Utafiti wazua taharuki, waibua maswali tata

Kura za maoni: Twaweza yaipa CCM ushindi wa 65%, Ukawa 25%
Msemaji wa kamati ya kampeni ya CCM, January Makamba.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
katika tukio lililorushwa moja kwa moja (live) na vituo vya
televisheni, Mkurugenzi Mkuu wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema utafiti
huo uliobebwa na anuani isemayo 'Sauti za Wananchi', umefuata taratibu
zote za kiutafiti na kuhusisha watu 1,848 kutoka mikoa yote ya Tanzania
Bara.
Alisema mbali na Magufuli kushinda kwa asilimia 65 ikiwa uchaguzi
mkuu utafanyika leo, vile vile chama chake (CCM) ndicho kinachopendwa
zaidi na wananchi kwa kiwango cha asilimia 66, kikifuatiwa na Chadema
asilimia 22, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
asilimia 3 na Chama cha Wananchi (CUF) asilimia moja. Ukawa unaomuunga
mkono Lowassa kwa nafasi ya urais, ni muunganiko wa vyama vya Chadema,
NLD, CUF na NCCR-Mageuzi.
Eyakuze alisema kati ya wahojiwa 10 katika utafiti huo, wahojiwa
sita walisema wanatarajia kumchagua mgombea wa CCM ifikapo siku ya
uchaguzi.
Hata hivyo, Eyakuze alitahadharisha kuwa utafiti huo hautabiri
matokeo ya uhakika ya uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka huu, bali ripoti hiyo
imelenga kutoa majibu ya baadhi ya masuala kuhusu uchaguzi na pia ni
fursa adimu kwa wananchi kusikika na kuwapatia taswira viongozi juu ya
wapigakura wao.
Alisema wakati huu ambao kampeni za uchaguzi mkuu nchini zingali
zikiendelea, viongozi wasiokubalika au kuwa na sera zisizo na ufanisi
wanaweza kukataliwa na kutoa nafasi kwa watu wengine.
Alisema ripoti hiyo inagusia zaidi masuala ya siasa na wagombea,
hususan kuhusiana na masuala yanayochukuliwa na jamii kuwa ni kero kwao.
Kati ya wahojiwa 10, sita kati yao walisema kwa asilimia 59 huduma za
afya ni tatizo la kwanza huku matatizo mengine makubwa kwao yakiwa ni
kupatikana kwa huduma ya maji (asilimia 46) na matatizo ya elimu
asilimia 44.
“Kwa mwaka huu, matatizo kuhusiana na huduma za kijamii yamekuwa
yakizungumzwa zaidi, yakiongozwa na afya, maji na elimu. Mwaka 2012 hadi
2014, tatizo lililotajwa zaidi lilikuwa umaskini na masuala ya
kiuchumi. Hivi sasa suala la kiuchumi limeshuka kutoka asilimia 63 hadi
34,” alisema Eyakuze.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa wananchi walisema ahadi wanazotoa wabunge
hazitekelezeki kwani asilimia 64 walisema wanafahamu ahadi zilizotelewa
katika kampeni zilizopita, lakini ni asilimia nane tu ndiyo walisema
kwamba mbunge wao ametekeleza ahadi zake.
Vilevile, ripoti hiyo imeonyesha kuwa asilimia 98 ya wananchi
wamejiaandikisha kupiga kura na zaidi ya asilimia 90 wamedhamiria kupiga
kura mwaka huu. Hata hivyo, ni asilimia 57 tu ya wananchi hao ndiyo
waliotaja kwa usahihi tarehe ya uchaguzi kuwa ni Oktoba 25.
Kadhalika, ripoti hiyo inaonyesha vilevile kuwa Magufuli anaungwa
mkono zaidi na wanawake kwa asilimia 68 na wanaume kwa asilimia 62 huku
Lowassa akiungwa mkono na wanaume kwa asilimia 28 na wanawake kwa
asilimia 22. Wagombea hao wanachuana vilevile katika kuungwa mkono
maeneo ya vijijini, Magufuli akionekana kukubalika kwa asilimia 66 na
mjini asilimia 61 huku Lowassa akikubalika maeneo ya mjini zaidi kwa
asilimia 28 huku vijijini asilimia 24 .
Ripoti ionaonyesha vilevile kuwa wanaomuunga mkono Lowassa
wanaamini kwa asilimia 12 kuwa ataleta mabadiliko, wanaoamini kuwa ni
mchapakazi ni asilimia mbili, na wanaoamini kuwa ana sera nzuri ni
asilimia tatu. Kwa Magufuli, asilimia saba ndiyo wanaoamini kuwa ataleta
mabadiliko, wanaoamini kuwa ni mchapakazi asilimia 26 na sera nzuri
asilimia tano.
MASWALI MAGUMU
Miongoni mwa maswali yaliyojitokeza kuhusiana na ripoti hiyo ni
juu ya kufanana kwake kwa kiasi fulani na ripoti iliyotolewa wiki
iliyopita na msemaji wa timu ya kampeni ya mgombea wa CCM, January
Makamba, iliyodai vilevile kuwa Magufuli atashinda kwa asilimia 69.3.
