzi wangu, Happy hajafa amelala mwambieni aamke leo asubuhi nakwenda kumtambulisha kwa wazazi,” kifo cha ghafla cha Happy kilimchanganya Kinape na kuonekana kama chizi. Lakini Deus alimuwahi na kumketisha chini rafiki yake.
“Kinape hebu kuna kuwa na moyo wa kiume.”
“Siwezi, siwezi Deus inauma sana.” “Najua inauma lakini imekwisha tokea kinachotakiwa kutafuta chanzo cha kifo chake.”
Baada ya kuufanyia uchunguzi mwili wa Happy alipelekwa mochwali kwa ajili ya kusubiri kuchukuliwa na kwenda kuzikwa.
****
Kilole alijikuta akijigeuzageuza kitandani akiyakumbuka matukio yote aliyoyafanya usiku ule. Moyo ulimuuma kwa kitendo cha kikatili lakini hakuwa na jinsi ilikuwa lazima afanye vile ili kupata anachokitaka. Matukio yalipokuwa yakijirudia kichwani alikwenda hadi kwenye friji ndogo ya chumbani na kuchukua chupa ya pombe kali na kunywa glasi nzima.
Baada ya kunywa alijikuta akipitiwa na usingizi na kujilaza nusu ya kitanda, Deus aliporudi toka hospitali alishangaa kumkuta mkewe aliyemwacha amelala akiwa katika hali ya ulevi. Alimshtua toka usingizini kwa kumwita na kumtikisa ili alale vizuri.
“Mke wangu.”
“Tafadhali, mimi sijamuua Happy,” Kilole alikurupuka usingizini baada ya kumuona mumewe amemsimamia mbele yake. “Nani kakuambia umemuua?”
“Sa..sa mahani mume wangu,” Kilole alijibu kwa sauti ya kilevi. “Mbona umekunywa pombe?”
“Hivi kweli Happy amekufa?”
“Kweli amekufa.”
“Basi kila dakika ananijia ndotoni, nikaamua bora ninywe pombe kali nilale fofofo.”
“Ooh! Pole sana.”
“Umefikia wapi?”
“Tumerudi kila kitu kitakuwa asubuhi ya leo.”
****
Siku ya pili asubuhi wakiwa sebuleni Kilole na Deus wakimsubiri Kinape atoke chumbani ili wawahi msibani huku macho yao yalikuwa kwenye runinga katika taarifa ya habari ya asubuhi ile. Katika taarifa ile ya habari vilitangazwa vifo vya watu watatu vilivyotokea usiku wa kuamkia siku ile waliouawa kwa risasi.
Mmoja wa maiti hizo alikuwemo mchumba wa Kinape, Happy, wengine waliouawa ni Jimmy mpiga picha na rafiki yake Rich. Deus alishtuka kuona na Jimmy amekufa mtu aliyekuwa akimfahamu kwa kumpiga picha nyingi zikiwemo za birthday na mkewe.
Taarifa ya habari ilielezea kwa ufasaha vifo vile kuwa mwili wa Happy ilikutwa nje ya geti la nyuma yao na miili mingine ya wanaume wawili Jimmy na Rich ilikutwa katika chumba cha Jimmy wote wakiwa wameuawa kwa risasi.
Pia taarifa iliongeza kupitia mashahidi majirani wa nyumba ile kuwa usiku wa saa sita walimuona mwanamke mmoja aliyekuwa amevaa hijabu iliyomziba mwili wote aliyeingia mule ndani.
Kwa vile hawakuwa na wasiwasi naye hawakujishughulisha naye lakini baadaye katikati ya usiku waligundua Jimmy hajafunga mlango kitu ambacho hakikuwa kawaida yake. Walipokwenda ndani ndipo walipokuta tukio lile la kutisha. Zilioneshwa picha za Jimmy na Rich zilivyokuwa zimelala kwenye kochi na sakafuni.
Lakini maiti ya Happy haikuonekana kutokana na kuchelewa kwa taarifa kufika kwenye vyombo vya habari. Kinape aliyekuwa ndiyo anafika sebuleni aliliona tukio lile. Kilichomshtua ni picha ya Jimmy.
“Jamani huyu si Jimmy mpiga picha?”
