HADITHI: REBEKA ( Zaidi ya Mwanamke) -18

SEHEMU: 18
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
... ILIPOISHIA:
Alijikuta kwenye majuto makuu na kumkumbuka mume wake Mabogo na kuona heri mara mia maisha aliyokuwa akiishi na Mabogo kuliko ya muda ule. Alijiuliza sura yake atauweka wapi akikuta na na wanaume wale ni sawa na kutembea uchi japo atakuwa amevaa nguo.
Aliapa akitoka hospitali atatoroka na kwenda sehemu yoyote asiyojulikana kukimbia kukimbia aibu ile.
SASA ENDELEA...
***
Roja Mo aliporudi safari zake alipatwa na mshtuko kusikia mkewe yupo hospitali amelazwa. Hakuwa na haja ya kuingia ndani alikwenda moja kwa moja hospitali. Rebeka alipomuona alitamani kukimbia lakini aliificha hofu yake.
Alipogundua uso wa Roja Mo una wasiwasi walimtoa hofu kwa kumchanulia tabasamu lililo upoza moyo wa Peza na kuhoji kwa wasiwasi.
"Vipi mpenzi kulikoni?"
"Aaah ni tumbo la kike tu lilinibana gafla jana."
"Oooh afadhali..vipi hali yako kwa sasa?"
"Naendelea vizuri"
"Huduma ya hapa unaridhika nayo au tubadili hospitali?"
"Kwa kweli ni nzuri sana nawashukuru manesi na madaktari wamenipa huduma na dawa nzuri."
Rebeka alitoka hospitali baada ya siku nne na kupewa masharti ya kutokufanya kazi nzito kwa miezi miwili. Toka atoke hospitali muda mwingi alikuwa ni mtu mwenye wasiwasi juu ya kitendo cha kinyama alichofanyiwa, alimuomba Mungu Roja Mo asijue.
Zilipita wiki mbili hali ikiwa ya kawaida kitu kilichofanya moyo wa Rebeka upunguze wasiwasi kwa kujua itabakia siri kati ya watenda na mtendewa. Aliweza kutembea japo si kwa kuendesha gari zaidi ya kuendeshwa.
Siku moja akiwa amemtembelea mwanaye na mumewe Mabogo alipofika moyo ulimshtuka pale alipomkuta Bibiana mke mwenzie akiwa mjamzito wa mimba kubwa. Japokuwa mimba ni kitu cha furaha kwake kilikuwa ni kama mkuki uliomwingia moyoni mwake.
Katika mawazo yake alipanga kurudi kwa Mabogo kumuomba msamaha na Bibiana arudi kuwa mhudumu wa ndani ambaye atamlipa kiasi chochote anachotaka lakini mambo yalikwenda sivyo Bibiana alikuwa mjamzito na yeye muda si mrefu atakuwa mama wa mtoto. Alikuwa na imani baada ya kupata mtoto atasababisha Mabogo kumfuta kabisa mawazoni mwake.
Rebeka alijikuta kila muda maumivu yanadizi moyoni mwake na kuona kama ni laana ya Mungu kwa kumkimbia mumewe na sasa anamuadhibu. Hata hamu ya kwenda kijijini kuwasalimia ilitoweka na kuamua kurudi mjini ili apange mikakati mipya ya kumtoroka Roja Mo na kwenda mbali sana hata ikiwezekana bora ajiue kabisa.
Alirudi hadi nyumbani alipoingia ndani alimkuta Roja Mo akiwa sebuleni akisoma gazeti la siasa juu ya uchaguzi, alipomuona alilitupa pembeni na kumlaki kwa kumkumbatia kwa furaha.
"Yaani huwezi kuamini nilikuwa nakuwaza sasa hivi sijui mimi bila wewe itakuwaje?"
"Hata mimi nimeamua kurudi nilipokuwaza tu bila wewe sina maisha yaani uliposafiri nilipata shida sana siku moja kwangu ilikuwa mwaka."
Baada ya kupigana mabusu na kujitupia kwenye kochi wakiwa bado wamekumbatiana walishtushwa na mlio wa kengere ya mlangoni.
"Pumzika wacha nikafungue," Roja Mo alimwambia mkewe wakati huo Rebeka alikuwa akienda ndani kubadili nguo ili aende akajimwagie maji.
Roja Mo alikwenda hadi mlangoni na kufungua alikutana na mlinzi wa getini ambaye alimkabidhi bahasha kubwa aliyekuwa na maandishi makubwa ya wino wa kalamu yenye wino mzito ya rangi nyekundu ilikuwa na maandishi yaliyoandikwa MLA CHA MWENZIE NA CHAKE HULIWA.
Baada ya kuisoma alimgeukia mlinzi ambaye alijua lazima ataulizwa swali alikuwa bado amesimama mbele yake.
"Nani kakupa hii bahasha?"
"Wale rafiki zako."
"Kina nani hao?"
"Si wale ambao mara nyingi huongozana nao muda wote mmoja ni yule mfupi mweupe ulinitambulisha kama sikosei anaitwa Kanyute"
"Oooh si Kanyute ni Kanuth."
