HADITHI: RAHA YENYE MAUMIVU - 12
SEHEMU:12MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
...ILIPOISHIA:
Aliirudia ile barua zaidi ya mara mbili huku machozi yakimmiminika kama maji. Alijifuta machozi kisha alitoka mpaka kwenye ofisi ya wauguzi na kuwakabidhi ile bahasha aliyokuwa ameiandika jina la mwanae Gift.
"Samahanini naomba akija mwanangu kama nitakuwa nimepitiwa na usingizi mumpe. Ila sipendi nionane naye kwa leo, akija mwambie tuonane kesho."
"Sawa mama," wauguzi aliipokea ile barua na kuendelea na shughuli zao hawakumtilia maanani.
SASA ENDELEA…
Mama Gift baada kuwapa ile barua alirudi hadi chumbani kwake na kuichukua shuka ambayo aliitengeneza kama kitanzi na kuifunga juu kwenye pangaboi. Baada ya kuifunga vizuri ile shuka alijifunga shingoni na kujifyatua kwenye kitanda.
Mmoja wa wauguzi pamoja alikuwa bize aligundua kitu fulani usoni kwa mama Gift, uso wake ulikuwa umevimba uikionyesha alikuwa akilia kitu kilichomfanya ashtuke. Baada ya kuondoka mama Gift aliwauliza wenzake.
"Jamani mmemuona yule mama?"
"Hata kwani ana nini?"
"Yaani mnajifanya mpo bize kama sio kwa ajili ya wagonjwa, ubize huo mgeupata wapi?"
"Mbona maneno mengi kwani yule mama ana nini?"
"Mnajua mimi nawashangaa sana, mgonjwa anakuja hata hamumuangalii usoni ninyi mnaendelea na porojo, bila kujua yupo vipi halafu kitu kingine kilichonishtua ni sauti yake inaonyesha ana tatizo."
"Sasa sisi tumfanyaje?" Mmoja alijibu huku akipaka rangi kwenye kucha.
"Haya ngoja yatokee, hizi porojo mtazipigia nyumbani, jamani kazi mbaya ukiwanayo."
"Zinduna kwani umegundua nini?"
"Wakati yule mama akija hapa mimi nilikuwa najaza ripoti ya dawa, lakini sauti yake ilinifanya ninyanyue macho, kuna kitu nimekiona usoni kwake si cha kawaida huenda yule mama amezidiwa hali yake si nzuri ni jambo ambalo linatakiwa tulijue sisi kama wauguzi, hivi aje daktari tutamwambia nini, tushukuru Mungu hapajatokea tatizo, lakini tabia yetu ya kuingia mpaka tunatoka hatuendi kumuangalia mgojwa sio nzuri."
"Ni kweli Zinduna, sasa unatushauri nini?"
"Kwa vile mimi najaza ripoti mmoja wetu akamjulie hali ya yule mama."
Mmoja wa wauguzi alinyanyuka na kuelekea chumba alicholazwa mama Gift. Alikwenda kwa kujivuta huku kama mtu aliyelazimishwa, mlango ulikuwa umerudishwa kwa kuegeshwa, alifika moja kwa moja na kuusukuma mlango.
Tukio aliloliona mbele yake lilimfanya apige kelele za woga pale alipomuona mama Gift akipapalika kwenye kitanzi cha shuka. Wauguzi wengine walikuja mbio na kumkuta mama Gift ameninginia juu.
Kwa ujasiri mkubwa walifanikiwa kuikata ile shuka na mama Gift kuanguka chini akiwa amelegea. Alikuwa amepoteza fahamu lakini mapigo ya moyo yalikuwa mbali sana ambayo yalifanya maisha yake yawe kwenye hatihati.
Walimkimbilia daktari ambaye alifanya kazi ya ziada lakini kila dakika mapigo ya moyo yalikuwa yakipungua kupiga. Ilibidi awekewe mashine ya kumsaidia kupumua hali yake ilikuwa mbaya sana.
Daktari Eliud alichanganyikiwa na kujiuliza yule mama alikuwa na siri gani? Kwanza alikataa familia yake isimuone, pili ameamua kujitoa uhai kuna siri gani? Mama Gift alikuwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi akipumua kwa kutumia mashine.
*******
Gift akiwa na mumewe waliwasiri hospitali ya TMJ na kuelekea moja kwa moja kwenye chumba alicholazwa mama yake. Wakati anapita maeneo ya ofisi ya wauguzi dada mmoja ambaye si mgeni na Gift alimkimbilia.
"Da’ Gift kuna mzigo wako."
"Nani kakupa."
"Mama yako aliuleta ofisi ili tukupe ukija."
"Ina maana ameisha toka?"
"Ha.ha..apa.na," alijibu kwa kubabaika.
