ad

ad

HADITHI: REBEKA ( Zaidi ya Mwanamke) - 20 ...Mwishoooooooo Kabisaaaaaaaa


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
Kweli shetani hupenda pale mtu unapokuwa na matatizo Rebeka alipata wazo baya la kutokukubali kuondoka peke yake alitaka kuacha simulizi ya marehemu kaacha orodha ndefu. Kuanzia hapo Rebeka alipunguza safari za kujijenga kimaisha kazi nyingi aliwatuma watu.
SASA ENDELEA...

Aliamua kuwa mtu wa kustarehe nao kina baba wakwale hawakuchoka, safari ile alikuwa mpole kila aliyemtongoza alimkubalia bila masharti kama mwanzo.
Kila aliyempata alijiona amepata kumbe amepatikana hakukubali kufanya mapenzi kwa kutumia mpira. Kila aliyempata alipolazimishwa kuvua mpira alitii amri, kila ulipoenda na mtu nyumba ya wageni alikuwa wa kwanza kuvua nguo ili uingie kichwakichwa hata wazo la kondomu linapotea.
Kila aliyegusa aliondoka nao naye aliugawa kama peremende, sifa zake mbaya ziliwanyima raha wake za watu mtu alikuwa tayari kukorofishana na mkewe ili tu ampate Rebeka.
Rebeka baada ya kumaliza waume za watu akawaanzia vijana ambao aliwahonga ili kufanya nao mapenzi wao waliona wamepata kumbe maskini walikuwa wamepatikana. Kila mmoja alimchukia pale mpakani hasa wanawake.
Siku moja akiwa peke yake amekaa dukani mwake walipita watoto wazuri wakitoka shuleni, walikuwa watoto wenye afya njema. Aliwaangalia alijikuta machozi yakimtoka moyo ulimuuma na kujiuliza nafsini hivi ataendelea kugawa maradhi yale mpaka nini nini hatma yake mbele ya Mungu.
Alijiuliza watoto wazuri kama wale wazazi wake watakapofariki lazima wataishi maisha ya kutangatanga kwa kukosa lishe bora elimu. Kilio cha mateso yao lazima kitamhukumu akiwa duniani au akiwa amekufa.
Jioni akiwa amekaa akiangalia kipindi cha mahubiri alimsikia mhubiri akisema kuwa kila mwenye mzigo wa dhambi ampelekere Bwana kwani ndiye mwenye uwezo wa kusamehe na kumfanya mtu aingie dunia mpya akiwa safi mbele ya Mungu.
Rebeka aliona hiyo ndio njia pekee iliyobakia ya kwenda kutubu mbele ya Bwana ili asamehewe makosa yake toka kumkimbia mume wake mpaka siku ile.
Jumapili Rebeka akiwa amepakatia Biblia mpya ambayo aliinunua siku alipopata wazo la kwenda kutubu madhambi yake. Hakuna aliyeamini kumuona Rebeka akiingia kanisa wapo walio mshukuru Mungu kwa kumuonyesha njia lakini wapo waliomuona shetani wa kike walitamani kutoka kanisani wamwache peke yake.
Rebeka baada ya kuingia kanisani alitafuta sehemu ya nyuma pembeni na kutulia tuli kusubiri ibada ianze. Baada ya ibada wapo waliokuja kutoa ushuhuda mbele ya kanisa. Kila mmoja alisema yale aliyoyafanya ambayo yalimchukiza Mungu.
Walikuwa wanaume na wanawake wapo waliohasi nyumba zao kwa ajili ya nyumba ndogo wapo waliotoka nje ya ndoa zao wapo waliotelekeza nyumba zao kwa ajili ulevi. Hata wachawi walitoa ushuhuda wao jinsi walivyo watesa watu kuwaua na kula nyama zao.
Ulikuwa ushuhuda wa kusisimua uliowaacha watu midomo wazi, akiwa amebakia mmoja akimalizia ushuhuda wake, Rebeka alitaka naye kwenda lakini moyo ulikuwa mzito lakini alijiuliza asipokwenda pale ambako kila mmoja alisema mabaya yake yeye anasubiri nini.
