Tatizo la umeme nchini lawa kizungumkuti
By Bakari Kiango
Tanga. Uwezo wa
kuzalisha umeme kwenye vituo vya Nyumba ya Mungu, Hale na New Pangani Falls
nchini umeshuka kutoka asilimia 100 hadi kufikia 15 kutokana na sababu
mbalimbali ikiwamo ya baadhi ya wananchi kuchepusha mkondo wa maji wa Mto
Pangani ambao ni tegemeo kubwa kwa uzalishaji wa vituo hivyo.Hayo yalisemwa jana na Mhandisi, John Skauki katika eneo la Mto Pangani kunakodaiwa mkondo wake wa maji kuchepushwa katika Kijiji cha Buiko, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.
Mhandisi Skauki alisema hali hiyo imesababisha umeme kuzalishwa chini ya kiwango tofauti na matarajio ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Alisema kituo cha Nyumba ya Mungu huzalisha umeme mita za ujazo 10 kwa sekunde chini ya kiwango cha ujazo wa mita 25 za kawaida. Kiwango kinachohitajika ni mita za ujazo 45.
“Suala hili la kuchepusha mkondo wa maji linashughulikiwa na mamlaka husika,” alisema Skauki.
Alisema kwa kawaida, maji hayo husafiri kwa ujazo wa mita 42 kwa sekunde kuelekea Bwawa la Nyumba ya Mungu linalotiririsha maji vituo vya New Pangani Falls na Hale kwa ajili ya kuzalisha umeme.
“Kwa sasa Bwawa la Nyumba ya Mungu linazalisha megawati tano badala ya saba, New Pangani 17 badala ya 68 za kawaida na Hale megawati nne kati ya 10 zinazotakiwa ,” alisema Mhandisi Skauki.
Mtaalamu wa Bonde la Maji la Mto Pangani, Vendelin Basso alisema ofisi yake imeendelea kulishughulikia tatizo hilo.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Buiko, Idd Seng’onyi alisema kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, wakazi wa eneo hilo wanapata hasara ya mazao yao kutokana na maji ya mto huo kutuama sehemu moja badala ya kutembea.

Post a Comment