HADITHI: Msafara wa Mamba - 06

MTUNZI: Ally Mbetu ‘DR AMBE’
ILIPOISHIA:
"Kufa shetani mkubwa wee," mama kwa hasira alichukua chupa nyingine ya pombe iliyokuwa juu ya meza ili amuyongeze mzungu aliyekuwa ameanguika chini, lakini nilimuwahi ili asimuumize zaidi.
"Mama basi utamuua."
"Wacha afe mshenzi hawezi kunichezea mimi na mwanangu, kwanza kwa kipi hasa?" Mama alikuwa amepandisha hasira.
"Mama tupige simu polisi," nilimshauri.
"Tena kweli na lazima afie gerezani."
Mama alipiga simu polisi baada ya muda polisi walifika na kumchukua yule mzungu na kumfungulia kosa la kubaka.
SASA ENDELEA…
******
Baada ya kuvunja mahusiano na mzungu, mama aliamua kuachana na wanaume na kuendelea na biashara zetu. Pamoja na kutokuwa na mtu wa kutufadhiri hali ya kimaisha haikuwa mbaya, vilevile nilimshukuru Mungu mama yangu kutulia na kuachana na wanaume.
Maisha yalikuwa mazuri tuliweza kufurahia maisha bila kuwa tegemezi, nami niliendelea kusoma bila tatizo lolote, mama aliyatamani yale maisha tungeishi tokea awali. Kwa kweli mama yangu alipendeza na kurudisha heshima iliyopotea.
Mwaka mmoja baadaye mama alianza kusumbuliwa na maradhi yasiyoeleweka, Mara leo kichwa kesho miguu kukosa hamu ya kula, ile hali nilimshauri mama twende hospitali. Lakini mama alikataa kwa kusema.
"Herena mwanangu wanadamu siwema, lazima wameniroga kutokana na maisha yetu kuonesha maendeleo."
"Sawa mama, lakini twende hospitali kwanza."
"Hapana twende kwa mganga, nina mganga wangu mmoja lazima atanieleza ukweli."
Basi sikuwa na jinsi nilikubaliana na mama kwenda kwa mtaalamu wa miti shamba. Tulipokwenda mama alipewa dawa nyingi za kunywa na kuoga, japo hali ya mama ilikuwa na unafuu kidogo lakini haikumuwezesha kufanya kazi zaidi ya kushinda ndani.
Matibabu ya mama yalikula pesa nyingi, tulijikuta tukiyumba kiuwezo na kufikia hatua ya duka kufilisika na mimi pesa zote benki kukatika. Utafikili labda ulisubiri pesa zituishie ndipo ugonjwa wa mama uzidi.
Nilichanganyikiwa mtoto wa kike hali ya mama ilikuwa mbaya na pesa zilikuwa zimetuishia. Nilijiuliza niende wapi kuomba msaada, wazo lilikuja niende kwa mjomba wa benki nikamuelezee hali halisi ili anisaidie.
Siku ya pili nilikwenda hadi benki kwa mjomba, aliponiona alinikarisha kwa heshima zote, kitu kilichonipa moyo wa kusaidiwa.
"Herena za siku mbona umepotea sana?"
Ajabu badala ya kumjibu nilianza kububujikwa na machozi kitu kilichomshtua mjomba na kuhoji.
"Herena vipi mbona unanidondoshea machozi?"
Sikumjibu upesi niliendelea kuinama nikiendelea kudondosha machozi, Anko aliponiona simjibu na kuendelea kudondosha machozi alinyanyuka kwenye kiti chake na kuzunguka kunifuata nilipokuwa nimekaa.
"Herena kuna nini tena mbona unanitisha?" Aliniuliza huku akinikanda mabegani.
"Hali ya mama ni mbaya sana."
"Ooh pole sana, anasumbuliwa na nini?" Aliondoa mkono mabegani na kuzichezea nywele zangu chache.
"Hata sijui kila siku hali yake inazidi kubadilika."
"Mm’hu kumbe ndilo hilo, vipi hospitali mmekwenda?"
"Hataki anang’ang’ania kwa waganga wa kienyeji."
"Sasa alikuwa unahitaji nini kwangu?"
"Msaada Anko."
"Msaada upi huo?"
"Wa pesa."
