Lowassa, Sumaye wauponda utafiti wa Twaweza majibu Oktoba 25
Mgombea
urais aliyesimamishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia
Chadema, Edward Lowassa, ameponda matokeo ya utafiti uliofanywa
naTwaweza, akisema taarifa
hiyo ni uwongo mtupu.

Alisema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano mkubwa wa kampeni katika Jimbo la Masasi jana na kuwaomba wananchi wampigie kura.
“Mmenifurahisha sana kwa mwitikio wenu huu, mmekuja kwa wingi na
mahudhurio yenu yamekuwa mazuri, asanteni sana kwa mahaba yenu. Sikujua
Masasi ina watu wengi namna hii, nimekuja kuwasalimia na kuwaombeni
kura…hii ni sunami,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Kama walivyoeleza vizuri sana awali John Mrema (Mkurugenzi wa
Uchaguzi na Bunge wa Chadema) na Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye
kuhusu ripoti ya Twaweza iliyotangazwa leo (jana), ripoti hiyo ni uongo
mtupu. Kuhudhuria kwenu kwa wingi namba hii kuna dhihirisha kuwa
nitashinda kwa kura nyingi Oktoba 25.”

Aliwaomba wananchi wampigie kura nyingi zaidi ya milioni 16. “Mnipe
kura nyingi ili hata hao jamaa wakiiba zibakie nyingi. Angalieni hao
jamaa ni wezi sana wa kura, nataka kura nyingi siyo mchezo,” alisema.
AELEZA SABABU KUUTAKA URAIS
Lowassa alisema anautaka urais kuwaili aweze kupambana na umaskini uliokithiri nchini.
“Nautaka urais ili niondoe umaskini, kwa mfano, mwenye kula kuku
mmoja ale kuku wawili, mwenye bodaboda moja au gari moja basi apate gari
mbili, na mwenye mke mmoja basi aweze kuoa wake wawili kama dini yake
inaruhusu na mkewe akiridhia hilo,” alisema.
Alitaja sababu nyingine ni kuinua elimu ili iwe bora na kuifanya kuwa bure kuanzia chekechekea hadi chuo kikuu.
Lowassa pia alisema akiwa Rais atainua zao la korosho na kupiga
marufuku utaratibu wa stakabadhi ghalani na kuwaruhusu wakulima kuuza
mazao yao popote ndani na nje ya nchi.
MGOGORO WA UBUNGE MASASI
Katika mkutano huo, Lowassa alifanya kazi ya ziada kuamua mgogoro
wa nani agombee ubunge katika jimbo hilo baada ya kuwapo kwa vuta ni
kuvute kati ya Ismail Issa Makombe (CUF), maarufu Kundambanda na
Mwenyekiti wa NLD, Dk. Emmanuel Makaidi.
Awali, baada ya kupima hali ya hewa ya umati uliojitokeza wakimtaka
Kundambanda agombee, Lowassa alisimama jukwaani na kumuomba Dk. Makaidi
kumpisha kijana huyo kugombea nafasi hiyo.
Hata hivyo, Dk. Makaidi hakuridhia ushauri huo na busara iliyotumika ni kuwaruhusu wagombea wote wawili kugombea.
MREMA
Mapema akizungumzia kuhusu utafiti wa Twaweza, Mrema alisema wana uhakika mgombea wao atapata ushindi mnono.
“Wapo watu Dar es Salaam wanakaa ofisini na kutunga matokeo ya
utafiti kuwa Dk. John Magufuli atapata ushindi kwa asilimia 65 dhidi ya
Lowassa. utafiti huo wa Twaweza haukuzingatia maoni ya watu kutoka
majimbo kama ya Masasi na Lowassa atashinda mapema asubuhi,” alisema.
SUMAYE
Kwa upande wake, Sumaye aliponda utafiti huo, akisema hauna ukweli wowote.
Aliwataka wananchi hao kupiga kura kwa wingi bila kuwa na hofu
kwamba nchi itaingia kwenye vita kwa sababu wananchi wameamua kuupigia
kura upinzani.
“Sisi tumetoka huko (CCM) na kuja huku upinzani kuonyesha upinzani una watu wenye ujuzi kuongoza,” alisema na kuongeza:
“CCM iliwaahidi maisha bora kwa kila Mtanzania, sasa wanayapata hayo maisha?” aliuliza na kujibiwa ‘hapana’.
Alimshambulia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, kuwa
amemtisha kwa kukiandama chama na yeye hataki siasa za kutishana.
“Mimi sio mtoto mdogo, hatutaki kutishana, tunauliza maswali kwa
niaba ya wananchi kuhusu biashara ya meno ya tembo, usafirishaji wa
twiga kwenye ndege kwani sisi tulikuwepo?. Sasa Warioba (Waziri Mkuu
Mstaafu, Jaji Joseph Warioba na Magufuli wanasema tumechanganyikiwa,”.
“Hakuna aliyechanganyikiwa, tunauliza hayo watupe majibu, sasa tukifanya hivyo tunaambiwa tumechanganyikiwa.”
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment