NYUMA YA MACHOZI - 22

MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
Kauli ya Mose ilizidisha machungu moyoni kwa Teddy na kuamini wazo lake na ushahidi aliopata lilikuwa sahihi. Alijitahidi kutengeneza tabasamu la uongo ili kuvuta muda wa kummaliza Mose. Muda wote alionesha mapenzi mazito yaliyomziba masikio asijue nini kilichokuwa kikiendelea. SASA ENDELEA...
Majira ya saa moja na nusu Teddy aliamini ule ulikuwa muda muafaka kwake kufanya alichokikusudia, hakutaka kumuua Mose kwa bastora kwa kuhofia sauti yake unaweza kufika mbali.
Kwa vile alikuwa amefunga dirisha la chumbani na kuamini sauti haitatoka nje aliona kisu kingefanya kazi yake vizuri kutokana na Mose kulewa sana asingeweza kushindana naye. Wakiwa watupu kitandani Teddy alisema kwa sauti ya mahaba: “Samahani mpenzi.”
“Bila samahani,” Mose alijibu kwa sauti ya kilevi.
“Nakuja mara moja,” Teddy alisema huku akinyanyuka kitandani.
“Basi usichelewe mpenzi, leo moyo wangu una furaha ya ajabu.” “Usihofu leo mimi na wewe mpaka lyamba.”
Teddy alikwenda hadi kwenye kabati na kuchukua kisu kikubwa na kurudi nacho kitandani. Wakati huo Mose alikuwa amejilaza chali akiwa amefumba macho kutokana na kunywa kiasi kikubwa cha pombe. Teddy alimkalia tumboni kama anataka kumuandaa kimahaba. Kwa sauti iliyojaa ukatili isiyo na chembe ya huruma alisema: “Wee mbwa Sali sala yako ya mwisho.”
“Vipi tena mpenzi?” Mose aliuliza huku alijitahidi kufumbua macho yaliyokuwa mazito kutokana kunywa pombe nyingi kupita kiasi. Macho yake hayakuamini kuona Teddy amemshikia kisu.
“Ha! Nini tena?” “Unauliza jibu, nilikueleza nini siku moja?”
“Mpenzi mbona sikuelewi.”
“Nilikueleza toka mwanzo kuwa hutaugusa mwili wangu labda maiti yangu, lakini leo umeugusa nikiwa mzima ni ishara ya kifo chako.” “Kwa hiyo unataka kuniua?”
“Si ulitaka kunipoteza? Sasa nakupoteza wewe.”
“Si..si..nimekueleza sa..sa..babu yake,” Mose alijitetea akiwa bado amelala chali mwili haukuwa na nguvu kutokana na kulewa sana.
“Fedha yote niliyopoteza baada ya kukamatwa itanunua kifo chako,”
Teddy alisema huku akikipunga kisu hewani.
“U..u..usi..ni..”
hakumalizia alikutana na mapigo ya kisu mfululizo yaliyompiga bila mpangilio.
Teddy alimshambulia Mose kwa visu mfululizo kama anatengeneza chujio la nazi. Mose kutokana na ulevi wa kupindukia hakuweza kujitetea.
Baada ya kupiga kelele za maumivu kwa muda bila msaada sauti ilizidi kupungua mpaka aliponyamaza kabisa, wakati huo kitanda kizima kilikuwa kimejaa damu kama kachinjwa ng’ombe ambazo zilizomrukia Teddy mwilini.
Teddy baada ya kuamini amemaliza kazi, alinyanyuka na kukimbilia bafuni kuoga kisha alibadili nguo na kuchukua vitu vya muhimu na kuhakikisha picha zake zote ameondoka nazo. Baada ya kubeba mizigo yake alikodi gari hadi uwanja wa ndege.
Alifika ikiwa imebakia nusu saa ndege iondoke, baada ya kupima mizigo alielekea kwenye ndege na kuketi huku akiomba Mungu aondoke kabla ishu haijashtukiwa. Hakujiamini mpaka ndege alipoondoka katika jiji la Sicily, safari yake ilikwenda vizuri mpaka alipotua katika jiji la Turin salama salimini. Alitafuta hotel yenye hadhi ya nyota tano iitwayo Principi di Piemonte.
