HADITHI: Msafara wa Mamba - 07

MTUNZI: Ally Mbetu ‘DR AMBE’
ILIPOISHIA:
Nilipokelewa na muhudumu na kunielekeza sehemu ya kumsubiri Anko. Aliniuliza natumia kinywaji gani, nilimjibu soda japo nilikuwa na hamu ya bia ya baridi.
Nikiwa pembeni ya ukumbi nikinywa soda yangu taratibu, nilishtushwa na mkono alionigusa begani nilipogeuka nilikutana na Anko.
"Aaah kumbe Anko, karibu."
"Asante, Helena umenifurahisha sana kwa kwenda na wakati nina imani hata hiyo kazi utaifanya vizuri na kupata malipo manono."
"Nitashukuru Anko maana hali ni mbaya sana."
Anko alivuta kiti na kukaa karibu yangu, huku akinichanulia tabasamu aliniuliza.
"Vipi mama yako anaendeleaje?"
"Aaah kidogo hajambo japo bado."
"Nina imani mambo yatakuwa mazuri baada ya leo."
"Hata mimi ndilo ninalo liomba kila siku."
Anko aliagiza pombe kali na kuanza kunywa taratibu na mimi nilikunywa soda yangu taratibu huku nikiwa na shauku kujua ni kazi gani hiyo nyepesi yenye malipo manono.
"Herena mbona unakunywa soda? hujawahi kunywa pombe?"
"Mara moja moja sana."
"Ooh, usiniogope kunywa hii au unataka bia?"
"Kilimanjaro ya baridi."
Nililetewa kilimanjaro ya baridi na kunywa taratibu huku nikisubiri kuelekezwa hiyo kazi. Nilijikuta nakata bia ya tatu bila kusikia lolote, mara ililetwa nyama choma ambayo tuliishambulia wote.
Muda wote sikuwa na wasiwasi wowote kutokana nilivyokuwa na Anko. Nilijikuta nikichanganya vinywaji vikali na baridi, mwisho kilichoendelea sikujua. Niliposhtuka nilijikuta kitandani nimelala na pembeni yangu kulikuwa na mwanaume amelala.
Nilipojichunguza vizuri nilijikuta sina nguo yoyote zaidi ya shuka niliyojifunika. Nilijikuta nikipandwa na gadhabu na kujiuliza ina maana kazi nyepesi aliyonitafutia Anko ni ukahaba. Nilipeleka mkono sehemu za siri na kujikuta nimeingiliwa.
Roho iliniuma sikuamini kama kweli Anko ndiye aliyenipeleka kwenye kazi ile au aliniacha na mtu kunichukua kama msamalia mwema na kunigeuza kitoweo. Mtu aliyekuwa amelala pembeni yangu ambaye alionekana eneo la kifua lililokuwa limesheheni manyoya, alikuwa bado kwenye usingizi mzito tena akikoloma.
Nilijikuta napata wazo na kuchukua kitu chocho kilichokuwemo mule ndani nimpige nacho kwa kitendo cha kuniingilia bila idhini yangu.
Nilijinyanyua kitandani huku nikiwa na hasira kwa kitendo nilichotendewa na mtu ambaye alikuwa kwenye usingizi mzito.
Nilisimama na kuivuta ile shuka ili nifuate nguo zangu, sikuamini kukuta yule mwanaume aliyekuwa uchi wa mnyama ni Anko. Nilijikuta nguvu zikiniisha na kuhisi kizunguzungu na kuanguka chini kilichoendelea sikujua. Nilipozinduka nilijikuta nikiwa nimelazwa kitandani nikiwa na nguo zangu. Niliposhtuka nilimuona daktari akiwa amesimama pembeni yangu.
Nilijiuliza pale nimefikaje na kwa nini nipo kitandani ikionesha ni mgonjwa. Anko alikuwa amesimama pembeni akifuta jasho kwenye paji la uso, nilitulia tuli nikiwaangalia wote waliokuwemo mule chumbani.