“Ndiye mwenyewe.”
“Mungu wangu na yeye kafanya nini?”
“Tena nasikia muuaji ni mwanamke,” Deus alimwambia Kinape aliyekuwa amesimama nyuma ya kochi waliokalia. “Mwanamke!” Kinape alishtuka.
“Ndiyo, tena alikuwa amevaa hijabu iliyomzima mwili wote.”
“Unataka kuniambia ndiye aliyemuua Happy?”
“Walaa, mume wangu hawakusema yule mwanamke ni muuaji bali ndiye aliyeingia chumbani kwa Jimmy,” Kilole alipinga kauli ya mumewe.
“Kwa nini ujifiche lazima atakuwa muuaji.”
“Jamani tuachane na hayo tuwahi msibani tukajue nini kinaendelea,” Kinape alikatisha ubishani wa mtu na mkewe.
Wote walinyanyuka kuelea nje kwenye gari, njiani wakiwa ndani ya gari kauli ya Deus kuhusiana na msichana aliyemshtumu kuvaa hijabu ilimshtua na kukumbuka jinsi alivyo mshangaa Kilole aliyekuwa amevaa usiku ule. Alijiuliza kama ni yeye aliyefanya mauaji yale alifanya kwa lengo gani. Alizidi kujiuliza kuhusu kifo cha Happy anaweza kuwa pia ni yeye?
*****
Msibani watu walikuwa wengi huku kila mmoja akizungumza la kwake, wengi walikuwa walionekana na huzuni hasa familia ya Happy baba, mama na dada yake ambaye alilia mpaka kupoteza fahamu. Mashoga zake nao walichanganyikiwa kwani walikuwa katika maandalizi ya harusi ambayo walipanga iwe ya kukata na shoka baada ya kuelezwa siku ile ndiyo ilikuwa ya kwenda kutambulishwa kijijini kwa mchumba wake. Kinape naye muda mwingi alikuwa amekaa chini kutokana na kutokuwa na nguvu za kusimama.
Deus alitumia muda wake mwingi kuwa karibu ya rafiki yake kumfariji kwani kila rafiki na ndugu wa Happy walipolia naye aliporomokwa na machozi. Kila aliyekuwepo msibani uso wake ulijaa simanzi nzito kutokana na kifo Happy msichana aliyekuwa bado mbichi pia mwenye malengo mazito katika maisha yake. Lakini ilikuwa tofauti kwa Kilole na wote waliokuwepo msibani, moyo wake ulijaa furaha kwa kutimiza lengo lake la kuweza kuuvunja uchumba wa Kinape na Happy ambao aliamini hautaunganika mpaka mwisho wa dunia.
Wakati watu wakiendelea kulia huku ibada ikiendelea kabla ya kuuchukua mwili wa Happy haujaenda kupumzishwa Kilole alijikuta akivuta kumbukumbu ya matukio ya kikatili aliyoyafanya jana.
Aliamini kabisa kwa Happy alifanya unyama wa hali ya juu, lakini kwa Jimmy na rafiki yake ilikuwa ni kulipa kisasi cha kubakwa kwani aliamini adhabu ya mbakaji Uarabuni au China ni kifo. Pia alikuwa kutimiza kile alichomuahidi Jimmy kama picha zake zitavuja basi angemfanyia kitu kibaya. Aliamini vifo vyao vilibakia simulizi ndani ya vinywa vya watu.
Alianza kukumbuka jinsi alivyotoka nyumbani baada ya kuhakikisha mume wake amelala fofofo baada ya kumwekea madawa kwenye chakula. Kwanza alimpigia simu Kinape ajue yupo wapi kwani alipanga na yeye siku ile naye angelishwa chakula kile na kulala fofofo ili aweze kutoka bila kutiliwa wasiwasi na mtu.
Lakini simu ya Kinape haikuwa hewani ile haikumsumbua sana japo wasiwasi wake aliwaza huenda wapo pamoja na Happy. Baada ya kuvaa vazi lake lililomziba mwili mzima, alichukua bastora ya mume ambayo aliikagua na kukuta risasi za kutosha.