Alijilazimisha kunyanyuka na kupita katikati ya mistari miwili ya waumini walio kuwa wamekaa. Kila mmoja alimtupia jicho kutaka kujua anakwenda wapi. lakini hakujali macho ya watu alikwenda kwa mwendo wa taratibu Mchungaji alipomuona alimfuata na kumshika mkono na kumpandisha kwenye madhabahu.
"Karibu mama," Rebeka hakumjibu zaidi ya kububujikwa na machozi ilikuwa tofauti na wote waliokuja kutoa ushuhuda ni yeye tu ndiye aliyetoa machozi.
Mchungaji alimpa kipaza sauti lakini alioendelea kulia huku akiwa ameshikilia mikono kifuani ikionyesha ana maumivu makali moyoni. Mchungaji alimuinamia na kuongea naye kwa sauti ya upole.
"Najua una maumivu makali moyoni mwako na kujutia makosa yako lakini huu ndiyo wakati wako wa kuyatubu yote, kama Bwana alivyosema wote wenye mizigo mizito njooni kwake naye atakutueni haya mama ongea yaliyokusibu."
Rebeka alinyamaza na kuanza kuongea kwa sauti iliyochanganyikana na kilio maisha yake yote tokea alipotoka tumboni kwa mama yake mpaka siku ile aliyosimama pale alimalizia kwa kusema:
"Nilipojijua mimi mzuri ndio mwanzo wa kuisaliti ndoa yangu na nilipojijua nimeathirika ndipo nilipoaanza kuusambaza ugonjwa kwa wanaume wote wakware na nilipojijua namkosea Mungu ndipo nilipokuja hapa kutubu....kwa sasa hivi mimi ni muathirika wa gonjwa wa UKIMWI."
Kauli ile ilikuwa kama mshare wa moyo kwa wanawake wote waliokuwa na uhakika kuwa Rebeka alitembea na waume zao. Kanisa muda mfupi baada ya ushuhuda mzito liligeuka jumba la vilio, wengi walilia mpaka kujitupa chini huku wakisema kwa sauti:
"Ooooh Mungu wangu tumekwisha...Eva umetuuua."
Ilibidi shughuli zote za kanisa zisimamishe na kufanya kazi ya kuwahudumia kina mama na kina baba ambao wengi wao walikuwa wamepoteza fahamu. Rebeka alijutia nafsi yake lakini ndiyo hivyo maji yalikwisha mwagika.
Baada ya masaa mawili kanisa lilirudi kwenye hali yake ya utulivu na maombi mazito yalifanya kuzifariji roho za wote walioathirika na ushuhuda wa Rebeka.
Siku ileile Rebeka alitangaza pale pale kanisani kuwa mali zake zote anazikabidhi kanisani ikiwa kusaidia watoto yatima na wajane aliomba baada ya kuondoka jumba lake liuzwe na pesa ziingizwea kwenye mfuko wa kanisa.
***
Siku ya pili Rebeka alijipakia kwenye gari lake na kuamua kurudi nyumbani kwa wazazi wake hakuwa na hamu ya kuishi tena mjini. Nyumbani kwao alipokelewa na wazazi wake wote na ndugu na jamaa.
Kijijini ilikuwa furaha isiyo kifani kwa wazazi wake bahati nzuri alimkuta mwanaye ambaye alikuwa amefuatana na baba yake. Mwanaye alikuwa kwenye afya njema, wazazi wake walitaka kujua alikuwa wapi muda huo wao walijua na yeye alikuwa amekufa kwenye mauaji yale ya kutisha ambayo hayataondoka akilini mwa watu haraka.
Baada ya mapumziko na kupata chakula aliwaweka sebuleni ndugu na jamaa na kuwaelezea tamu na chungu ya maisha yake. Kila mmoja alijikuta machozi yakimtoka Rebeka naye alikuwa akiongea huku akilia kwa majuto ya kuufuata moyo wake kwa kila ulilotaka.
Wakiwa katikati ya majonzi kila mtu akitokwa na machozi Mabogo na mkewe Bibiana waliingia wakiwa na mtoto wao Mafuru. Macho yake yalitua kwenye uso wa baba mkwe alikutana na michirizi ya machozi ilibidi ajiulize kulikoni.
"Jamani kulikoni kuna habari gani?"