Baada ya kupata chumba aliagiza chakula na kula kidogo kwani bado picha ya kitendo cha kinyama alichomfanyia shemeji yake ilijirudia akilini mwake. Aliamua kuagiza pombe kali ambayo alikunywa mpaka alipopoteza mawasiliano na kulala alipokuwa amekaa. Alishtushwa siku ya pili na hodi iliyokuwa ikigongwa.
Alishangaa kujikuta amelala pembeni ya kitanda kwenye zulia. Aliponyanyuka alizidi kujishangaa kukuta haja ndogo aliimalizia pale bila kujielewa kutokana na kunywa pombe nyingi kupita kiasi.
Alinyanyuka na kukimbilia bafuni na kuchukua cha kufutia kisha alifungua mlango.
“Za saizi?” mhudumu alimsalimia. “Nzu..nzuri, karibu.”
“Asante, nilikua naomba kufanya usafi.”
“Kwani sasa hivi ni saa ngapi?”
“Saa tano.” “Ooh! Kumbe nimelala sana.”
“Inaonesha ulikunywa sana.”
“Okay, fanya haraka usafi nataka kupumzika.”
Teddy alimwacha mhudumu afanye usafi, baada ya kufanya usafi alioga na kuagiza kifungua kinywa kisha alizimua kidogo. Akiwa amejipumzisha kwenye sofa huku akinywa whisky taratibu, tukio la jana yake lilimjibu kwenye akili na kujikuta akiwasha luninga labda habari za kifo cha Moze kitatangazwa.
Alifungua luninga ya taifa, alikuta kuna matangazo ya magazeti na moja ya habari iliyotawala kwenye ukurasa wa mbele ilikuwa yake. Kichwa cha habari kilisomeka unyama wa kutisha, juu kulikuwa na picha ya Mose akiwa amelala kitandani mwili wote ukiwa katika dimbwi la damu.
Picha ile ilimtisha alijikuta akifumba macho kwa woga na kuchukua chupa ya whisky na kuipeleka mdomoni kwake na kujaza kiasi kikubwa na kukimeza chote kwa shida huku amefumba macho mpaka mishipa ya kichwa ikamsimama, baada ya kutikisa kichwa alisema kwa sauti ya chini.
“Ooh! Mungu wangu, nimemuua Mose kifo kibaya sana.”
Akiwa ameinamisha kichwa huku akisikitika na machozi kumtoka kutokana na unyama aliofanya, alinyanyua macho na kushtuka kuona Mose hakufa yupo hospitali ila katika chumba cha wagonjwa mahututi. Akiwa bado anatumbulia macho habari za Mose ambaye alionekana mfu.
Alimuona mkuu wa makosa ya jinai akitoa taarifa kuwa mpaka muda ule upelelezi ulikuwa unaendelea ili kujua nani aliyefanya tukio la kikatili kama lile baada ya kukosa ushirikiano wa mgonjwa ambaye alikutwa katika hali mbaya mpaka wakati ule alikuwa akipumua kwa mashine. Taarifa za daktari zilisema mgonjwa kutokana na kupoteza damu nyingi kutokana na kutobolewa na kitu chenye ncha kali aliongezwa damu zaidi ya chupa kumi.
Habari zile hazikumfurahisha hata kidogo Teddy na kuamini kama Mose atapona na kutoa ushahidi basi atamtia kwenye matatizo makubwa na akishikwa adhabu yake ni kifo. Wazo la haraka lilikuwa kuondoka ndani ya nchi ya Italy na kwenda kuishi Afrika kati ya nchi ya Tanzania au Kenya. Aliamini upelelezi lazima utajua kuwa ni yeye mhusika aliwasiliana na washirika wake na kukubaliana akajifiche Kenya mpaka hapo mambo yatakapojulikana yamefikia wapi.
