ad

ad

Singidani (A Story From My Heart) - 12



 

ILIPOISHIA...
"...lakini inanipasa nikubali kuwa nimeshatekwa na ninampenda. Nitahakikisha nampata Chris, lazima, " aliwaza Laura.
SASA ENDELEA...
SAA 10:00 alasiri, Basi la Beffe lilifunga breki katika kituo cha Mkalama - Shuleni. Dk. Chris alishuka na mizigo yake. Akakodisha baiskeli iliyomfikisha nyumbani kwao.
Alipokelewa kwa shangwe na bibi yake aliyekuwa akisuka jamvi kwa kutumia  ukindu kiambazani mwa nyumba yao mpya. Walikuwa na eneo kubwa lililozungushwa kwa uzio wa michongoma. Maboma mawili makubwa ya mifugo yalikuwa pembeni mwa nyumba zao.
Walifuga ng’ombe, mbuzi na kondoo. Nyumba yao mpya iliyojengwa kwa matofali ya kuchoma na kuezekwa kwa bati haikuwafanya wabomoe nyumba yao ya asili ambayo ilijengwa kwa fito na udongo na kuezekwa kwa tembe.
“Aaaah! Mume wangu huyoo...” bibi alitamka kwa sauti kuu, akijaribu kumkimbilia mjukuu wake.
Alikuwa ajuza hasa, akiwa na umri wa miaka themanini na tatu, alimudu kufanya shughuli zake ndogondogo za kila siku. Aliishi na wanaye wawili; Shamakala ambaye alikuwa na mke na watoto wawili na Maria aliyekuwa na mtoto mmoja.
Ilikuwa famili yenye upendo mkubwa. Dk. Chris aliongeza mwendo na walipokutana na bibi yake alimpokea na kumlaza kifuani mwake.
“Ooh! Daktari wangu huyo... karibu sana baba,” bibi alisema, akishindwa kuficha furaha yake.
“Ahsante bibi, shikamoo.”
“Marhaba mume wangu, habari za nyumbani?”
“Nzuri kabisa.”
Pamoja na kuzaliwa na kukulia kijijini Mkalama, bibi huyo alimudu vizuri sana kuzungumza Kiswahili japo kuna wakati huchanganya na lugha yao ya Kinyiramba.
Mara moja bibi aliingia ndani, akatoka na kipeyu kilichojaa togwa kisha akamkabidhi Dk. Chris apooze koo na kinywaji hicho cha asili. Salamu zikaendelea.
***
Sura ya mwanamke mrembo ilimchanganya Dk. Chris, alimwangalia umbo lake. Akatazama hipsi zilizochomoza vyema pembeni ya mapaja yake, akazidi kutibuka! Matiti madogo yaliyosimama yenyewe kifuani kama embe bolibo, ilikuwa kishawishi kingine kwa Chris.
Nyongo ya huba ikapasuka. Alikiri kweli mwanamke yule alikuwa mrembo. Chris aliumia moyoni alipogundua kuwa, hawezi kumpata mwanamke yule tena. Ni Laura alikuwa akimjia mawazoni kwa kasi sana.
Akiwa amekaa chini ya mti, Chris alidongosha machozi kwa kumbukumbu za mwanamke huyo. Alitamani sana kubadilisha ukweli, awe hajaolewa lakini haikuwezekana.
“Vipi wewe?” Shamakala, baba yake mdogo alitamka akimgusa begani.
Chris alishtuka na kugeuza shingo  kumwangalia aliyemgusa. Hapo akakutana na sura ya baba yake mdogo. Shamakala akashangazwa na machozi ya Chris.
“Vipi, mbona unalia?” Shakamala akamwuliza.
Shamakala na Chris walipishana kidogo sana kiumri. Alikuwa kitindamimba katika uzao wa babu na bibi yake. Sababu hiyo iliwafanya wawe marafiki na kuelezana siri zao zote. Chris hakuona sababu ya kumficha. Alimweleza kila kitu kuhusu kisa cha Laura.
“Tulia Chris, imekuwa vizuri umegundua mapema.”
“Lakini kuna tatizo lingine kubwa zaidi.”
“Lipi?”
“Mke. Baba amesema natakiwa kurudi Dar na jibu linaloeleweka. Ameniagiza nije huku kutafuta mke, amesisitiza kwamba lazima nioe huku kwa sababu mke bora anapatikana huku kijijini.”
“Uamuzi wako ni nini juu ya hili?” akauliza Shamakala.
“Sitaki kuongozwa katika suala hili. Natakiwa kutafuta na kuamua mwenyewe nimuoe nani na wapi. Hata hivyo nilipokutana na huyo Laura, nikaona ndiye mke wangu, imekuwa tofauti.
“Si neno sana, maana siwezi kubadili ukweli ila baba sitaki kuoa huku kwa sasa, lazima nitulie kwa muda, nirudi mjini nitafute mwanamke mwingine,” akasema Chris.
“Wazo zuri, lakini mzee atakuelewa? Maana Joseph namjua vizuri sana misimamo yake.”
“Hapo ndipo ninapohitaji msaada wako baba mdogo. Itabidi tufanye mchezo. Mimi nitamwambia baba nimeshapata mke, wewe ndiye uliyenitafutia. Muda huo nitautumia kuanza kutafuta mwanamke mwingine. Unaonaje?”
“Sawa kabisa, nipo upande wako. Kaka naye pamoja na kusoma kote huko bado ana mawazo ya kizamani sana. Nitakusaidia, nipo kwa ajili yako!”
“Ahsante sana baba mdogo.”
Kilichompeleka kijijini ni kama alikuwa ameshakamilisha. Kilichokuwa mbele yake kwa wakati huo ilikuwa ni kupanga safari ya kurudi Dar. Alitakiwa kurudi haraka kwa sababu  alikuwa ameshasaini mikataba  miwili ya filamu na alitakiwa  kurekodi.
“Inabidi nirudi Dar keshokutwa.”
“sawa ila unaniachaje?”
“Usijali.”
***
“Jambo moja muhimu ninalohitaji kujua kutoka kwako ni kama umefanikiwa nilichokuagiza kijijini au lah!” mzee Joseph Shila alimwambia mwanaye Chris, alipomkuta nyumbani usiku huo baada ya kurudi kutoka kazini.
“Nimefanikiwa baba,” akajibu Chris, akitengeneza tabasamu la uongo usoni mwake.
“Vizuri sana. Moyo wangu sasa una amani. Bila shaka sasa tunatakiwa kufikiria kuhusu mipango ya ndoa tu!” mzee Shila akauliza tena.
Chris hakujibu!
Powered by Blogger.