"Hata hivyo wewe si mjibuji kwa vile yupo mwenyewe atajibu."
Baada ya kuipokea ile barua aligeuka ili aondoke
"Samahani da Gift kabla ya kwenda chumba cha mgonjwa daktari alisema mpitie kwake kwanza."
"Kuna nini? Mbona mambo ya hapa yananichanganya."
"Yanakuchanganya nini, we twende kwa daktari hatujui anataka kutuambia nini tukitoka tunakwenda kumuona mama," Tell me alimwambia mkewe.
Waliongozana wote hadi kwenye ofisi ya daktari. Walimkuta akiwa amesimama akifuta jasho na kufungua friji ndogo kutoa maji baridi. Alipowaona waliwakaribisha.
"Oooh Mr and Mrs Tell me karibuni sana."
"Asante," walijibu kwa pamoja wakiwa wamesimama.
"Chukueni viti," walikaa kwa pamoja.
Daktari walikunywa yale maji kwa mkupuo alishupa pumzi nzito kisha alikaa kwenye kiti chake. Kabla ya kuongea alichukua cheti kilichokuwa juu ya meza yake kama anakisoma, kumbe alikuwea akitafuta neno la kuongea ili aeleweke.
Baada ya kupata la kuanzia alikohoa kidogo japo hakuwa na kikohozi na kusema:
"Samahanini jamani."
"Bila samahani."
"Sasa jamani nimewaiteni ili..." walikatishwa na sauti ya muuguzi ambaye aliingia huku akipiga kelele.
"Dokta mashine imezimika."
"Oooh Mungu wangu! Samahanini nakuja mara moja," Dokta alipitia koti lake na kutoka kwa mwendo wa kasi, kitu kilichofanya Gift na mumewe watazamane na Tell me kunyanyua mabega juu.
Wakiwa wamebakia peke yao kwenye ofisi ya daktari zaidi ya masaa robo saa Gift alimwambia mumewe.
"Mpenzi kwa nini tusiende kwanza kumuona mgojwa ili akirudi akute na sisi tumeisha mjulia hali mgojwa?"
"We subiri hujui kwa nini ametuita huku kabla ka kuonana na mgonjwa, najua madaktari pengine wanataka kukuuliza chanzo cha tatizo."
"Mbona jana tulimwambia."
"Huenda alikuwa amechanganyikiwa kwa ajili ya kuokoa maisha ya mgonjwa, pengine alikusikia lakini hakukuelewa."
"Haya wacha tumsuburi"
Wakiwa wametulia kumsubiri daktari, Gift aliamua kuisoma barua aliyopewa na muuguzi ajue imeandikwa nini? Aliifungua ile barua na kuanza kuisoma wakati huo mdogo wake Malon alikuwa amepakatwa na Tell me .
Aliisoma ile barua taratibu kila alivyokuwa akisoma ndivyo mapigo ya moyo yalivyokuwa yakipanda na joto kuongezeka mwilini. Aliisoma hadi mwisho alijikuta akisema.
"Hapana..Hapana...Ooooh maskini mama yanguuuu," Gift aliteleza toka juu ya kiti akiwa amelegea na kupoteza fahamu. Lilikuwa tukio la pili lililofanana la watu wawili, moja la mama Gift na la sasa ni la Gift mwenyewe.
Tell me alijikuta akichanganyikiwa na kushindwa kuelewa kwa nini mkewe yupo kwenye hali ile. Alimuwahi kabla hajaanguka chini toka juu ya kiti na kumlaza. Wakati huo Malon na yeye alianza kulia kitu kilichozidi kumchanganya Tell me.
Alishindwa aanzie wapi kumuhudumia mkewe na Malon shemeji yake ambaye ni mwanaye na yeye alikuwa akilia. Bahati nzuri daktari aliingia na kukuta tukio lingine kitu kilichomshangaza.
"Tell me vipi tena shemeji?"
"Ndugu yangu yaani hata sijui alikuwa akisoma hii barua akiwa kimya mara alianza kupayuka hapana..hapana kisha alisema maskini mama yangu na kupoteza fahamu."
"Mmh shughuli ipo, wewe mwanaume jikaze mambo ni mazito."
"Kwa nini daktari?"
"Kila tukio ni zito."
"Una maana gani?"
"Ngoja kwanza tumuhudumie shemeji."
Gift alipewa huduma ya kwanza na kurudiwa na fahamu, alipopata fahamu aliangua kilio cha sauti ya juu.
"Oooh maskini mama yangu...kwa nini umechukua uamuzi huo, japo kila baya malipo yake ni mabaya…mama hukutakiwa kujihukumu."
Nini kitaendelea? Kuyajua yote endelea kufuatilia.
Post a Comment