"Ndiye huyo huyo walikuwa wote wanne."
"Wameelekea wapi?"
"Mmh, sijui waliponipa tu waliingia kwenye gari na kuondoka wakati huo mimi nakuja kwako."
"Walisemaje?"
"Waliniuliza kama upo nilipowaambia upo walinipa mzigo huu na kuniambia nikuletee..tena nimekumbuka waliniuliza na mama kama yupo?"
"Uliwajibu nini?"
"Niliwajibu yupo ajabu aligonga mikono na kusema shughuli imekwisha walikumbatiana na kuondoka wakicheka kwa furaha."
"Shughuli imekwisha wana maana gani na hili neno mla cha mwenzie wana maana gani?"
"Bosi kwa kweli maswali kama hayo mimi utanionea wewe ndiye unayewajua vizuri."
"Ooh! Samahani kaendelee na shughuli zako."
Yule mlinzi aligeuka na kurudi kwenye lindo lake na kumwacha Roja Mo akiwa ameshikilia bahasha mkononi ambalo lilionekana lina picha.a Alifunga mlango na kurudi kwenye sofa na kujilaza kisha aliifungua ile bahasha ili aone kuna kitu gani.
Wakati Roja Mo anafungua bahasha Rebeka alikuwa amejifunga kanga moja na juu alikuwea ameweka taulo begani akielekea kuoga. Alipotoka chumbani alishtuka kumuona Roja Mo akifungua bahasha moyo ulimpasuka alijua huenda ni ile siri ambayo sasa inamfikia bwana yake.
Alitamani kuikimbia na kuinyakua kabla Roja Mo hajaanza kuziangalia zile picha. Miguu ilikuwa mzito alibakia amesimama kama sanamu akimwangalia Roja Mo alichambua picha moja baada ya nyingine.
Roja Mo ambaye baada ya kuanza kuziangalia zile picha hazikuwa tofauti na zile alizopewa Rebeka kote alipotazama hapakumshtua sana japo sehemu ya Rebeka kuongozana Lyasingo Hotel lilimfanya jasho limtoke alijua kazidiwa akili.
Pigo kubwa lililomfanya apige kelele na kuzirai lilikuwa ni zile picha chafu alizokuwa amepigwa Rebeka na ujumbe wa maneno unaosema:
Mheshimiwa kazi imekwisha huwezi kutuzidi akili sisi ndiye tuliyekukaribisha mjini ongea na watu uvae viatu, siku zote mla cha mwenzie na chake uliwa. Chetu chako cha kwako chako mwenyewe hii haipo ukijua kupokea ujue na kutoa.
Hii shughuli unayoiona imeghalimu milioni mia mbili hamsini kwa hiyo ili issue hii ibakie siri yetu malipo yake milion mia nne bila hivyo kona yote ya nchi hii na jirani picha za mpenzio zitazagaa kuanzia kesho tunataka hizo pesa, wewe si kiburi basi hapa ni maji marefu.
Upatapo ujumbe huu tujulishe tupo sehemu yetu ya kawaida.
Roja Mo baada ya kusoma ujumbe ule alipiga ukelele na kuzimika kwa kusema
"Oooh wamenimaliza."
Rebeka aliyekuwa akimfuatilia Roja Mo alishtuka kama mtu aliyepigwa na shoti ya umeme na kujikuta akikurupuka kumkimbilia.
Alimkuta akiwa chini ameishapoteza fahamu, alizitupia macho zile picha zilikuwa zile zile chafu. Wazola ghafla lililomuijia ni kutoroka kwa kuhofia Roja Mo alipata fahamu huenda atachukua maamuzi mabaya.
Alikumbuka kauli ya Roja Mo kuwa yupo tayari kutoa roho ya mtu ili kuhakikisha anamlinda kwa gharama yoyote tena alimuonyesha siraha kwa kusema mwenye pesa hata akiua hadharani hafungwi wanaofungwa ni masikini tu.
Hakutaka hata kumsaidia alikimbilia chumbani na kuchukua vitu vyake muhimu na kuvipaki kwenye mabegi na pesa zilizokuwepo kwenye kabati kama milion sabini na kupitia zile picha na kuviweka kwenye gari lake na kuondoka huku mlinzi alikiwa amepigwa butwaa.
Rebeka alipitia kituo cha mafuta kujaza mafuta na safari ya sehemu isiyojulikana ilianza. Pamoja na kuelezwa usifanye kazi nzito lakini aliamua liwalo na liwe. Aliendesha gari kwa kasi kufuata barabara inayotoka nje ya mji.
****
Mlinzi ile hali ya uondokaji wa tajiri wake kike Rebeka ilimtia wasiwasi maana hata mlango hakufunga. Aliamua kwenda ndani japo huwa haruhusiwi kuingia ndani bila sababu maalumu. Alipoingia ndani aliona hali imekaa sagarabagara. Alikwenda kwa mwendo wa taadhari hadi subuleni. Macho yake yalitua kwenye mwili wa mtu aliyekuwa amelala chini.
Nini kitaendelea? Kuyajua yote endelea kufuatilia.
Post a Comment