Bila kupoteza muda alipanda ndege moja kwa moja mpaka Kenya na kwenye kujificha katika jiji la Nairobi katika jumba moja la mshirika wao lililokuwa na kila kitu ndani maeneo ya Kasalani. Mwezi mmoja akiwa anaishi kwa kificho katika jiji la Nairobi aliziona habari na picha yake za kutafutwa kwake kuhusiana na jaribio la kutaka kumuua Mose.
Baadhi ya vyombo vya habari na luninga alitoa kila siku sura ya Teddy kutafutwa huku donge nono likitangazwa kwa mtu atakayetoa habari zake na kufanikisha kukamatwa. Taarifa zile zilizidi kumficha Teddy ambaye alikuwa akitoka usiku tu kwenda club za usiku na baada ya hapo alishinda ndani tu. Aliweza kumuona Mose katika hali ya umajeruhi kutokana na shambulio kali la kutaka kumuua.
Mwili wake ilionesha kuharibika vibaya hata kuzungumza kwake alizungumza kwa shida. Katika mahojiano na mwandishi wa habari mmoja alimsikia akisema kuwa akipona atamtafuta popote hata kaburini ili kulipa kisasi.
****
Majira ya saa sita za usiku Kinape alijirudisha nyumbani kwa kuamini muda ule Kilole atakuwa amelala. Alipokaribia nyumbani aliona teksi ikisimama mbele kidogo na nyumbani kwao. Aliendelea kusogea kwa vile alikuwa upande wa giza aliweza kuliona lile gari ambalo hata namba zake hazikuwa ngumu kuzinakili kichwani.
Kabla ya kupiga hatua alishangaa kumuona mwanamke aliyevaa hijabu na nikabu iliyomziba uso wake akitelemka kwenye teksi na kuelekea kwenye geti la nyumba yao na gari ile kuondoka. Alijuliza ni nani aliyevaa vazi lile kuelekea kwao muda kama ule. Ilibidi atembee kwa taadhari ili kujua yule mwanamke anakwenda kufanya nini kwao muda ule.
Alisimama nje ya uzio na kuweza kumuona yule mwanamke akifungua mlango kwa taadhari kubwa, alijiuliza yule mwanamke ni nani au mwizi. Hakutaka kumshtua alitulia kutaka kuona mwisho wake, lakini kilichomshangaza kilikuwa kufungwa mlango kwa ndani. Moja kwa moja alijua yule ni Kilole, lakini swali lilikuwa usiku ule anatoka wapi na katika vazi lile ambalo hakuwahi kuliona hata siku moja.
Hakutaka kupitia mlango wa mbale alizunguka nyuma na kuingia chumbani kwake kwa kutumia dirisha. Mara zote anapojua anachelewa kurudi alilitegesha dirisha na aliporudi aliingilia kupitia dirishani.
Baada ya kuingia ndani alibadili nguo na kwenda kuoga na kurudi kulala ili alfajiri awahi kuamka kabla Kilole hajaamka. Alikumbuka muda wote alizima simu ili kumkwepa Kilole asimsumbue, alipowasha haikuchukua muda simu iliita. Ilikuwa simu ya dada ya mchumba wake, aliipokea. “Haloo shemu.”
“She..she..mu,” hakuendelea kuzungumza alivuta kamasi za kilio kitu kilichomshtua Kinape na kutaka kujua kuna nini, kwani simu ilikuwa hewani kwa mbali alisikia sauti kama za vilio.
“Haloo shemu,” aliita lakini upande wa pili haukupokea zaidi ya kuendelea kusikia vilio vya upande wa pili.
Aliamua kukata simu na kupiga, iliitaka kwa muda mfupi ilipokelewa upande wa pili na dada ya mchumba wake.
“Shemu upo wapi?” aliulizwa.
“Nyumbani.”
“Una habari gani za Happy?” “Sina! Amefanya nini?” alishtuka.
“Amefariki.”
“Nini?” Kinape alishtuka. “Amefariki,” kauli ile ilirudiwa. “Muongo acha kunirusha roho shemeji.”
