Walimu kugoma Oktoba mosi..Wanaidai serikali sh bilioni sita.
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT), kimetoa mwezi mmoja kwa
serikali kulipa malimbikizo yao ya madeni ya walimu yanayofikia bilioni
33.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, rais wa
chama hicho, Greisoni Mukoba, alisema wamechoka kupewa ahadi hewa na
serikali ndio maana wamefikia hatua hiyo.
‘Tumetoa mwezi huu wa tisa uwe wa mwisho kuililia serikali, baada ya
hapo tutaamua hatua gani tufanye, maana tumekutana na makatibu wakuu wa
wizara zinazowahudumia walimu lakini bado tunaishia kupewa ahadi hewa,”
alisema Mukoba.
Mukoba aliongeza kuwa Agosti 14, mwaka huu, walikutana na makatibu
wakuu wanaowahudumia walimu pamoja na Katibu Mkuu ofisi ya Rais
Menejimenti ya Umma, wakatakiwa kuwasilisha madai yao yote.
“Tulikutana na makatibu, katika kikao hicho, tuliwafahamisha kuwa
walimu wanaidai serikali zaidi ya sh bilioni 33 na mwisho wa kikao hicho
tulikubaliana CWT iwakilishe madai hayo ndani ya wiki mbili,”
aliongeza Mukoba.
Mukoba alisema wiki mbili zilipofika, walienda kuonana tena na Katibu
Mkuu, ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na kuwasilisha
vitabu vyenye madai mbalimbali ya walimu.
“Madai hayo tuliyaambatanisha kwenye barua Na CWT/004/UTMS/VOL.11/94
na madai hayo sasa yamefikia sh bilioni sita,” alisema Mukoba.
Mukoba aliishangaa serikali kuanzisha Mpango wa Matokeo Makubwa sasa
“Big Result Now”, huko walimu ambao ndio watekelezaji wakubwa wa mpango
huo, wana maisha magumu kutokana na mishahara kuwa midogo na kuzidi kwa
malikimbizo ya madeni yao.
“Walimu ambao ndiyo watelekezaji wakuu wa mpango huu japo hawaelewi au
hawajapewa semina elekezi, lakini ndio watekelezaji wakubwa.
Naishangaa serikali kuwadharau walimu na nakuhakikishia mpango huo
hautafanikiwa kama walimu hawapati haki zao,” alisema Mukoba.
Mukoba aliionya serikali ikamilishe madai ya walimu ili wafanye kazi kwa moyo tofauti na sasa ambapo wengi wamekata tamaa.
‘‘Walimu wa nchi hii wamekata tamaa. Mioyo yao imekufa ganzi kwa sababu serikali imekataa kuwalipa malimbizo yao.
Kwa nini serikali imeamua kuwatendea jeuri walimu kiasi hiki?” alihoji Mukoba.

Post a Comment