Pluijm aanza na pointi tatu Yanga
MSIMU uliopita, ikiwa chini ya Mbrazili, Marcio Maximo, Yanga ilifungua msimu kwa kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar, lakini msimu huu Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, amefunguka kuwa wapo fiti na anahitaji kupata pointi tatu katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Coastal Union.
Yanga inatarajiwa kucheza mchezo wake siku ya Jumapili wiki hii dhidi ya Coastal Union, ukiwa ni mchezo wao wa kwanza wa msimu, itakumbukwa msimu uliopita walipokuta hapo Taifa, Yanga iliiadhibu timu hiyo mabao 8-0.
Akizungumza kocha huyo alisema kuwa siku chache zilizobaki, atahakikisha anakiweka sawa kikosi chake na kukaa na wachezaji, lengo likiwa ni kuanza vyema ligi hiyo.
Kocha huyo alisema kuwa maandalizi yake yapo vyema, baada ya wachezaji wake kurejea kutoka katika timu za taifa kila mmoja akiwa na morali ya hali ya juu.
“Mechi ya kwanza siku zote inakuwa na ‘tension’ kubwa, hasa kwa wachezaji na mashabiki, lakini kama unavyofahamu mpira hautabiriki siku zote, sisi tunahitaji kupata pointi zote na kusonga mbele zaidi.
“Wachezaji wangu wapo fiti kwa ajili ya kupambana ingawa si mchezo wa kuudharau hata kidogo na kwa kuwa tutaanzia nyumbani, ni lazima tupambane ili tuweze kufanya vizuri,” alisema Pluijm.

Post a Comment