HADITHI: Msafara wa Mamba - 01
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DR AMBE’
Siku zote kwenye msafara wa mamba huwa haukosi kenge na mijusi. Msichana Herena bila kutegemea amejikuta akisafiri kwenye msafara wa mamba yeye akiwa kama kenge. Lakini yote ni kutokana na siri nzito ya mama yake ambayo imekuwa majuto kwake, lazima amlaumu mama yake kwa nini hakumueleza ukweli. Ni ukweli gani huo fuatana na mtunzi kwenye mkasa huu wa kusisimua.
****
Ni kweli toka nizaliwe nilikuwa simjui baba yangu lakini hiyo haikunipunguzia kitu chochote kwenye maisha yangu. Mama yangu alinilea maisha mazuri kwa kunipa chochote kinachokihitaji, ikiwemo elimu ambayo ni bora katika ulimwengu wa leo wa sayansi na tekinorojia.
Nilisomeshwa shule za gharama tokea kindagate mpaka elimu ya sekondari. Mama yangu alikuwa na mapenzi ya kweli kwangu kwa kunilea kama mboni ya jicho lake. Lakini pamoja na kulelewa malezi ya kudekezwa , sikuielewa tabia ya mama yangu kuwa na mabwana tofauti tena wenye pesa.
Kila mwanaume niliyemuona nilitambulishwa kama mjomba, mwanzoni sijui ilikuwa akili ya utoto nilijua kweli wale ni wajomba. Lakini baada ya kukua na kupata akili pamoja na mama kuniona bado mtoto nisiyejua chochote. Nilitambua kuwa wale si wajomba bali wanaume wa mama.
Hapo moyo ulinishtuka na kumuona mama yangu kama anajichimbia kaburi kwa mikono yake.Yaani kila kukicha mama yangu alibadili wanaume kama nguo, ni kweli Mungu alimjalia umbile na sura ya mvuto. Lakini matumizi yake aliyatumia vibaya ya kuudharirisha utu wake.
Pamoja na kutofurahia tabia za mama yangu lakini sikuwa na uwezo wa kumwambia asifanye vile. Kwanza ningeanzia wapi pili ningemuelezaje? Angeniuliza nina uhakika gani na yale niyasemayo ningemjibu nini.
Maisha yaliendelea huku na mimi nikiendelea na masomo yangu, wakati huo nilikuwa kidato cha pili. Kutokana na uwezo wangu wa akili nilifanya vizuri mtihani wa kidato cha pili na kufanikiwa kuingia kidato cha tatu.
Siku nilipopata matokeo nilirudi nyumbani nikiwa na furaha tele moyoni ya kuweza kuingia kidato cha tatu. Nilipofika nyumbani sebuleni nilimkuta mama akiongea na mzee mmoja ambaye kama sikukosea macho yangu alikuwa mkurugenzi ya moja ya benki jijini.
Nilipoingia nilikwenda moja kwa moja hadi kwa mama na kumkumbatia huku nikipiga kelele za furaha
"Yoyooo mama nimepitaaa."
"Usiniambieee!" mama alijibu huku akinikumbatika kwa nguvu.
"Kweli mama, tena pamoja na rafiki yangu Fatuma."
"Oooh hongereni sana."
"Asante mama," nilijibu huku machozi ya furaha yakinitoka.
"Sasa mwanangu nitakutayarishia zawadi yoyote uitakayo."
"Ooh, asante mama nashukuru, mama unakumbuka ulisema utaninunulia simu ya laki tano?"
"Kama nilivyo kwambia ahadi zangu zipo palepale."
"Vipi huyu ni binti yako?" aliuliza yule mgeni.
"Ndio...tena wa pekee."
"Mmh! Basi na mimi naongezea zawadi."
"Anko zawadi gani?" niliuliza kwa shauku.
"Kwanza nitakulipia kidato cha tatu mpaka cha nne, kisha nitakutafutia shule ya hadhi ya juu ambayo utasoma kidato cha tano na sita kisha kitakutafutia chuo nje ya nchi."
"Usiniambie Anko," nilijikuta nimemkumbatia Anko kwa furaha bila kujijua.
"Usiwe na wasi jione mtu mwenye bahati, leo hii nitakufungulia akaunti kwenye benki yangu, sawa binti?"
"Mjomba Mungu akuzidishie."
"Asante."
Kama kawaida yangu nilikwenda chumbani kwangu ambako kulikuwa na kila kitu. Kutokana na tabia za mama hakupenda nitumie sebule zaidi ya kuniwekea vitu muhimu chumbani kwangu. Kama tivii na redio kubwa pamoja na kompyuta.
