Niyonzima siyo ishu, Pluijm ataka mabao
Dar es Salaam
MBUYU Twite amepewa jukumu la unahodha wa Yanga, lakini timu hiyo imesema haioni athari za kutokuwa na kiungo Haruna Niyonzima badala yake inakinoa zaidi kikosi chake ili kipate mabao mengi.
Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, ameamua kumpa unahodha Twite kwani nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ni majeruhi na msaidizi wake ambaye ni Niyonzima amesimamishwa.
“Haina haja ya kusumbua kichwa, nina wachezaji wazoefu sana wenye uwezo wa kuongoza timu. Sina manahodha wote kwa sasa, lakini Mbuyu ndiye atachukua jukumu hilo,” alisema Pluijm.
“Twite ndiye nahodha namba tatu baada ya Cannavaro na Haruna.”
Kuhusu kukosekana kwa Niyonzima kikosini, Pluijm alisema: “Muhimu ni kupata suluhisho lake, sioni pengo la Niyonzima japokuwa ni mtu muhimu kwetu. Hapa nina wachezaji wengi wa kucheza nafasi yake.
“Hata hivyo, kama kocha natamani amalize haraka matatizo yake na uongozi ili ajiunge nasi kikosini kwani ninafahamu kinachoendelea kwake.”
Niyonzima amesimamishwa Yanga baada ya kuchelewa kuripoti kwa siku 12 tangu kumalizika kwa michuano ya Kombe la Chalenji huko Ethiopia akiichezea Rwanda.
Wakati huohuo, Kocha wa Yanga, Pluijm ambaye leo timu yake inacheza na Stand United kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika Ligi Kuu Bara, amesema anataka kikosi chake kipate mabao mengi katika kila mechi.
“Nimeona kuna kila sababu ya kutengeneza mabao, tunataka kupata mabao ya kutosha kwenye michezo yetu, najua Stand ni timu ngumu lakini nitahakikisha vijana wanafanya vizuri,” alisema Pluijm.

Post a Comment