"Mmh, Herena najua unaelewa ugumu wa maisha kwa sasa," alizungumza huku akizunguka meza na kurudi kwenye kiti chake.
"Ndiyo" nilijibu kwa kifupi.
"Unataka kuniambia nitamsaidia kivipi ikiwa hata familia yangu ina matatizo nayo inanitegemea mimi?"
"Anko kiasi chochote kila sio lazima kiwe kikubwa."
"Herenaaa, dunia hii ya leo pesa haitoki bure nina imani we mkubwa sasa una miaka mingapi?"
"Anko miaka yangu ya nini?"
"Herena hebu nijibu sihitaji swali."
" 19."
"Mmh, umekuwa mtu mzima una uwezo wa kumsaidia mama yako."
"Kumsaidia kivipi na kazi sina."
"Upo tayari kumsaidia mama yako?"
"Sijakuelewa kivipi?" Nilishindwa kumwelewa Anko.
"Ukipata kazi nyepesi yenye malipo makubwa."
"Nipo tayari kama nikiipata," alijibu bila kujua kazi hiyo.
"Ok, njoo leo saa mbili usiku pale ABC Hotel."
"Aah, Anko kama kazi ya hotel nitapata muda gani wa kusoma?"
"Herena mbona unakuwa si muelewa, nani amekwambia kazi ya hotelini."
"Sawa Anko nitakuja."
Nilinyanyuka ili niondoke nilipogeuka ili niondoke Anko aliniita.
"Herena."
"Abee Anko," niliitika huku nikigeuka kumwangalia.
Bila kusema kitu aliinama na kuvuta droo na kutoa pesa.
"Herena hizi zitakusaidia kwa matumizi ya leo na nauli, usikose sawa?"
"Sawa Anko Mungu akuzidishie," nilimshukuru Anko huku nikizipokea pesa ambazo sikuzihesabu.
"Atuzidishie sote."
Baada ya kuzipokea niligeuka na kuondoka huku moyoni nikimshukuru Anko kwa kuonesha utu japo maneno ya mama kuonekana kumchefua. Nilijikuta nikiionea wivu familia yake kwa kuwa na mzazi wenye ubinaadamu.
Nilipofika nje ya ofisi nilizihesabu zile pesa nilizopewa, sikuamini macho yangu pale nilipokuta laki mbili taslimu. Nilibadili wazo la kupanda daladala na kukodi bajaj, kwanza nilipitia sokoni na kununua mahitaji muhimu ambayo nyumbani hayakuwepo pamoja na dawa za mama zilizokuwa zimekwisha. Mahitahi yangu yote nilitumia elfu sitini.
Nilirudi nyumbani na kumweleza mama jinsi Anko alivyonisaidia na jinsi alivyodhamilia kunisaidia zaidi kwa ajili ya kazi ya muda mfupi na kupata pesa kidogo za kuweza kumsaidia. Nilimuona mama yangu akilia na kujuta kuachana na Anko na maneno machafu aliyomtolea.
"Herena mwanangu nikipata nguvu kidogo nitakwenda kumuomba msamaha."
"Ndicho kilichobaki, kwa jinsi ninavyomjua lazima atakusamehe."
Baada ya shughuli za siku nzima, nilifanya kazi zangu harakaharaka ili kuwahi miadi na Anko ABC saa mbili usiku. Majira ya saa moja baada ya kumuogesha mama na kumpatia chakula cha usiku nilimuaga mama ili nimuwahi Anko asije kukasirika.
Nilikodi bodaboda hadi ABC Hotel njia nzima nilikuwa najifikilia ni kazi gani hiyo mpaka tukutane hotelini. Lakini wazo lingine liliniambia huenda ni kunikutanisha na wakubwa wenzake ambao watanipa kazi kama mtoto wake, nilifuata maelekezo kama alivyonielezea.
Nilipokelewa na muhudumu na kunielekeza sehemu ya kumsubiri Anko. Aliniuliza natumia kinywaji gani, nilimjibu soda japo nilikuwa na hamu ya bia ya baridi.
Nikiwa pembeni ya ukumbi nikinywa soda yangu taratibu, nilishtushwa na mkono alionigusa begani nilipogeuka nilikutana na Anko.
Nini kitaendelea? Endelea kufuatilia.
Post a Comment