Siku zote nikimaliza kuongea na mama huenda chumbani kwangu na kukutana naye kipindi cha chakula, mara nyingi mama alipenda tule pamoja. Nilikwenda chumbani kwangu na kuendelea na programu zangu za mazoezi ya kompyuta.
Nikiwa chumbani kwangu mama alinifuata kunieleza kuwa mjomba wa benki anataka kuniaga. Nilikwenda hadi sebuleni na kumkuta mjomba akijiandaa kuondoka, aliponiona alinisogelea na kunishika kichwani huku akichezea nywele zangu fupi:
"Herena kesho njoo ofisini ukitoka shule ili upigwe picha na kukufungulia akaunti yako."
"Sawa Anko, lakini kesho siendi shule mpaka shule itakapofunguliwa kwa ajili ya kujiunga na kudato cha tatu."
"Ooh, vizuri basi kesho njoo na mama yako ili nimpe pesa za malipo ya miaka miwili na wewe ufungue akaunti yako kabisa."
"Asante Anko Mungu akuzidishie," sikuamini yote aliyokuwa akiyasema niliona kama ndoto. Mjomba huyu alikuwa tofauti na wote ambao walikuja pale nyumbani wengi walinipa pesa si suala la maendeleo yangu.
****
Siku ya pili mimi na mama tulikwenda hadi pale kwenye ile benki, tulipokelewa kama waheshimiwa fulani. Mkurugenzi mwenyewe ndiye aliyesimamia kufungua akaunti yangu japo kulikuwa na watu wengi. Baada ya kufungua akanti Anko ambaye nilijua ni mpenzi wa mama yangu alimpa mama pesa ambayo sikujua idadi yake.
Tulipotoka pale benki tulikwenda moja kwa moja hadi shule ambapo mama alilipa karo ya shule ya miaka miwili nikishuhudia kwa macho yangu. Baada ya pale tulirudi nyumbani nikiwa na furaha tele na kuwa na uhakika wa maisha yangu kwa kupata elimu mpaka mwisho wa pumzi yangu.
Malengo yangu yalikuwa ni kusoma kwa bidii ili nifike mbali kielimu na kuweza kupata kazi ambayo ingenifanya nisiwe mwanamke tegemezi. Moyoni nilijiapiza kamwe sitaifanya kazi chafu kama ya mama ya kutouthamini mwili wake na utu wake.
Japo hakuwa na mume lakini alitakiwa atafute bwana mmoja ambaye ndiye atakaye kuwa mume wangu na kujijengea heshima mbele ya jamii. Kwa hali ile niliuapia moyo wangu nitasoma kwa bidii zote na kwa nguvu zangu zote.
Nakumbuka siku moja niliporudi nyuimbani kutoka twesheni, sebuleni nilimkuta mama na mwanaume mwingine. Sio siri kwa mara ya kwanza nilichukizwa na kitendo kile cha kukosa heshima na kushindwa kujiheshimu. Ilikuwa ni wiki tu nimepata ufadhiri wa kusomeshwa mpaka mwisho wa maisha yangu.
Nilijiuliza kama atatokea Anko wa benki na kuikuta hali ile kungekuwa na usalama kweli au hatima yangu itakuwa nini kama sio kukatishwa kwa huduma muhimu ambazo ndizo ufunguo wa maisha yangu. Kuliko kutegemea kitega uchumi cha mwili.
Kwa kweli nilikasikilika sana na kujikuta nikisimama mbele ya mama na yule mgeni kama jini la kutumwa na kuuliza:
"Mama huyu nani?"
"Aaah huyu Anko Mody," alijibu huku akinilazimisha nikubaliane na upuuzi wake.
"Anafanya nini hapa?"
"Herena ni maswali gani, unafikili bila kuwa karibu na watu hawa maisha yetu yatakuwa magumu."
"Mama Mungu akupe mara ngapi, huyu bwana atakusaidia nini?"
"Herena hebu toka mbele yangu umefikia hatua ya kunikosea adabu mbele ya wageni au kwa vile nakupenda sana?"
"Noooo mama nasema hivi naomba mgeni aondoke sitaki kumuona," niligeuka mkali kama pilipili.
"Herenaaaa! Hebu ondoka mbele yangu sitaki kukuona nitakubadilikia sasa hivi," mama alinitisha, pamoja na vitisho vya mama sikuwa tayari kuendelea kuuona uchafu ule. Nilijua yule atakuwa wa mfano. Niligeuka na kuelekea jikoni ili nije nimuonyeshe mama mimi ni nani?
Nini kitaendelea? Endelea kufuatilia.

Post a Comment