Taratibu kumbukumbu zilinirudia na kujikuta nikianza kulia na kutaka kunyanyuka kitandani huku nikisema kwa uchungu
"Ankoooo.. kwanini Anko?"
Kabla ya kunijibu nilimuona akimpa ishara yule daktari atoke nje ya chumba naye alifanya hivyo. Chumbani tulibakia wawili tu, nilinyanyuka na kutaka kusimama lakini alinishika kifuani na kunirudisha kitandani.
"Herena hebu tulia."
"Hapana Anko kwa nini umenifanya hivi au kwa ajili ya umasikini wangu?"
"Hapana Herena nina malengo mazuri sana kwako."
"Anko..Anko..ya.a.ani huwezi kunisaidia hadi unitumie, ni unyama gani huu?" nilijikuta nikilia kwa uchungu na kukumbuka maisha ya tabu ya mama yangu ndiyo yaliyopelekea niwe kwenye hali ile."
"Usifikilie hivyo mimi siwezi kukutumia ila nataka uwe mke wangu mdogo."
"Anko ni uchafu gani huo yaani utembee na mama yangu halafu utembee na mimi? Hata siku moja."
"Sikiliza Herena usiwe mjinga mimi sina uhusiano wowote na wewe lakini nimekuwa nikikusaidia kwa kiasi kikubwa. Nina imani nikikuoa kabisa matatizo ya mama yako tutayatatua kwa kiasi kikubwa. Kama kutokea imeisha tokea, hivi mimi ni kiumbe gani nitakaye fanya kazi isiyo na malipo."
"Anko Mungu angekulipia."
"Herena unanichekesha, ni nani aliyekweenda kwa Mungu akarudi akasema amelipwa malipo kwa matendo yake mema. Siku malipo ya duniani ubakia duniani na ndio maana tunafanya kazi na kupata mshahara na hatusubuiri malipo ya kwa Mungu si tungekufa njaa.
“Sikiliza mipango yangu kwako ni ya muda mrefu toka mama yako alipokata mahusiano na mimi. Herena kilichotokea nina imani hutakijutia ila jione kiumbe mwenye bahati, hebu fikilia leo nakupa laki tano siku ya mwanzo wa mahusiano yetu nina imani huu ni ukurasa mpya wa ukombozi wa maisha yenu..Kamata hizi."
Alinipa burungutu la pesa na kunikabidhi mkononi, nilisita kuzipokea lakini alining'ang'aniza. Nilijua yameisha tokea na hali ya mama ni mbaya na pa kukimbilia sina niliamua kuzipokea.
Baada ya kuzipokea nilifuta machozi kwa kwenda bafuni kunawa uso, niliporudi nilimkuta Anko akinisubiri na kuniambia.
"Herena nina imani jioni tutakutana hapa hapa, nina mpango wa kumpeleka hospitali mama yako kwa ghalama yoyote."
Nilijikuta nikijilamu kwa kumchukia Anko ambaye hakunipunguza kitu chochote hata nikiendelea naye bado nitabakia Herena yule yule. Vilevile tatizo la ukata na matibabu ya mama yatapata ufumbuzi. Nilimkubalia Anko kukutana naye jioni, tuliagana na kunipa elfu 50 za nauli ya kuja jioni. Jumla ya pesa alizonipa siku ile zilikuwa laki nane, yaani asubuhi ya jana laki mbili na nusu na usiku laki tano na nusu.
Nilirudi nyumbani na kumkuta mama akiwa amelala, sikutaka kumwamsha kwa vile nilikuwa nimeisha kula, nuilikwenda bafuni kuoga na kupanda kitandani. Asubuhi nilikutana na mama ambaye alitaka kujua hatma ya safari yangu.
Nilimdanganya mama kuwa mambo si mabaya ila nimetakiwa kurudi jioni ya siku ile. Nilimficha mama kuwa nimepata pesa, nilijua lazima atakuwa na wasiwasi na kutaka kujua pesa zote zile kwa kazi gani, nilizificha ndani kwa ajili ya kututatulia matatizo yetu.
