ad

ad

Ngoma, Cannavaro ‘waua’

Dar es Salaam
Matukio mawili makubwa uwanjani ya wachezaji wenye majina makubwa na nyota yalitosha kuilaza Yanga na mashabiki wake mapema katika mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Kagame dhidi ya Gor Mahia ya Kenya ilipofungwa mabao 2-1.

Mgeni wa heshima kwenye ufunguzi wa mashindano hayo ni aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga badala ya mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli ambaye ni rafiki yake wa karibu.


Dk Magufuli ndiye aliyetajwa awali kuwa angekuwa mgeni rasmi, lakini hakutokea Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kutolewa kwa kadi nyekundu kwa mshambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma, dakika ya 23 ya mchezo na mwamuzi Mashood Ssali kutoka Uganda na lile la nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kukosa penalti, kipindi cha pili katika mchezo, yalitosha kuzima ndoto za Yanga kuanza vyema mashindano hayo.

Timu hiyo iliyocheza vizuri mwanzo wa mchezo na kwa karibu dakika 67 ikiwa upungufu, ndiyo iliyotangulia kuandika bao la kwanza la ‘zawadi’, dakika ya 6 ya baada ya Ngoma kuambaa na mpira katika wingi ya kushoto na kumimina krosi iliyosindikizwa wavuni na beki Dirkir Glay wa Gor Mahia katika jitihada za kuokoa.

Dakika za mwanzo za mchezo huo, Ngoma alianza kwa kasi akiwasumbua mabeki wa Gor atakavyo na kutoa krosi ambazo zilionyesha kuwasumbua alianza siku vibaya kwa kadi ya njano baada ya kumvuta jezi mpinzani wake, Godfrey Walusimbi. Beki wa Gor Mahia, Sibomana Abouba naye akionyeshwa kadi ya njano dakika ya 11 kwa kumchezea vibaya Juma Abdul wa Yanga.
Gor walisawazisha bao kupitia kwa Haroun Shakava akiunganisha wavuni mpira wa adhabu uliochongwa na Dirkir Glay baada ya Juma Abdul kumfanyia madhambi Walusimbi, huku mabeki wa Yanga wakishindwa kuwakaba wapinzani wao.

Bao hilo lilipokewa kwa shangwe na nderemo na mashabiki waliokaa kwenye jukwaa ambalo kwa kawaida hukaliwa na mashabiki wa Simba, huku upande wa mashabiki wa Yanga ukipooza kwa kushindwa kuamini kitu kilichokuwa kikitokea.
Dakika ya 23, mwamuzi Ssali alimtoa nje Ngoma baada ya mshambuliaji huyo aliyetua Yanga akitokea Platinum ya Zimbabwe mwezi uliopita kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kwa kumpiga ngumi Shakava.

Adhabu hiyo inamfanya Ngoma kukosa mchezo ujao wa Kundi A baina ya Yanga na Telecom ya Djibouti, Jumatano.
Mshambuliaji wa Gor Mahia aliyekuwa mwiba kwa ngome ya Yanga, Michael Olunga alikaribia kuifungia timu yake bao la pili dakika ya 32, lakini shuti lake alilopiga akiunganisha krosi ya Walusimbi lilipaa sentimita chache kutoka lango la Yanga. Dakika ya 40, kipindi cha kwanza, mabingwa hao wa Kenya kupitia kwa washambuliaji wake, Olunga, Walusimbi na Shakava walilitia lango la Yanga katika misukosuko, lakini mabeki walikaa imara na kuokoa hatari.
Katika mfululizo wa mashambulizi hayo, shuti la Olunga liligonga mwamba na mpira kuokolewa na mabeki wa Yanga na hivyo hadi mapumziko timu zilikuwa zimefungana bao 1-1.
Gor Mahia ilijipatia bao la pili, sekunde chache baada ya kipindi cha pili kuanza kupitia kwa Olunga baada ya kuwachambua walinzi watatu wa Yanga kabla ya kupiga shuti lililomshinda kipa Ally Mustafa ‘Barthez’.

Dakika ya 61, Walusimbi alionyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea vibaya Juma Abdul wa Yanga. Mabadiliko yaliyofanywa na kocha mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm ya kumtoa Simon Msuva na kumwingiza Kpah Sherman yaliiongezea kasi kwenye safu ya ushambuliaji na kupata penalti dakika ya 72.Penalti hiyo ilitolewa baada ya Nigiziyimana Karim wa Gor Mahia kuunawa mpira akiwa ndani ya eneo la hatari kufuatia krosi iliyopigwa na beki Mwinyi Haji.

Hata hivyo, mpira hafifu uliopigwa na nahodha Cannavaro uliokolewa na kipa Oluoch anayesemekana kuwa katika rada ya usajili ya Simba inayosaka kipa mzoefu, hatua iliyoibua nderemo kutoka kwa mashabiki wa Simba walioishangilia kwa kiasi kikubwa Gor Mahia.
Yanga walifanya maadiliko dakika ya 84 kwa kumtoa Deus Kaseke na kuingia Salum Telela, huku Gor Mahia ikimtoa Walusimbi na nafasi yake ikichukuliwa na Ronald Omino.
Vikosi vilikuwa:

Yanga: Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Deus Kaseke, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Amissi Tambwe, Simon Msuva.
Gor Mahia: Boniface Oluoch, Karim Nizigiyamana, Sibomana Abouba, Mussa Mohamed, Haruna Shakava, Dirkir Glay, Innocent Wafula, Khalid Aucho, Medie Kagere, Michael Olunga, Godfrey Walusimbi.

Nao wawakilishi wengine wa KMKM kutoka Zanzibar wameanza vyema mashindano hayo baada ya kuilaza Telecom ya Djibouti bao 1-0 katika mchezo mwingine wa Kundi A uliofanyika kwenye Uwanja wa Karume.

Katika mechi ya mapema, Kundi B, APR ya Rwanda ilisubiri hadi dakika ya 64 kuandikisha ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Al- Ahly Shandy ya Sudan.
Leo, Azam wanaanza kibarua dhidi ya KCCA ya Uganda, Kundi C Heegan ya Somalia dhidi ya LLB ya Burundi, saa 8.00 mchana na Adama City ya Ethiopia na Malakia ya Sudan Kusini.
Powered by Blogger.