Tamko la Chadema baada ya kukamatwa mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea jana
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
Kama ambavyo
imeripotiwa kwenye vyombo vya habari na njia zingine za upashanaji habari tangu
jana kuwa Mbunge wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya CHADEMA, Ndugu Saed Kubenea
aliwekwa chini ya ulinzi na kuamriwa kwenda kituo cha polisi kwa amri ya Mkuu
wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ambaye inadaiwa hakutaka mbunge huyo
azungumze na wananchi ambao ni Wafanyakazi wa Kiwanda cha Tanzania Took
Garment, waliokuwa wamemuita mbunge huyo kwa ajili ya kumweleza matatizo
wanayokumbana nayo kazini hapo, ikiwa ni pamoja na ujira kidogo na mazingira
magumu ya kazi.
Aidha
akitambua kuwa alichofanya matumizi mabaya ya dhamana ya uongozi, hivyo
akakusudia kuficha umma usijue uovu huo, katika tukio hilo Makonda aliwaagiza polisi wakamate kamera za
waandishi wa habari waliokuwa katika eneo hilo wakitimiza wajibu wao wa kikazi
na kitaaluma kwa jamii.
Katika hatua
ya sasa, tunaomba kusema ifuatavyo;
1.
Tukitambua kuwa mamlaka ya DC kuamuru watu kukamatwa yamefafanuliwa kisheria na
kuwekewa mipaka yake ambayo Makonda amedhihirisha kuivuka katika nyakati
tofauti sasa, Mkuu huyo wa wilaya hana mamlaka ya kisheria wala ya kisiasa
kuhalalisha amri aliyoitoa ya kumkamata mbunge, tena aliyekuwa anatekeleza
wajibu wake, tunamtaka DC Makonda amwachie Ndugu Kubenea mara moja huku tukitoa
wito kwa mamlaka zilizomteua kumwangalia kwa makini kama bado anazo sifa za
kuwa kiongozi wa ngazi hiyo.
2. Kwa kuwa
amri hiyo si halali kwa sababu haina msingi wowote wa kisheria, tunatoa wito
kwa Jeshi la Polisi kumuachia Ndugu Kubenea ili aendelee na uhuru wake huku
akitekeleza wajibu wake wa kuwawakilisha wananchi wa Ubungo badala ya kumsumbua
kwa mambo yasiyokuwa ya msingi.
3.
Halikadhalika, Jeshi hilo liwarudishie waandishi wa habari vifaa vyao vya kazi
vikiwa katika hali salama na bila athari yoyote ama ya vifaa vyenyewe au
materials yaliyoko ndani yake.
4.
Tunalitaka Jeshi la Polisi kutoa kauli ya kuwahakikishia usalama waandishi wa
habari na vifaa vyao kila wanapotimiza wajibu wao kwenye matukio yanayomhusisha
Makonda kwa sababu tayari ushahidi unaonesha anaweza kuwa tishio kwao binafsi
na vitendea kazi vyao hususan pia wanapokuwepo polisi.
5. Kwa
kitendo cha DC Makonda kuamuru kiongozi wa wananchi akamatwe bila kuwepo kosa
lolote la kisheria, CHADEMA tutachukua hatua za kisheria dhidi ya DC huyo ili
liwe fundisho kwake mwenyewe, wakuu wa wilaya wengine na utawala mzima wa
Serikali ya CCM chini ya Rais John Magufuli, ili watambue kuwa suala la
kuongoza nchi kwa kuzingatia Haki, Katiba, Sheria na taratibu si suala la
kupenda bali ni lazima kuzingatiwa kwa ajili ya amani na utulivu wa kweli.
Tutachukua
hatua hizo huku tayari kukiwa na kumbukumbu za Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora (THBU) ambayo hivi karibuni ilimuonya DC Makonda na wakuu wa
wilaya wengine na wakuu wa mikoa ambao wameanza tabia ya kuendesha nchi kwa
amri ambazo hazina uhalali wowote zikiwa nje ya mamlaka yao ya kisheria kufanya
hivyo.
Tuliamini
angalizo hilo la THUB ambacho ni chombo huru cha serikali, lingeweza kuwa
mwongozo sahihi kwa viongozi wa serikali na kwamba kosa la awali la Makonda
kuwaweka mahabusu watumishi wa Wilaya ya Kinondoni walioko chini yake
lingechukuliwa kama fundisho kwake, lakini bahati mbaya watawala wanaweka nta
masikioni linapofika suala la haki za binadamu na uongozi bora.
Imetolewa
leo Jumanne, Nov. 15, 2015 na;
Tumaini
Makene
Mkuu wa
Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

Post a Comment