***
Kuanzia siku ile nikawa nyumba ndogo ya Anko nikiwa nimemrithi mama yangu mzazi. Lakini ilikuwa siri kubwa ambayo mama hakuijua, na matibabu ya mama yalikuwa mazuri yaliyorudisha hali ya mama upya.
Kwa kweli maisha yalikuwa mazuri na Anko kukubali kutusaidia kwa kisingizio ananiona kama mwanaye wa kuzaa. Sikuwa na sababu ya kuacha kunihudumia kiumbe nisiye na hatia, mmh kumbe tulikuwa tunamla mama kisogo.
Shule niliendelea kama kawaida, sikuwa tena yule Herena msichana mbishi mwenye msimamo mkali kwa walimu wapenda ngono. Siku za nyuma nilikuwa nipo tayari kuadhibiwa na walimu niliowakataa kimapenzi. Lakini baada ya kujua faida ya mwili wangu wa kunisaidia kwenye matatizo, sikuwa tena mbishi, mwalimu alipotaka kuniadhibu bila kosa nilimuuliza tatizo nini, jibu aliniambia kwani sijui, basi nilimwambia anione kwa wakati wake.
Herena nilijikuta nikipoteza mwelekeo kwa kuwa mama huruma kwa kugawa mapenzi ovyo bila kuhofia hatari iliyopo mbele yangu.
********
Siku zilivyozidi kwenda nilijikuta hata hamu ya masomo inapotea na muda mwingi nilifikilia mapenzi hasa penzi la Anko. Nlijikuta nikiacha shule kwa sababu ya ugomvi wa kila siku na wanafunzi wenzangu juu ya kuchangia mabwana yaani walimu.
Kingine ni ile hali ya kuutoa mwili wangu bure kwa walimu na pindi nikataapo huambulia adhabu kali. Ajabu ilikuwa tofauti na awali nilipomueleza Anko juu ya uamuzi wangu wa kuacha shule, aliupokea kwa mikono miwili. Hakuonyesha kunijutia kwa uamuzi wangu mgumu, alinieleza kitu ambacho kwa kweli siku ile nilikufurahia sana kumbe...Anko alinieleza kuwa.
"Herena kusoma kote ni kwa ajili ya kupata pesa kama una mtu mwenye pesa kusoma kuna maana gani? Unakosa nini Helena muda si mrefu nitakamilisha jumba lako la kifahari pamoja na usafiri wa nguvu.
“ Wewe sasa hivi hutakiwi kuumiza akili yako bali kuituliza na kula raha ya maisha, au hujui wanaume tumeumbwa kuwatafutia wanawake. Herena maisha mazuri yanakusogelea kwani hujui kusoma?"
"Najua." nilimjibu huku nikimtazama usoni, wakati huo nilikuwa nimemlalia mapajani tukiwa juu ya kitanda ndani ya nyumba ya wageni.
"Kingereza unaongea kwa ufasaha sasa tatizo nini?"
"Hakuna mpenzi."
"Hapo ndipo ninapokupendea, unajua mama yako angekuwa kama wewe sasa hivi ningekuwa nimemjengea ghorofa lakini kwa vile ameichezea bahati nafasi hiyo ni yako. Kula raha mtoto wa kike umri bado unaruhusu."
Yalikuwa maneno yaliyonivimbisha kichwa na kujiona mimi ndiye mimi, ni mwanamke niliye bahatika kuliko wanawake wote. Baada ya kuacha shule kwa kweli sikuwa Herena yule uliyenizoea, muda mwingi niliutumia kujipodoa na kuvaa nguo za gharama.
Pamoja na kufanya upuuzi ule sikumuacha mbali mama yangu nilimpa kipa umbele katika kumshughulikia matibabu yake. Kwa kweli pesa haishindwi na kitu. Mama alijenga afya yake kwa mara nyingine, kwa kweli mama alinishukuru kwa kuyaokoa maisha yake.
Uamuzi wa kuacha shule nilipomweleza mama kwanza alikuja juu, lakini nilimueleza sababu za muhimu moja walimu kunitaka kwa nguvu kimapenzi na Anko kuamua nipumzike huku akinitafutia shule nyingine. Nilitengeneza uongo ambao mama aliukubali.
