AZAM WAZUNGUMZIA TAARIFA ZA KUMSAJILI MESSI
SIKU moja baada ya kiungo
mshambuliaji wa Simba, Ramadhan Singano ‘Messi’ kuonekana katika viungo
vya makao makuu ya Azam fc eneo la Mzizima jijini Dar es salaam, uongozi
wa klabu hiyo umekanusha kumsainisha nyota huyo.
Taarifa zimesambaa kwenye
vyombo vya habari kwamba Azam imemsajili Messi ambaye ana mgogoro wa
kimkataba na klabu yake ya Simba, lakini makamu mwenyekiti wa klabu
hiyo, Nassor Idrissa ‘Father’ amekanusha habari hizo akidai hawajaingia
kandarasi yoyote na Messi.
“Ramadhan Singano sina hakika
nalo kwasababu mimi sikumuona kwa macho yangu, hata kama kuna mtu
alimuona sio tatizo, ofsi zetu si jela au mahakama, Singano ni mtu
huru,anaweza kuonekana si tatizo”. Amesema Idrissa na kufafanua: “Hakuna
kandarasi yoyote tuliyoingia na Messi, hatujazungumza naye, narudia
maneno yangu, kwa macho yangu sikumuona katika ofsi zetu”
Hata hivyo Azam wanaiwinda saini ya Messi na kama sakata la mkataba wake litakwisha, wanaweza kumsainisha wakati wowote.
Messi anadai alisaini mkataba
wa miaka miwili katika klabu yake ya Simba Mei 1, 2013 na unamalizika
Julai 1, 2015, wakati Simba wao wanasema alisaini mkataba wa miaka
mitatu Mei 1, 2013 na utakwisha Julai 1, 2016.
Post a Comment