HADITHI: Msafara wa Mamba - 03
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DR AMBE’
ILIPOISHIA:
Namshukuru Mungu kipindi kile nilikuwa likizo muda mwingi nilikuwa karibu ya mama. Faraja nyingine niliyoipata ni kutokana na kukuta akiba yangu Anko wa benki ameniongezea. Nilikuwa sina budi kumfuata kazini kwake kumshukuru.
Aliponiona alifurahi sana kwa kwenda kumtembelea, aliniuliza hali ya mama.
"Herena vipi mama yako yupo?"
"Yupo, lakini alikuwa akiumwa"
"Oooh mpe pole, anaendeleaje?"
"Sasa hajambo kidogo."
"Na tabia zake?" Mmmh lilikuwa swali gumu, lakini nilijilazimisha kujibu:
SASA ENDELEA…
"Kidogo ametulia."
"Una uhakika gani?"
"Siku hizi muda wote yupo nyumbani."
"Labda sababu ya ugongwa."
"Hapana sasa amebadilika," nilimtetea mama ili Anko alirudishe moyo kwa mama.
"Unajua nini Herena?"
"Hata Anko?"
"Yaani mama yako amenichanganya sana, nilikuwa nina mipango mizuri sana kwenu, hasa wewe."
Kauli ile iliuumiza moyo wangu na kujikuta nikimlaumu mama kwa tamaa zake za muda mfupi, nilijikuta nikijibu kwa sauti ya unyonge.
"Ndiyo hivyo tena sina jinsi, akili za mtu haziazimwi."
"Lakini Herena kuna kitu nimekuandalia kizuri sana."
"Kipi hicho Anko?" nilijikuta nikiuliza kwa shauku kujua nini ameniandalia.
"Taratibu Herena, utakijua siku si nyingi."
"Sawa Anko nakisubiri kwa hamu kubwa."
Niliagana na Anko wa benki na kunipa pesa za matumizi laki mbili. Yaani sikuamini ukarimu wa Anko, nilitamani kama angekuwa baba yangu mzazi. Nilijikuta nikitembea barabara nzima huku nikilia na kutamani kumjua baba yangu.
Nilifika nyumbani macho yamenivimba kwa kulia njia nzima, hata dereva wa teksi alinishangaa na kutaka kujua kulikoni. Lakini nilimdanganya mama yangu ni mgonjwa na nilikuwa natoka kwa baba.
Nilipoingia ndani mama alishtuka kuniona nikiwa kwenye hali ile, alinikimbia na kunihoji kutaka kujua kulikoni?. Nilijikuta nikijitupa chini na kuendeleza kilio, kilicho mchanganya mama.
"Herena mwanangu umekuwaje?" sikumjibu niliendelea kulia huku nikigaagaa chini.
"Vipi umeibiwa?"
"Heri ningeibiwa."
"Sasa umekubwa na maswahibu gani?"
"Mama baba yangu ni nani?" nilimuuliza bila sauti ya kilio ilikuwa sauti kavu inayohitaji jibu sahihi.
"Herena nini?" mama aliniuliza kama hakunisikia vizuri.
"Mama namtaka baba yangu."
"We mwana yameanza lini?"
"Leo."
"Kwani tatizo nini?"
"Tatizo ni kwamba namtaka baba yangu, kila mmoja ana baba na mama heri baba yangu ningejua amekufa ningejua moja"
"Herena mbona mwanangu unanipa kazi nzito."
"Mama kunieleza baba yangu ni fulani hiyo ni kazi nzito?"
"Mmh! Mwanangu sijui nianzie wapi?"
"Mamaa uanzie wapi kivipi au sio mtoto wako uliniokota?"
"Mwanangu wapi unakoelekea huku?"
"Kuna ugumu gani kunieleza baba yako fulani, kama huwezi ni wazi mimi si mwanao."
"Herena naomba suala la baba yako uliache kama lilivyo."
"Hapana mama kuna umuhimu kumtafuta baba na mama yangu wa kweli."
"Herena mwangu kwa haki ya Mungu mimi ni mama yako mzazi."
Mama alijiapiza miungu yote.
"Kama wewe ni mama yangu baba yangu ni nani?"
Mama kabla ya kujibu aliinama kwa muda, mara nilimuona akidondokwa na machozi. Japo sikupenda kumuona mama yangu hata siku moja akitokwa na machozi kwa ajili yangu. Lakini kwa suala lililokuwa mbele yangu sikuwa na huruma kwa mama zaidi ya kuelezwa ukweli.
Nilimuacha mama alie na akimaliza anieleze ukweli juu ya mzazi wangu wa kiume yupo wapi. Mama alitulia kwa muda huku akiendelea kububujikwa na machozi. Baada ya kulia kwa muda alinyamaza na kuvuta kamasi nyepesi.
Kisha aliniangalia kwa jicho lililokuwa jekundu na kuanza kuvimba, sio siri nilimuonea huruma mama yangu hasa kutokana na hali aliyokuwa nayo. Baada ya kuniangalia aliniita jina langu
"Herena."
"Abee mama."
