ad

ad

HADITHI: RAHA YENYE MAUMIVU -14 (Mwishooooooooooooooo)

 
HADITHI:  RAHA YENYE MAUMIVU
SEHEMU:14
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500.
... Siku ya pili mama Gift alitoka hospitali akiwa mzima wa afya njema, muda wote Gift aliutumia kuwa karibu ya mama yake kuhakikisha achukui uamuzi mbaya ambao hapendi kuuona tena.
Baada ya wiki mama Gift aliongozana na mwanaye Gift hadi kwa baba yake Tabata Kisukuru. Walimkuta baba yake akiwa anatengeneza gari lake lililokuwa limeharibika alipowaona aliwakaribisha, lakini moyoni akijiuliza mtalaka wake umekosea njia mpaka kufika pale kwake. Baada ya kutengana hapakuwa na mawasiliano zaidi ya miaka saba.
"Karibuni."
"Asante." Walijibu kwa pamoja.
"Shikamoo baba."
"Marahaba mumeo hajambo?"
"Hajambo anakusalimia."
"Shikamoo baba Gift," mama Gift alimuakia mumewe wa zamani.
"Marahaba mama Gift karibu."
"Asante."
Aliwaacha wageni watangulie ndani na yeye kutoa maelekezo ya mwisho kwa mafundi, kisha na yeye aliwafuata ndani huku ajifuta mikono kwa tambala kutoa gilisi iliyokuwa mikononi baada ya kulizika na usafi wa mikono yake alilitupa lile tambala na kuingia ndani.
Aliwakuta wakiwa sebuleni wamekaa kwenye makochi alipofika alikaa mbali nao na kuwa wakitazamana.
"Haya wageni karibuni."
"Asante."
"Baba huu mguu ni wako."
"Mwanangu mguu ungekuwa wangu usingekuwa nao?" baba yake kama kawaida alimtania mwanaye.
"Baba Gift hujaacha masihara yako,"mama Gift alisema huku kila mmoja akicheka.
"Haya mama hebu nipe huo mguu wangu?"
"Baba kwanza napenda kukuomba samahani kujibebesha madaraka mazito ambayo hayalingani na uwezo wangu wala umri wangu. Lakini ina imani busara si umri wa mtu bali maneno hutamkayo."
"Sawa kabisa mwanangu," baba Gift alikubali.
"Baba mimi ni mtoto wa watu wawili yaani wewe baba na mama, bila mmoja wenu mimi nisinge kuwepo sijui nipo sawa?"
"Sawa kabisa mwanangu," baba Gift alijibu.
"Basi siku zote tangu baba na mama mtengane nimekuwa kiumbe kilichopungukia kitu fulani maishani mwangu ambacho hakionekani kwa macho, kitu ambacho kimenighalimu siku zote.
“Kila kukicha nilimuomba Mungu ili aweze kusikiliza dua zangu ili siku moja wazazi wangu mrudiane na muishi kama zamani na kutenganishwa na kifo, kama ndoa yenu ilivyofungwa mbinguni itakayotenganishwa na kifo.
“Siku zote shetani hutumia udhaifu uliopo kwenye maisha ya wanadamu kuhakikisha anaharibu kila kitu. Nina imani aliweza kufanikiwa azima yake lakini uwezo wake haushindani na nguvu za Mungu.
“Leo hii kwa uwezo wa Mungu naomba wazazi wangu muijenge upya ndoa iliyojengwa na Mungu, Baba."
"Naam mwanangu."
"Naomba uziheshimu juhudi zangu nilizozifanya usiku na mchana, uyaheshimu mapenzi yangu kwako, unilindie heshima yangu kwako na kuhakikisha baada ya kunipa idhini ya kuolewa naomba unipatie kilicho baki.
“Si kingine ni furaha ya milele ili niliapo basi nibembelezwe na wazazi wangu wote wawili nakuomba nipo chini ya miguu yako nakuomba kwa uwezo wa Mungu umsamehe mama kwa yote aliyotenda. Siku zote Mungu humpenda yule awae tayari kusamehe, aliyekosea hata bwana wetu Yesu Kristo alitufundisha tusamehe saba mara sabini. Najua baba dini umeishika sina shaka na hilo, naomba umrudie mama." Gitf aliyazungumza yale huku akilia.
Yalikuwa maneno mazito yaliyomtoa machozi kila mmoja aliyekuwepo pale. Lilikuwa pigo mujarabu kwenye moyo wa wa Mzee Bilikila ambalo lilifanya akose la kusema, kwenye ubinadamu mwanaye kamaliza kwenye dini kamaliza hata kwenye malezi.
Akiwa ametulia huku machozi yakimtoka mzee Bilikila aliwaza mengi huku akiamini siku zote busara si umri bali maneno ya mtu. Hakuamini maishani mwake kama wanaye tena wa kike ataweka kuongea maneno mazito kama yale.
Akiwa bado ameinama machozi yakimtoka mama Gift alitoka kwenye kochi na kutembea kwa magoti kwenda kumuomba msamaha mumewe.
"Baba Gift naomba unisamehe mume wangu maneno aliyoongea mtoto ni mazito, najua nimefanya kosa tena kubwa nahitaji msamaha, siku zote ng'ombe akivunjika mguu hurudi zizini," mama Gift aligaagaa chini huku akilia.
Mzee Bilikila hakujibu kitu machozi yaliendelea kumtoka kama maji na kamasi nyembamba nazo ziliendelea kumwagika. Gift aliongezeka kumuangukia baba yake.
"Baba wewe ndiye nguzo ya familia, siku zote haiyumbi, baba wewe sawa na chini kila kirukacho hutua chini mpokee mama."
Mzee Bilikila aliwanyanyua wote na kuwakumbatia kuonyesha amekubali kumsamehe mkewe. Walikubaliana kumaliza tofauti zao na mama Gift alirudi rasmi kwa mumewe huku wakiendelea kuichicha siri ya mtoto Malon.
Naye Tell me aliendelea kumpenda mkewe na kumheshimu mama mkwe kama mkwewe. Wakiwa wamekaa siku moja Gift na mama yake wakiongea mama yake alimshukuru mwanaye kwa kazi nzito aliyoifanya kurudisha upendo kwenye familia naye Gift alimweleza mama yake kuwa siku zote mwanadamu unapofanya kosa usikimbilie kujihukumu bali kilio chako mkimbizie mwenyezi Mungu kwani ndiye mwenye uwezo wa kusamehe peke yake.
Mwisho tuziheshimu ndoa zetu tuvumiliane wakati wote wa shida na raha wakati wa furaha na majonzi na wakati wa uzima na ugonjwa. Mungu azipe nguvu ndoa zote. Na siku zote kutenda kosa ni kosa ila kurudia kosa ni kudhamilia.
Mwishooooooooooo Kabisaaaaaaaaaaa
Powered by Blogger.