Kuanzia hapo hakuna aliyeulizia maisha yangu zaidi ya kila kukicha kuongeza huduma nyumbani. Siku moja mama aliniambia kitu ambacho kilinishtua.
"Mwanangu Herena siwezi kukuzuia kwenye matamanio ya mwili ni wazi kuna mtu ana mahusiano na wewe. Ninacho ogopa ni Anko wako kujua huenda akapunguza au kukata kabisa huduma zake.
“Hivyo basi sipendi tumuudhi kwa mara nyingine samahani ilizidi hugeuka kero. Pia mwanangu kama kweli huyo mwenzako anakupenda basi usikubali akugeuze gunia la mazoezi. Mlete hapa atambulike kisha muwe mke na mume naogopa mwanangu anaweza kukupa ujauzito na kukukimbia.
“Nitajisikia vibaya siku moja ukija kuishi maisha kama yangu, haya sio maisha ni maisha yasiothaminika katika jamii yetu. Pia mwanangu sipendi siku moja uingie kwenye msafara wa Mamba wakati wewe ni mjusi hata ukenge hujafikia."
"Una maana gani mama?"
"Mwanangu ugonjwa wa ukimwi ni mbaya ukikupata yataka ujasiri la sivyo unaweza kuyakatisha maisha yako kwa kuhofia aibu. Hivyo mwanangu chukua taadhari kabla ya hatari, nife unizike sio ufe uniache."
Mmh! Maneno ya mama yalikuwa mengi pia angejua huyo anayemzungumzia ni Anko sijui angesemaje. Ni kweli nilikuwa nimefanya makosa kutembea na mwanaume ambaye tayari ameisha tembea na mama yangu ambaye alikuwa sawa na baba yangu.
Lakini siku zote makosa ndiyo huzaa kosa, sikuwa na njia nyingine ya kunusuru uhai wa mama uliokuwa ukichungulia kaburi zaidi ya kujirahisi kwa Anko. Nilifanya siri kama tulivyo kubaliana na Anko kwa kuogopa domo la mama pale atakapojua tumeoga bwawa moja.
Hali ya mama ilitengamaa na kujikuta akirudi kilingeni kama kawaida, kwa kweli sikumchunguza ana fanya nini zaidi ya muda mwingi kujishughulisha na mambo yangu. Siku zilivyozidi kwenda ndivyo na mimi nilivyoondoa woga na kutembea na Anko popote alipotaka kwenda.
Safari zake nyingi za nje nilikwenda naye kama mkewe, huwezi kuamini nilinenepa na kupendeza hata mimi nililitambua hilo. Niliweza kuondoka na Anko na kwenda naye mikoani zaidi ya miezi miwili na kutumbua maisha. Kilichonifurahisha ni hali ya mama kuongezeka kuimalika na kuweza kufanya kazi zake kama zamani.
Mama naye baada ya kupata kurudi kwenye hali yake ya kawaida alirudia kazi yake ya ukahaba. Pamoja na kujua athari zake lakini moyo ulinisuta zaidi ya kumuacha afanye atakavyo. Ahadi ya Anko ilianza kukamilika pale aliponipeleka kwenye Site kunionesha ujenzi wa nyumba yangu.
Nilijikuta nikimshukuru Anko kwa kuonesha ananijali sikujutia uamuzi wangu wa kuchangia mwanaume mmoja na mama. Tokea hapo sikusikia ya mnadi swala msikitini au mgonga kengele kanisani. Siri siku zote ya mtu mmoja akizidi wa pili si siri tena.
Hilo sikuhofia kwa kujua hata mama aliipata nafasi kama ile na alijimwaga bila woga. Naikumbuka siku moja ambayo itakuwa vigumu kunitoka akilini na ndio mwanzo wa kuelewa nini nilichokuwa nikikifanya na kunipelekea kuandika walaka huu.
Nini kitaendelea? Endelea kufuatilia.
Post a Comment