Alichukua na kiwambo cha kuzuia sauti. (bomba linalowekwa mbele ya bastora au bunduki kuzuia sauti) Baada ya kuviweka vitu vyake vizuri alikwenda hadi kwenye bodaboda na kukodi. “Samahani kaka angu, Masaki shilingi ngapi?”
“Masaki ipi?”
“Mwanzoni kutokea Salenda?”
“Kwa vile usiku buku ishirini.”
“Naomba uniwahishe.”
Baada ya kupanda dereva aliondoa pikipiki kwa mwendo wa kasi kidogo, Alipokaribia nyumba ya kina Happy aliomba ashushwe mbali kidogo. Kwa vile muda ule magari hayakuwa mengi alitumia dakika kumi tu.
“Nina imani umewahi?” dereva wa bodaboda alimuuliza huku akipaki pikipiki. “Ndiyo ila naomba unisubiri hapa.”
“Dada mbona unanitisha?” aliogopa kukabwa.
“Hapana kaka yangu, bado kuna sehemu nakwenda, nafika nyumbani mara moja narudi sasa hivi.”
“Na fedha yangu?” “Chuku hii nikirudi tutapatana tena,” Kilole alipa dereva elfu arobaini.
“Poa wahi basi.”
Kilole alichepua mwendo kuwahi nyumbani kwao na Happy ambapo palikuwa na kipande chenye giza kutokana na nyumba za sehemu ile kuachana eneo kubwa. Alipokaribia alitoa simu yake ambayo aliiseti sauti ambayo muongeaji huwezi kuijua sauti yake mara moja hata laini alikuwa ameinunua siku ileile ambayo ilikuwa haijasajiliwa.
Baada ya kujipanga alipiga simu ya Happy ambaye alikuwa amejilaza kitandani akiwaza safari ya kesho yake ambayo alijiuliza sijui itakuwaje atakapo kutana na wazazi wa Kinape mwanaume aliyemkabidhi moyo wake. Happy aliichukua simu yake na kuitazama namba ambayo ilikuwa ngeni kwake, aliipokea. “Haloo.”
“Haloo Happy hongera shosti.”
“Ya nini?”
“Yaani kumbe kesho unakwenda kutambulishwa ukweni hujanijulisha.”
“Lakini hiyo si kwenda kutambulishwa lakini mambo bado, nikirudi kila kitu kitakuwa wazi, lakini mazungumza na wewe bado asijakufahamu sauti yako?”
“Mimi Betha,” Kilole alimdanganya.
“Betha yupi?”
“Happy hilo si muhimu kama hili ninalotaka kukueleza?”
“Lipi tena hilo?” Happy alishtuka na kujiweka vizuri kitandani. “Najua
naweza kuonekana mbeya lakini lazima niseme juu ya tabia za mchumba wako Kinape.”
“Tabia gani?”
“Japo kweli ni mchumba wako lakini si muaminifu, hivi ninavyozungumza yupo nje ya gari tulilokuja nalo na shoga yangu wakilana denda kibaya zaidi ni jirani na nyumba yenu kweli huu ni ustaarabu?” “U..u..unasema?” Happy aliingia kigugumizi.
“Tena kama unaweza wahi uwafumanie ‘live’ ukichelewa hata dakika kumi Kinape ataondoka.”
“Okay, nakuja.”
Happy bila kumweleza mtu alikurupuka kuwahi kumfumania Kinape, wakati huo Kilole alijiandaa kummaliza baada ya kujua anakuja.
Alitoa bastora na kufunga kiwambo na kumsubiri. Mara alimuona akitokeza kwao akiwa na gauni la kulalia bila hata ya viatu kwani aliamini angevaa kiatu angechelewa kufumania.
Kwa vile alikuwa kwenye giza alimuona Happy akisogea upande ule akipepesa macho, alitumia nafasi ile kumpiga risasi mbili za kifuani upande wa kushoto kama alivyoelekezwa na mumewe Deus jinsi ya kuua adui kwa risasi.
Alimuona Happy akiruka kwa nyuma hakutaka kuona kinachoendelea alichepua kwendo huku akiiweka bastora ndani ya hijabu. Alipofika alimwambia dereva wa bodaboda: “Tuondoke.”
“Tunaelekea wapi?”
“Mikocheni B.”
Itaendelea

No comments

Powered by Blogger.