Ubunge viti maalum CCM waibua mapya Singida
Kinyang’anyiro cha ubunge wa viti maalum
katika mkoa wa Singida kimeibua mapya, baada ya Mwenyekiti wa Jumuiya
ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Ikungi, Christina
Hamis, kutishia kususia kuingia kwenye ofisi za jumuiya hiyo na kuhama
chama.
Mwenyekiti huyo anakusudia kuchukua uamuzi huo kwa madai kuwa
Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Aluu Segamba, anamlazimisha amuunge mkono
mgombea ubunge wa Viti Maalumu (CCM), Wema Sepetu.
Christina alisema pamoja na kwamba yeye ni Mwenyekiti wa UWT
wilaya, jambo linalomshangaza ni kuona mambo yasiyoridhisha yakifanyika
ndani ya nyumba za mawakala wa mgombea ubunge huyo.
Alisema tangu mchakato umeanza amekuwa akipokea kauli za kashfa na
matusi kutoka kwa watu wa karibu wa Wema akiwamo mama yake, Mariam
Sepetu, kutokana na kutomuunga mkono mtoto wake.
Mariam Sepetu alipoulizwa kuhusu kutoa maneno ya kashfa kwa
Mwenyekiti wa UWT, alisema hawezi kujibu mambo yoyote kuhusu kiongozi
huyo.
Christina alisema kwa mara kadhaa amewasilisha malalamiko yake kwa
Katibu wa CCM wilaya ya Ikungi, Segamba kuhusu matusi, kashfa na vitisho
anavyopata, lakini hapewi ushirikiano.
“Nimemweleza Katibu wa Wilaya mambo nayofanyiwa, lakini niliishiwa
kuambiwa siwezi kupata msaada wowote kwenye ofisi hiyo na kwamba
niachane na Wema kwa sababu ameletwa na kiongozi mmoja mkubwa wa
serikali, mawaziri na mtoto wa kigogo agombee ubunge,” alisema.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, maamuzi ya kugombea ubunge kwa Wema
kumetokana na kushawishiwa na vigogo wa serikali na kwamba viongozi
waliopo mkoani hapa wanatakiwa kumuunga mkono.
Christina alisema baada ya kuona hasaidiwi, aliwasilisha malalamiko
kwa Katibu wa UWT Mkoa wa Singida, Anjela Mirembe, lakini jibu
alilopatiwa ni kwamba Wema ameletwa na wakubwa na hivyo aachane naye.
Alipotakiwa kuzungumzia malalamiko ya mwenyekiti huyo wa UWT wilaya
ya Ikungi, Mirembe alithibitisha kupokea malalamiko hayo kwa maneno,
badala ya maandishi kama taratibu za kiutendaji wa kazi za kiofisi
zinavyoelekeza na hivyo kushindwa kuyafanyia kazi.
Katibu wa UWT wilaya ya Ikungi, Yagi Kyaratu, alisema alipokea
malalamiko hayo kutoka kwa mwenyekiti wake na kuyawasilisha kwa Katibu
wa UWT mkoa wa Singida.
Katibu wa CCM wilaya ya Ikungi ambaye pia ni kaimu katibu wa CCM
Mkoa wa Singida, Segamba, alipotafutwa ili aweze kujibu tuhuma
zilizoelekezwa kwake alijibu kuwa yupo kwenye kikao.
Kwa upande wake, Wema alipotafutwa jana, simu yake hukupatikana na
hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi, hakujibu hadi tunakwenda
mitamboni.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment