ad

ad

Asiyejiweza kiuchumi hafai kuwa mchumba, soma hapa?



JUMAMOSI nyingine mpenzi msomaji wangu tunakutana katika safu hii na kuweza kupeana elimu ya uhusiano. Kwa tuliokuwa pamoja wiki iliyopita tuliweza kujifunza kuhusiana na ishara mbalimbali ambazo mwanaume akikuonesha moja kwa moja uweze kung’amua kuwa hakutaki.
Wengi walipongeza kuonesha kwamba wamejifunza na kuamua moja. Wamekataa kuendelea kuteseka kila siku. Mapenzi ni hisia, mapenzi ni furaha na yanahitaji amani. Mmoja wenu anapokosa amani, upendo unapotea, maana ya mapenzi pia inatoweka.
Happy-CouplesUpendo unapokuwa umetoweka, unapaswa kuchagua mambo mawili; kuurudisha au kuamua kubwaga manyanga ili uwe huru. Ni kosa kubwa watu wengi wanalifanya kwa kuendelea kumpenda mtu ambaye hakupendi. Amekuonesha kila aina ya vitendo kuashiria hakutaki lakini wapi, huelewi.
Wewe unabaki unateseka tu, eti unampenda, haupo tayari kumpoteza. Ya nini kuendelea kuteseka kwa mtu ambaye hateseki kwa ajili yako? Hana habari na wewe. Ameshasahau kama aliwahi kukutana na mtu kama wewe maishani. ‘Anainjoi’ maisha kivingine na mtu mwingine, wewe unateseka tu, ni ujinga wa kujitakia!
Nikirejea kwenye mada yangu ya leo, kizazi cha sasa kimetawaliwa na mapenzi ya kuigiza. Mtu hampendi mtu anapenda kile alichonacho mtu. Yupo kimasilahi zaidi. Kwamba anaamini akiwa na mtu fulani maisha yatanyooka na yeye kuitafuna raha ya dunia.
Watu hao hawana muda wa kujua mapenzi ya kweli. Ndiyo maana siku hizi matatizo ya ndoa yanakuwa mengi. Migogoro ya ndoa kila kukicha, watu wanaachana. Watu wanauana kwa sababu tu ya kuendekeza fedha kuliko utu au penzi la kweli.
Maana halisi ya ndoa inapotea katika jamii. Tatizo hili lipo kwa wanaume na wanawake. Siku hizi mwanaume anamfuata mwanamke kwa kigezo cha fedha zake, mwanamke pia anamkubali mwanaume mwenye fedha tu.
Tatizo hili zaidi linaonekana kuwa kubwa kwa wanawake. Limekwenda mbali zaidi hadi kwa wazazi. Wanawafundisha wawakubali wanaume ambao wana fedha. Hawataki waolewe na wanaume ambao hawajiwezi kiuchumi.
Binti akimuambia mzazi wake amepata mchumba, kitu cha kwanza mzazi anamuuliza ana biashara gani? Ana fedha? Amejenga au amepanga? Akiambiwa ni hohehahe, haraka sana anamzuia binti yake. Anamshauri asubiri ampate yule mwenye fedha zake, anayejiweza kiuchumi na si vinginevyo.
Hapo ndipo linapokuwa tatizo. Ni vyema wazazi wakawafundisha watoto wao kwamba upendo wa kweli si fedha au utajiri. Watoto nao waishi wakijua maisha yana changamoto zake. Mapenzi ya kweli si fedha. Ni vyema tukajifunza kutoka pia kwa wazazi wetu.
Ambao waliishi miaka mingi ndani ya ndoa. Suala la kuolewa na mtu kwa kuangalia ana fedha kiasi gani linasababisha binti kukosa chaguo sahihi la kumpata mwenza sahihi. Binti anakosa muda wa kumchunguza mchumba wake kwa kupumbazwa na kipaumbele cha utajiri.
Anajikuta ameolewa na mtu mwenye tabia mbaya, asiyekuwa na hofu ya Mungu na matokeo yake ni kuishi ndani ya ndoa miaka miwili mitatu, ndoa inasambaratika. Kumbe pengine angefuata misingi mizuri, akaweka utajiri wa mwanaume pembeni, angeweza kubaini kama kweli mwanaume huyo anafaa au hafai kuwa mume.
Angeweza kupata muda mzuri wa kumchunguza mwanaume, kujua historia yake. Kufahamu ndugu zake, kujua marafiki zake kabla ya kufikia uamuzi wa kufunga ndoa. Kwa imani yake, alipaswa kumshirikisha Mungu kwamba amsaidie ampe mume mwema.
Sasa hivi mume mwema amegeuka kuwa yule mwenye fedha. Ukiwa huna fedha huwezi kuwa mwema. Hili ni tatizo. Pasipo kujisahihisha, pasipo kumchunguza mwenzako vizuri katika hatua za mwanzo kama nilivyoelekeza hapo juu, hakika utaambulia maumivu katika ndoa na si furaha, amani wala upendo.
Ni bora ukakosa utajiri lakini ukampata mwenza ambaye mtaelewana, mtaheshimiana na kupendana katika kila hali. kuliko kuwa na mwanaume tajiri halafu ukaambulia mateso maisha yako yote ya ndoa. Ndoa si uwanja wa vita.
Ndoa ni mpango wa Mungu, ameuweka ili mwanaume apate msaidizi, mwanamke. Wasaidiane, waishia kwa matakwa yake, wapate familia bora, waifundishe mafundisho ya Mungu ili na wao waje kuwa wazazi bora kwa watoto wao.
Kwa leo inatosha, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri!
Powered by Blogger.