Akijibu swali hilo kutoka kwa mmoja wa wananchi waliohudhuria
uwasilishwaji wa ripoti hiyo, Eyakuze alisema kuwa ripoti hiyo haina
uhusiano wowote na CCM wala chama chochote cha siasa na kwamba, mbinu
zilizotumika katika utafiti wake zinakubalika duniani kote.
Kuhusiana na ufafanuzi juu ya matumizi ya simu katika kuuliza
wahojiwa, Eyakuze alisema utafiti huo wa kutumia simu za mkononi katika
maeneo 200 ya kuhesabia yaliyochaguliwa kutoka Tanzania Bara ulihusisha
kaya 10 zilizochaguliwa kutoka katika orodha ya kaya zote. Alisema mtu
mzima mmoja alichaguliwa kinasibu katika kaya na kupatiwa simu
inayotumia nguvu ya jua na kila mwezi wahojiwa walipigiwa simu kuhusu
mada mbalimbali.
Eyakuze alisema wananchi waliochaguliwa kuhusika na utafiti huo,
walichaguliwa sawa sawa na nasibu ni mbinu ambayo hutumika kukadiria
wastani wa mgawanyo wa tabia, mtazamo, au maoni ya wananchi na pia ni
mbinu inayokubalika na wanasayansi, wanatakwimu wa jamii na pia Ofisi ya
Takwimu za Taifa (NBS), vyuo vikuu, kampuni binafsi za utafiti kama za
Synovate, Ipsos, Gallup na Pew Research.
TAHARUKI
Kufuatia utafiti huo, wasomi na wanasiasa mbalimbali walitoa maoni
yao yanayopinga kwa hoja mbalimbali huku wengine wakiunga mkono.
Mkurugenzi wa taasisi ya Sikika, Irenei Kiria, alisema maoni hayo
ya utafiti hayawezi kuchukuliwa kuwa ndiyo hali halisi itakavyokuwa kwa
sababu kipindi cha wiki mbili tangu kukamilika kwa utafiti huo na sasa
kunaweza kutokea jambo lolote linalobadili misimamo ya watu.
“Wiki mbili zilizopita utafiti ndiyo ulikamilika kwa mujibu wa
Twaweza. Sasa inawezekana vipi kutueleza matokeo haya sasa... muda wa
wiki mbili ni mkubwa. Hali ya siasa inabadilika na kama utafiti huu
ungefanyika leo, huenda wangepata matokeo mengine,” alisema Kiria.
Kuhusu hali halisi ya utafiti, alisema tofauti ya CCM na upinzani
imekuwa tofauti zaidi kati ya majibu ya tafiti na muonekano wa watu.
Kuhusu matumizi na aina ya watu waliohojiwa kupata tafiti hizo,
alisema wahojiwa walipewa simu na chaji zake, hali ambayo inaonyesha
kunawerza kukosekana kwa uhuru wa kupata takwimu sahihi.
“Kitendo hiki cha kuandaliwa kwa wataalamu na kupewa vifaa vya
kufanyia utafiti kinaweza kuwafanya wafanya utafiti kuandaa majibu
mazuri ya kuwajibu wataalamu,” alisema Kiria.
Alisema wanaweza kuhofia kutoa majibu yasiyowaridhisha wataalam kwa
kuhofia kutafutwa na kuulizwa mara baada ya utafiti kubainishwa.
Pia akizungumzia kuhusu hali ukosefu wa huduma za jamii kama maji,
umeme, elimu na afya kwa zaidi ya asilimia 60, alisema ni kweli jambo
hilo linalingana na uhalisia.
“Kuhusu takwimu walizotoa juu ya uhalisia wa hali ya maisha ya
wananchi kuwa hawana huduma muhimu kama, afya, elimu, umeme na maji ni
ukweli usiopingika na wanasiasa wanapaswa kutambua suala hilo,” alisema
Kiria.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Profesa Alphonce Kessy, alisema
hawezi kutoa maoni ya utafiti huo ambao alisema haujabainisha aina ya
watu waliohojiwa na kupata majibu ya tafiti.
“Siwezi kutoa maoni ya tafiti ambazo bado sijafahamu ni aina gani
ya watu waliohojiwa... kwa mfano, waliingia ofisi gani? Na pia kujua
kama waliingia kanisani, msikitini, ofisi za CCM au vyama vingine vya
siasa kuwahoji hao watu na kupata takwimu walizozitoa,” alisema Kessy.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, msemaji wa kamati ya
kampeni ya CCM, January Makamba, alisema matokeo yaliyotolewa na Twaweza
kuonyesha kuwa chama chake kitashinda ni ya kisayansi na hivyo
hayapaswi kubezwa kwa namna yoyote ile.
Alisema walioguswa na matokeo hayo wanatakiwa kuwa na uvumilivu katika kupewa taarifa hiyo hata kama ni mbaya kwao.
“Miezi kadhaa iliyopita Twaweza walifanya utafiti na walitoa
matokeo kama hayo mimi nikiwa miongoni mwao wahusika na nilikuwa mbali
na aliongoza mgombea mwingine kwanini asingenifanyia upendeleo kama
kigezo ni ukaribu wetu?...”alihoji na kuongeza.
“Kama wanaubeza utafiti huo kwamba amechakachua mimi nashauri wamuombe radhi Eyakuze wanamkosea sana, alisema Makamba.
Post a Comment