Zoezi la BVR ni balaa Dar
Haruni Sanchawa, Dar Zoezi la uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia mashine za Biometric Voters Registration (BVR) lililoanza juzi jijini Dar es Salam, limekuwa ni balaa kwa wakazi wake kutokana na matatizo mengi yaliyojitokeza hivyo kusababisha adha kwa wananchi.
Katika Kata ya Chanika, wilayani Ilala,
gazeti hili lilishuhudia jana maofisa wakifika kituoni wakiwa
wamechelewa kwani saa mbili zoezi la uandikishaji lilikuwa bado kuanza
huku wananchi wakiwa wamewahi kufika saa 11 alfajiri, hivyo kuzusha
manung’uniko.
Kero nyingine iliyolalamikiwa na
wananchi ni ucheleweshwaji wanapoingia kwenye mashine hizo tatizo ambalo
lilielezwa na mtaalamu mmoja wa mtandao (IT) aliyeomba jina lake
kuhifadhiwa kwa kuwa siyo msemaji kwamba linachangiwa na vumbi.
Aliongeza kusema kuwa mashine hizo ni za kielektroniki, hivyo zinatakiwa kuwa safi hazipaswi kukutana na vumbi.
Katika Kituo cha Mwenge Mlalakua,
wananchi wengi walilalamikia foleni kuwa ndefu na zoezi kwenda taratibu
sana huku wakidai kuwa kuna makundi ya wazee wanaingizwa ndani na
huchukua muda mrefu kutoka.
“Tulikuwa watu wengi sana hapa, zaidi ya
mia tatu, lakini tukaambiwa wataandikishwa watu mia mbili tu kutokana
na uwezo wa mashine. Hii ni mbaya na inakatisha tamaa,” alisema John
Kijo mkazi wa Mwenge.
Gazeti hili lilifika Mitaa ya Kawe, Bunju, Sinza, Msasani, Kijitonyama na Kinondoni na kukuta matatizo ni hayohayo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi
Meck Sadiki alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana alisema
ana imani zoezi hilo litakwenda kama lilivyopangwa kwani uandikishaji
huanza saa mbili hadi saa 12 jioni.
“Tangu juzi hadi jana hakuna taarifa
yoyote iliyonifikia kuhusu uvunjifu wa amani au mtu kuharibu utaratibu
uliokuwa umeandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, changamoto nyingine
zitatatuliwa haraka,”alisema.
Jiji la Dar es Salaam lina jumla ya watu
4,713,217 kati yake wenye sifa ya kupiga kura ni 2,932,930 na lina
Wilaya za Temeke, Kigamboni, Ubungo, Kinondoni na Ilala, huku majimbo
yakiwa ni kumi baada ya Nec kuongeza majimbo mawili ya Mbagala na
Kibamba.

Post a Comment