HADITHI: Msafara wa Mamba - 02
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DR AMBE’
ILIPOISHIA:
"Mama Mungu akupe mara ngapi, huyu bwana atakusaidia nini?"
"Herena hebu toka mbele yangu umefikia hatua ya kunikosea adabu mbele ya wageni au kwa vile nakupenda sana?"
"Noooo mama nasema hivi naomba mgeni aondoke sitaki kumuona," niligeuka mkali kama pilipili.
"Herenaaaa! Hebu ondoka mbele yangu sitaki kukuona nitakubadilikia sasa hivi," mama alinitisha, pamoja na vitisho vya mama sikuwa tayari kuendelea kuuona uchafu ule. Nilijua yule atakuwa wa mfano. Niligeuka na kuelekea jikoni ili nije nimuonyeshe mama mimi ni nani?
SASA ENDELEA…
Nilikwenda hadi jikoni na kutafuta kisu lakini nilipata kisu kidogo, nilipekua pekua lakini sikufanikiwa kupata kisu kikubwa. Nilipoangalia pembeni nilikutana na sufulia aliyokuwa imejaa maji machafu ya vyombo tulivyolia usiku.
Kwa bahati mbaya siku ile mfanyakazi alikuwa anaumwa na vyombo vilinisubiri mimi. Nilibeba lile sufulia la shombo ya vyakula tulivyokula jana yake usiku. Nilitoka nalo hadi sebuleni na kumkuta mama akiendelea kuongea na mgeni wake bila wasiwasi wowote.
Bila kuwashitua nilikwenda hadi pale na kumwagia mgeni shombo la uvundo wa samaki na mchanganyiko wa vyakula. Alijaribu kuyakwepa lakini alichelewa shati lote lilijaa ukoko, nilifoka kwa sauti:
"Nasema toka la sivyo yatakukuta makubwa," nilisema yale huku nikielekea jikoni kutafuta chochote cha kumpigia na zaidi ningemuitia kelele za wizi.
Nilikwenda hadi jikoni huku nikilia kwa uchungu na kupitia kisu cha mkate na kutoka nacho. Mama aliponiona alipiga kelele akimwambia yule mgeni akimbie. Baada ya mgeni kukimbia nilikitupa kisu chini na kuanza kulia.
Mama alinibembeleza huku akiniomba msamaha:
"Basi mwanangu nimekosa."
"Mama haya ni maisha gani?"
"Basi mwanangu, lakini hawa ndio wanaoendesha maisha yetu ya kila siku."
"Hapana...hapana si kweli, hivi mama mngekuwa na mjomba sijui ba’ mdogo mmoja kama yule wa benki ungekuwa amepungukiwa nini?"
"Ni kweli, lakini yule ni mume wa mtu wakati wowote anaweza kukata mawasiliano tutaishi vipi. Kama unavyojua mama yako sina mume sina kazi lakini mwanangu unaishi maisha mazuri pengine kuliko watoto wengi wenye wazazi wawili."
"Yote unayosema sikatai, lakini ulitakiwa kuwa na mwanaume mmoja ambaye atakuwa kama mumeo. Sio kila mwanaume wako mama kwa mtindo huu kuna kupona kweli?"
"Mwanangu hiyo ni mipango ya Mungu."
"Mipango ya Mungu pamoja na kujilinda."
"Basi nimekusikia mwanangu nitafanya hivyo."
Kuanzia siku ile pale nyumbani mwanaume mmoja aliyeruhusiwa alikuwa Anko wa benki tu.Wote niliowakuta niliwatoa kama siwajui, huku nikiwaeleza baba amerudi. Waliponihoji alikuwa wapi niliwajibu hiyo siyo juu yao.
Lakini toka niliwapiga marufuku wale wanaume, mama naye akawa tena si wa kushinda nyumbani kama zamani. Kila niliporudi nilikuwa simkuti, ilifikia hatua ya kupita hata siku mbili bila kuonana. Kuna kipindi Anko wa benki alipokuja nymbani hakumkuta na simu alipompigia ilikuwa haipatikani.
Kweli mzowea punda farasi kupanda hawezi, ilionyesha mama yangu jinsi gani alivyopenda kuwa na wanaume wengi na kuamua kuwafuata baada ya kuwapiga marufuku kuwaona pale nyumbani zaidi ya Anko wa benki.
Siku moja nilipokwenda kumtembelea Anko wa benki, siku ile sikumkuta kwenye hali yake niliyoizoea. Alionekana kama mgonjwa kitu kilichonifanya nihoji kulikoni.
"Anko vipi unaumwa?"
"Herena mama yako ana matatizo gani?"
"Kwa nini Anko?"
"Yaani nimeisha mfumania na wanaume tofauti zaidi ya watano na kumsamehe, lakini sasa imetosha mimi na yeye tumeisha vunja mkataba," kauli ile iliushtua moyo wangu na kujikuta nikipiga ukelele wa mshtuko.
"Toba! Mbona mkosi huu," nilisema yale huku nikishika mikono kifuani kwa mshtuko.
"Lakini Herena pamoja na kuvunja ukataba na mama yako, bado nitaendelea kukuhudumia kama nilivyo kuahidi. Nimesikia juhudi zako za kumkanya mama yako, hiyo imenipelekea kutositisha huduma zangu kwako. Nitakufanyia kama nilivyokuahidi ila mimi na mama yako inatosha. Herena mimi mtu mkubwa siwezi kuchangia wanuka jasho."
"Ooh! Mungu mkubwa, asante Anko," nilimshukuru nusra nimalambe miguu.
Niliporudi nyumbani nilimkuta mama yupo kwenye hali ya kawaida kama hakuna kitu kilichotokea. Ilionyesha kiasi gani mama yangu jinsi moyo wake ulivyo na sugu, hakubabaika na kitu wala kuonyesha mabadiliko yoyote.
Baada ya shughuli za kutwa nzima na chakula cha usiku, nilikaa na mama na kumuuliza juu ya Anko wa benki.
"Mama vipi Anko wa benki?"
"Kuhusu nini?"
"Eti mmekorofishana?"
"Tatizo nini? Huli...huvai....husomi?"
"Hapana mama."
"Alinikuta na amenicha, kuondoka kwake sipungukiwi na kitu amenikuta nifurahia maisha na nitaendelea kuyafurahia maisha."
Mmh maneno ya mama yalinifanya niwee mpole kwa kuwa hakuonyesha kubabaika na tukio lililotokea japo kwa upande wangu liliutikisa moyo wangu. Nilimuaga mama na kwenda kulala huku nikilaani kiburi cha shetani cha kumpotosha mama yangu.
******
Siku zilikatika na mama aliendelea na tabia zake za kuuza mwili wake bila kuangalia madhara yake siku za usoni. Anko wa benki na yeye aliendelea kuhudumia bila kinyongo huku akinipa pesa za matumizi ambazo kwa upande wa mama zilikuwa zimekata eti kwa sababu ya kuwatimua wanaume zake.
Mama akaanza kuumwa kidogo kidogo, kila tulipokwenda hospitali tulitibu na kupata nafuu. Kuna kipindi hushikika na kulala kitandani na kushindwa kutoka nje. Maradhi yale mama yangu yalimfanya ayumbe kidogo.
Lakini mama alikuwa na pesa kidogo benki ilimsaidia kutupunguzia ukali wa maisha. Pesa nyingi alizitumia kwa waganga wa kienyeji kwa kusema amerogwa. Pesa benki zilipoisha, ilibidi na mimi nizichukue nilizoingiziwa na Anko wa benki.
Kwa kweli pesa zilikuwa nyingi kidogo, ambazo zilitusaidia kupunguza makali ya maisha ikiwa pamoja na kumsaidia kulipia malipo ya waganga pamoja na dawa alizoagizwa kununua. Alipopata unafuu kidogo alitoka kama kawaida yake.
Lakini kila alipokuwa akitoka alirudi asubuhi akiwa hoi na kunisababishia nisiende shule ili kumuhudumia. Kutokana na hali ya mama kumzidia kila akienda kulala nje, nilimshauri ajipumzishe ili kuangalia hali yake. Nilishukuru Mungu mama yangu alinisikiliza na kuamua kutulia nyumbani.
Mabwana walipomfuata niliwafukuza kama wizi, japo mama aliniomba niwaache waingie ndani. Kusikuwa tayari kukubali uchafu ule kutokana na wao kusababisha mama na mjomba wa benki kuachana. Kila nilipomkumbuka mjomba wa benki roho iliniuma sana.
Lakini ningefanya nini kwa vile ni mtoto mdogo kila nitakacho mweleza atakiona cha kitoto. Kwa kweli pamoja ya ugumu wa maisha sikuwa tayari kukubali kuwaona wanaume wa mama ndani kwetu. Mama alinikubalia kwa shingo upande, nami sikulegeza uzi wa kuhakikisha hali ya mama yangu inaimalika.
Namshukuru Mungu kipindi kile nilikuwa likizo muda mwingi nilikuwa karibu ya mama. Faraja nyingine niliyoipata ni kutokana na kukuta akiba yangu Anko wa benki ameniongezea. Nilikuwa sina budi kumfuata kazini kwake kumshukuru.
Aliponiona alifurahi sana kwa kwenda kumtembelea, aliniuliza hali ya mama.
"Herena vipi mama yako yupo?"
"Yupo, lakini alikuwa akiumwa"
"Oooh mpe pole, anaendeleaje?"
"Sasa hajambo kidogo."
"Na tabia zake?" Mmmh lilikuwa swali gumu, lakini nilijilazimisha kujibu.
Nini kitaendelea? Endelea kufuatilia.
Post a Comment