“Si kukurusha roho ukweli ni huo mchumba wake ameuawa saa mbili zilizopita.”
“Hapana sikubali Happy hawezi kufa kirahisi namna hiyo nimeachana naye jioni akiwa na mzima wa afya.”
“Hakufa kwa ugonjwa.”
“Nini kimemuua mpenzi wangu?” “Ameuawa.”
“Nini?”
“Ameuawa.”
“Na nani?”
“Hatujajua ile sasa hivi tunaupeleka mwili wa Happy hospitali.”
“Nakuja sasa hivi.”
Kinape alikata simu na kujikuta akichanganyikiwa kwa kuvaa fulana na taulo. Alikwenda moja kwa moja kugonga katika mlango wa Deus kumjulisha taarifa za mchumba wake Happy.
Aligonga mlango kwa muda, Deus aliyekuwa kama yupo ndotoni alishtuka na kunyanyuka hadi mlango. Alipofungua alikutana na Kinape aliyekuwa akitokwa na mchozi na macho yalikuwa mekundu kuonesha ana tatizo zito.
Deus alishtuka na kutaka kujua rafiki yake kipi kimemsibu usiku mkubwa kama ule.
“Best vipi?” Kinape alishindwa kuzungumza alijitupa kifuani kwa Deus na kuangua kilio bila kusema neno.
“Best kuna nini?”
“Happy.”
“Happy amefanya nini?”
“Amefariki.”
“Wewe! Acha utani, si leo asubuhi mnakwenda kijijini?” Deus alishtuka na kumshika Kinape mabegani na kumsogeza mbele yake ili kumtazama vizuri.
“Ndiyo, lakini nimepigiwa simu muda huu amefariki.”
“Alikuwa akiumwa?” “Hapana.”
“Nini kimemuua?”
“Na..na..sikia.. ameuawa.” “Ameuawa! Na nani?”
“Hata wao hawajui.”
“Mwili wa marehemu upo wapi?” “Wameniambia ndiyo wapo njiani kuupeleka hospitali.”
“Unasema kauawa, kivipi?”
“Hata najua, nakwenda kujua huko huko.”
“Nisubiri basi tuongozane.”
Deus alirudi chumbani kumjulisha mkewe habari za Happy.
“Mke wangu,” alimwita huku akimtikisa.
“A.aa..bee mume wangu.” “Kuna tatizo limetokea.” “Tatizo gani tena?” Kilole aliuliza huku akifikicha macho. “Happy amefariki.”
“Nini?” Kilole aliuliza kwa mshtuko. “Happy amefariki.”
“Acha utani, Happy mchumba wa shemeji Kinape?”
“Ndiyo.”
“Muongo, si kesho wanakwenda kijijini kumtambulisha?”
“Ndiyo.”
“Nini kimemuua?”
“Nasikia ameuawa saa mbili zilizopita.”
“Sasa inatakuwaje, kwani Kinape yupo wapi?” “Yupo ananisubiri twende hospitali.”
“Sasa hospitali kufanya nini ikiwa mnasema amekwisha kufa?”
“Wamesema wanaupeleka mwili wa marehemu.”
“Kwa hiyo twende wote?”
”Hapana nilikuwa nakutaarifu tu.”
Wakati Deus akibadili nguo ili awahi hospitali, Kilole alitoka nje na kilio hadi kwa Kinape na kujitupa kifuani kwake.
“Maskini shemeji yangu nini kimemsibu mke mwenzangu?”
“Ha..ha..ta sijui.”
“Kinape tuwahi nipo tayari,” Deus alisema huku akimtoa Kilole kifuani kwa Kinape.
“Okay twende.”
“Mbona hujabadili nguo?”
“Mbona nipo sawa.”
“Sasa utakwenda na taulo?”
Kinape alipojiangalia akijikuta amejifunga taulo, alikimbilia ndani kubadili kisha walitoka kuwahi hospitali.
Itaendelea
Post a Comment