"Mwanangu kwa nini leo umeniuliza neno hili?"
"Mama hivi kuulizia juu ya baba yangu kuna ubaya? Roho uniuma kila niwaonapo wenzangu na baba zao. Vilevile naamini kama baba yangu angekuwepo aibu hii isingetokea."
"Herena mwanangu kwa ukweli wa moyo wangu baba yako simjui."
Kauli ya mama ilikuwa ya kuchekesha lakini kwangu ni kama kuupasua moyo bila ganzi
"Eti nini?" nilimuuliza nikiwa nimemsimamia mbele kama jini la kutumwa.
"Ni kweli kabisa mwanangu baba yako simjui."
"Mama yangu mbona unanichekesha, baba yangu humjui mimba yangu ilijitunga?"
"Herena mwanangu japo sikutaka ulijue hili ambalo linaweza kuupokonya moyo wako furaha ya kila siku. Ndio maana nilikubali niadhirike mwanangu, lakini nihakikishe unaishi maisha yenye furaha na kutopungukiwa na kitu," mama alimeza mate kisha aliendelea.
"Herena mwanangu maisha niliyoishi mama yako sikupenda hata siku moja mwanangu uyajue, lakini sina jinsi zaidi ya kukueleza ukweli. Herena mimi mama yako nimefikia kufanya kazi hii baada ya kuikimbia elimu na kuyakimbilia maisha.
“Ukweli mama yako nimeacha shule nikiwa darasa la sita, baada ya kudanganywa na mwanaume mmoja aliyenitoroshea mjini. Mwanzo nilijua mama yako nimepata, kutokana na kuishi maisha mazuri tofauti na ya kijijini. Mwanangu kumbe bwana yangu alikuwa ni jambazi.
Siku moja nikiwa ndani nimekaa kwenye tivii, niliona picha ya jambazi lililouawa. Picha iliposogezwa karibu, mwanangu nilichanganyikiwa. Kibaya zaidi pale sikuwa nawajua ndugu zake, sikutaka kujitokeza.
“ Bwana yangu alizikwa na jiji, nami eneo lile sikuweza tena kukaa kwa kuhofia macho ya watu. Vilevile nilijua lazima wana usalama watataka kujua siri zaidi ya mume wangu. Nilihama usiku usiku na kuhamia sehemu ya mbali ambako nilikuwa sijulikani.
“Huku niliyaanza maisha nikiwa peke yangu, japo ilikuwa peke yangu sikuona tatizo lolote kutokana na hawara yangu kuniachia pesa nyingi. Kwa kweli sikupungukiwa na kitu na kujiona nitaishi maisha yoyote niyatakayo .
Niliyaishi maisha ya kuitanua na kwenda kumbi zote za starehe wakati nikiwa na baba yako huyo."
"Ina maana ndiye baba yangu?" nilimuuliza mama
"Hapana kwa vile nilishea naye mwili ni baba yako."
"Nimekuelewa, endelea."
"Basi mwanangu kama ujuavyo mali bila daftali huisha bila habari na bandu bandu humaliza gogo. Pesa ziliisha taratibu bila kujua kuja kushtukia pesa zimekwisha na mimi ndio hivyo sikuwa na mradi hapo ndipo mama yako nilipoingia kwenye kazi ya kutumia mradi wa mwili wangu.
“Aliyenifundisha ni shoga yangu ambaye tulikuwa majirani mwanangu japo kazi ilikuwa ya kunidhalilisha lakini ilikuwa inalipa na kunipunguzia ukali wa maisha. Kutokana na kutembea na wanaume wengi nilijikuta nashika ujauzito na aliyenipa sikumtambua.
“Hiyo ndiyo iliyokuwa mimba yako, kwa kweli mpaka leo baba yako simjui mimba yako niliipata kwenye ukahaba. Mimba yako kidogo initoe roho baada ya kujaribu kuitoa bila mafanikio. Ukweli Mungu hakupenda nikuue bila sababu, baada ya kushindikana nilikubali kuilea na kufanikiwa kujifungua salama.
Kutokana matatizo niliyokumbana nayo niliamua kukitoa kizazi."
Kufika hapo mama aliinama na kububunikwa na machozi kisha alijifuta na kuendelea kunipa simulizi nzito. Roho iliniuma sana kwa kujua mimba yangu imepatikana kwenye biashara ya mwili hivyo kushindwa kumjua baba yangu.
"Basi mwanangu, baada ya kujijua sina kizazi nilihamishia mapenzi yangu yote kwako. Nilihamishia nguvu zangu zote kwako kuhakikisha unapata maisha mazuri elimu bora ili usijeishi maisha niliyoishi mama yako."
Mama alitulia kama anawaza kitu kisha aliendelea kunipa simulizi ambazo kwa upande wangu zilikuwa sawa na kuupasua moyo wangu bila ganzi. Sijui maumivu yake yako vipi ukiyapimia, nilishindwa kulia kutokana na kumuonea huruma mama yangu kwa simulizi yake ambayo hakupenda niijue.
Nini kitaendelea? Endelea kufuatilia.
Post a Comment