Maisha halisi ya Kassim Kayira
Kutoka mkimbizi, babantilie, BBC hadi Azam TV
Aeleza uwezo wa kuzungumza lugha na makabila 30
HELADIUS Banzi, mmoja wa madereva mahiri
ofisini kwetu, naanza kumuona akiishiwa na uvumilivu wa kuendelea
kusubiri. Macho yake yanaashiria kukata tamaa, lakini hataki kuniambia
kwa mdomo, anaruhusu vitendo vinipe ujumbe, hakutaka kuendelea kuwepo
eneo hilo.
Tuko Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu
Julius Nyerere, jijini Dar, lengo ni moja tu. Kumpokea mtu ambaye macho
yangu yalikuwa na hamu kubwa ya kumuona, muda aliouahidi kufika jijini
Dar, sasa ulikuwa umetimia.
Wakati natafakari jinsi ya kumtuliza
Banzi, ghafla naona umati wa watu ukikodolea macho eneo la kutokea
abiria, kila aliyefika mahali hapo kwa lengo la kupokea wageni, anasogea
kwa ukaribu zaidi.
Ghafla namuona mtu aliyenifanya kuwepo
eneo hilo, akivuta begi kubwa, miwani ya jua ikiwa kichwani, haraka sana
namfuata na kujitambulisha tena kwake, huyu si mwingine bali ni
mtangazaji maarufu ulimwenguni, kupitia Idhaa ya Kiswahili ya BBC yenye
makao yake makuu katika jiji la London nchini Uingereza, Kassim Kayira.
“Ooh, ni wewe? Yeah kweli naipata picha
yako sasa,” anasema Kayira wakati tukisalimiana, huku akijaribu
kunikumbuka zaidi kwani tumekuwa tukiwasiliana kupitia mitandao ya
kijamii, sasa tumeonana ana kwa ana.
“Kabisa, ni mimi Brighton, karibu sana
nchini Tanzania, karibu sana Kayira,” namkaribisha, tayari kwa safari ya
kuelekea ofisini kukamilisha kilichotufanya tukutane, mahojiano.
“Aah, kuna watu wengine walitakiwa pia
waje kunipokea hapa, lakini sasa siwaoni, sijui tufanyeje sasa,” anasema
huku akiangaza huku na kule kama anayejaribu kubahatisha kitu.
“Akina nani hao?,” namuuliza huku nikimkazia macho.
“Hawa watu wa Azam TV, kama nilivyokueleza, naanza rasmi kufanya nao kazi, sasa siwaoni unashauri nini?
“Nadhani tuondoke kwanza, eneo hili huku
mawasiliano mengine yaendelee, nashauri tuelekee ofisini kwao, kuanzia
hapo tutajua ratiba kamili ya mahojiano yenu,” haraka sana Banzi
aliyekuwa kimya anaingilia mazungumzo yetu kwa ushauri ambao sote
tunajikuta tukikubaliana nao.
“Lakini mahojiano yaanzie njiani, hatuna muda wa kupoteza, sijachoka na niko tayari kwa kazi,” anasema Kayira.
“Sawa, hakuna shida, basi twendeni,” nasema na kumuonesha ishara ya kutufuata.
“Siwezi kuchoka nimeshazoea sana mambo
ya safari, si unajua unapokuwa mtangazaji wa kimataifa, kusafiri mara
kwa mara inakuwa sehemu ya maisha,” anasema tena Kayira na kugeuka nyuma
ambapo namuona akichukua simu yake ya mkononi na kuanza kupiga picha
mazingira ya uwanja wa ndege, hapohapo anamkabidhi Banzi simu na
kumuomba atupige kwa pamoja, anafanya hivyo.
Kufika hapo, mimi na Kayira tunaamua
kukaa viti vya nyuma kwa lengo la kuanza mahojiano wakati tukielekea
yaliko makao makuu ya Azam Tv, Tabata Relini, Ilala.
“Unawezaje kuzungumza lugha ya Kiswahili
kwa ufasaha namna hii?,” naanza kumuuliza huku nikifunua kitabu changu
cha kumbukumbu (diary) tayari kwa kudondosha wino, huku nikiweka kifaa
cha kurekodia sauti mahali ambapo kila kitu kitaratibiwa.
“Ni kujifunza tu, napenda sana lugha, si
Kiswahili tu, nazumgumza zaidi ya makabila na lugha 30 duniani, si
mchezo eti,” anajibu Kayira kwa lafudhi ya Kiganda huku akimalizia
kufunga mkanda wa gari kwenye siti yake.
“Zingine ni zipi?,” namuuliza kwa shauku kubwa.
“Ooh, nazungumza Kiingereza, Kifaransa,
Kiarabu, Kireno, Kiitaliano, Kichina, Kikorea, Kihispaniola, Kijapani,
na Kiswahili kwa upande wa lugha. Kwa makabila najua Kirundi, Kihaya,
Kinyankore, Kihutu, Kitusi, Kinyoro, Kinende na Kirinashi na sasa
naendelea kujifunza lugha na makabila mengine zaidi,” anasema Kayira
huku akiachia tabasamu na kumfanya dereva, Banzi ageuke kumtazama huku
akiachia kicheko kinachoashiria kunogewa na mazungumzo yetu.
KUZALIWA KWAKE:
“Wewe ni raia wa wapi na umezaliwa lini?,” namuuliza.
“Mimi ni Mganda kwa upande wa baba na
Mnyarwanda kwa upande wa mama, nilizaliwa Januari 27, 1974 huko Mbarara
nchini Uganda, baba yangu anaitwa Sheikh Ibrahim Kayira na mama yangu
anaitwa Hajat Amina ,” anasema Kayira na hapohapo simu yake inaita
mfululizo.
“Ooh, samahani kidogo,” anasema kabla ya kupokea.
“Hakuna shida kaka,” namjibu kwa sauti ya upole kabisa huku nikimtazama usoni.
Baada ya kumalizana na simu yake, mazungumzo yanaendelea.
Je, nini kitafuata? Usikose kufuatilia wiki ijayo.

Post a Comment