Kauli ile ilimfanya Rebeka anyanyue uso na kukutana na mumewe Mabogo alijikuta akisema:
"Aaah Mabogo!"
"Mungu wangu ni wewe Rebeka!?"
Rebeka bila kuongeza neno alijitupa mzimamzima kwenye miguu ya Mabogo
"Mume wangu nimekwisha kweli mshahara wa dhambi mauti."
"Rebeka una maana gani kusema hivyo?"
"Nimeathirika."
"Nini?"
"Nimeathirika nimevuna nilichopanda."
Kauli ile ilimfanya Mabogo kutokwa na machozi kama mtoto mdogo, alimnyanyua na kumkumbatia kwa mahaba mazito huku akimweleza maneno yaliyomliza kilio cha sauti Rebeka:
"Rebeka mpenzi mwanamke niliyempenda kwa moyo wangu wote na kwa nguvu na akili zangu zote najua tatizo lililokutokea si lako ni letu sote nakuahidi kauli yangu ni ileile niliyoitoa mbele ya padri siku ya kutufungisha ndoa nitakupenda kwa uzima na ugonjwa mpaka Mungu atakapomchukua mmoja wetu.
“Pamoja na yote yaliyokukuta lakini amini wewe ni mwanamke zaidi ya wanawake ni mwanamke jasiri mwenye moyo wa upendo na huruma kwa watu wote, Mungu huwa hampi vyote mwanadamu tatizo ni maamuzi bila kufikiria faida na hasara zake wewe ulifikiria faida bila kujua hasara zake ambazo ni furaha ya muda mfupi lakini majuto ya muda mrefu.
“Hilo ndilo kosa kubwa ambalo mwenyezi Mungu atakalo tuhukumiwa wanadamu ametupa akili ya kuwaza kabla ya kutenda kitu kilicho tutofautiana na wanyama ambao ni mahayawani...Lakini Nakuhakikishia Rebeka kuugua sio kufa ondoa wasiwasi moyoni mwako. Yoyote anaweza kufa sio lazima uugue kufa ni ahadi unaweza kufa bila kuumwa au kwa ajari wakati asubuhi uliamka mzima afya njema.
“Jione kiumbe uliyezaliwa upya tena sasa hivi umezaliwa kiroho ni maisha yaliyo bora mbele ya Mungu...Rebeka nakupenda sintasita kukupenda bado mke wangu mbele ya Mungu."
Rebeka alijikuta akilia kilio kilichomliza kila mmoja pale lakini Mabogo alimfariji kitu kilichomfanya moyo ulitulia. Mabogo alimuacha Rebeka kijijini kwa hakutaka tena maisha ya mjini alijenga kanisa kubwa na kituo cha kuwahudumia waathirika wa Ukimwi na kununua gari la kijiji litakalo kuwa likihudumia watu wenye matatizo.
Jina lake lilikuwa tena midomoni mwa watu mwanamke jasiri mwenye moyo wa huruma na upendo alifahamika kama dada wa kanisa. Pesa zake zote alizitumia kwa maendeleo ya kanisa. Pamoja ya yote linalomuumiza moyo wake ni upendo wa mume wake Mabogo anaamini mpaka anaingia kaburini Mabogo ni mwanaume bora mwenye sifa zote za kuwa mume wa mtu ambaye pamoja na kumfanyia yote bado upendo wake bado mbichi usioisha moyoni mwake.
Lakini ndio hivyo Bibiana ndiye mrithi wake hana jinsi amekubali yaishe. Sasa hivi Rebeka mama wa shamba mjini anakuogopa kama ukoma.
Mwisho kila mtu ameona moyo si wa kuuendekeza kila mmoja aridhike anachopata tuziheshimu ndoa zetu hata kama tunakula mara moja kwa siku. Tamaa ya mwili ni majuto ya moyo Mungu huwapenda wenye subira ya moyo ambao huwapa farijiko la milele. Hadithi hii ni tunu kwa wote waliokuwa waaminifu kwenye ndoa zao, hata kwa walio athirika nawaeleza kuugua si kufa waishi kufuta ushauri maisha yao hayatakuwa na dosari kufa kwa mtu ni ahadi.
Mwishoooooooo Kabisaaaaaaaa 
Powered by Blogger.