ad

ad

Kitanzi, Kisu au Bastola - 12

Wakaingizwa ndani ya lifti na kupelekwa hadi ghorofa nyingine, huko wakakabidhiwa kwa Madam Bernadeta na kupewa nguo zenye rangi sawa kisha wakapelekwa kwenye jukwaa kubwa ambalo ndani yake kulikuwa na wasichana wengi wakiwa na nguo kama zao.


Kwa harakaharaka, Carolina na Sonia wakajua kwamba tayari wamerudishwa tena kutumika ndani ya jumba la Serenity kwa kuwa hawakuwa wageni ndani ya mazingira hayo.

Wakati huo, Sonia alikuwa akitokwa na machozi mfululizo kwa kuwa alimkumbuka sana mume wake Side na watoto wake ambao mpaka siku hiyo hakujua nini kilichokuwa kikiendelea kwa upande wao.
Wakati huohuo, Carolina alikuwa akiwaza jinsi ya kumpata Salima msichana ambaye aliongea naye siku chache zilizopita. Moyoni mwake alijua kama akionana na msichana huyo basi kila kitu kinachomhusu Dedan atakifahamu.
“Niambie, unamfahamu Salima?” Carolina alimuuliza Julieth bila kutoa salamu yoyote ya kiungwana. 
“Salima! Unamaanisha Caro?” aliuliza Julieth.
“Mimi namfahamu kwa jina la Salima tu na si vinginevyo.”
“Kwani mnafahamiana?”
“Sijawahi kumuona hata siku moja. Naomba unioneshe kama yupo hapa tafadhali.”
“Tangu leo asubuhi sijamuona… labda nikupeleke kwenye chumba chake,” alisema Julieth na kumuongoza Carolina huku Sonia naye akifuatia kwa nyuma.
“Hiki ndiyo chumba chake,” alisema Julieth huku akiufungua mlango wa chumba cha Salima bila kubisha hodi.
Wakiwa wanajishauri waingie au wamsubiri, mwenyeji wao awakaribishe, mara wakasikia kicheko kikali kikitoka ndani ya chumba hicho. Walipoingia walimkuta Salima akirukaruka juu ya kitanda chake huku masikioni akiwa na ‘headphone’ alizozichomeka kwenye ‘ipod’ yake. Ni wazi kwamba alikuwa akisikiliza na kucheza nyimbo fulani kwa fujo.
Salima alipowaona, akaacha uchizi aliokuwa akiufanya na kuteremka kitandani kisha kwa mashauzi akamfuata Julieth na kumtazama kwa madaha kabla ya kufanya vivyohivyo kwa Carolina na Sonia.
“Caro, una nini leo? aliuliza Julieth kwa mshangao baada ya kuhisi mabadiliko makubwa kwenye tabia ya Salima tofauti na alivyokuwa akimfahamu.
“Kwani vipi! Hawa akina nani?” Salima aliongea kwa dharau huku macho yake yakitua kwenye uso wa Carolina na kumuangalia kwa muda huku akisubiri jibu la swali lake.
“Hawa ni wageni wako. We wasikilize mwenyewe bwana!” Julieth alijibu kwa hasira na kutaka kuondoka, lakini aliamua kusubiri asikilize kitu gani wasichana hao walitaka kuongea na Salima au Caro kama alivyokuwa akiitwa.
“Mimi naitwa Carolina, tuliongea wote kwenye simu siku chache zilizopita,” aliongea Carolina kwa sauti ya chini baada ya kubaini kamera iliyokuwa imetegwa kwa kificho pembeni ya ua, akahisi lazima kutakuwa na kinasa sauti mahali fulani karibu na waliposimama.
“Carolina? Mbona mimi sikufahamu,” Salima alijibu kwa sauti na harakaharaka bila ya kuipa nafasi akili yake ifikirie.
“Tulikuwa tumuongelee Dedan. Bado haujakumbuka?” Carolina alisisitiza.
“Sikia dada, mimi sikukumbuki hata kidogo…naomba tusipotezeane muda. Kama hauna kitu cha msingi, ondoka.”
“Lakini…wewe si ndiyo Salima?”
“Hapana, mimi naitwa Caro,” aliongea Salima na kuvaa headphone zake huku akiendelea kucheza wimbo aliokuwa akiusikiliza.
Carolina alivunjwa nguvu na kauli hiyo ya Salima kwa kuwa alimtegemea msichana huyo kama mtu pekee atakayeweza kumsaidia kukutana na Dedan wake kwa mara nyingine.
***
Afande John akiwa kwenye haraka, alikatiza wodi ya watoto, Muhimbili akielekea kwa daktari mkuu wa kitengo hicho, Dr. Denis Mtima ambaye alimpeleka moja kwa moja mpaka kwenye chumba walicholazwa watoto wa Side. Watoto ambao walinusurika kifo kwenye ajali mbaya ya moto.
Mengi yalikuwa yakiongelewa kuhusiana na tukio hilo, lakini ukweli ulikuwa ndani ya mioyo ya watoto hao ambao kama walikuwa wamerudiwa na fahamu basi watawataja wahusika wote pamoja na chanzo cha moto ule.
Kwa mujibu wa daktari huyo, watoto hao walikuwa wameanza kupata nafuu na kuweza kuongea, hivyo hiyo ilikuwa ni nafasi pekee ya afande John kuwauliza maswali ili kujua nini kilichokuwa kimetokea siku ile.
“Hamjambo watoto wazuri?” aliongea afande John huku akiwapatia pipi na chokleti watoto wale ambao walikuwa wamelala kwenye vitanda tofauti. Wakapokea na kushukuru.
“Eti mama na baba wapo wapi?” aliuliza Habida, mtoto wa kwanza wa Side na kumfanya mwenzake aitwaye Safia ageuze shingo yake haraka na kumtazama afande John kwa makini.
“Baba na mama wanakuja sasa hivi. Wamenituma niwaletee hizo zawadi kwanza,” aliongea afande John huku moyo wake ukimuuma kwa kuongea uongo.
Akafungua mkoba wake na kutoa picha za watu kadhaa. Akawaonesha wale watoto picha moja baada ya nyingine akitaka wachague picha za watu waliowahisi kuwaona siku ya tukio. Picha ya kwanza kuchaguliwa ilikuwa ya Dedan na baada ya kuchambua picha nyingine ilionekana picha ya Henry.
Wa kwanza kushtuka alikuwa ni Safia ambaye alipoitazama picha ile alifumba macho kwa woga na kugeuza shingo yake kana kwamba aliiona taswira mbaya ya ‘Lusifa’ mwenyewe.
Baada ya kugundua hilo, afande John akaigeuza picha hiyo haraka na kuirudisha kwenye mkoba wake ili asiwaumize watoto hao walioonekana kupitia maumivu makali tofauti na umri wao.
Kwa kitendo cha watoto hao kuiogopa picha ya Henry, tayari afande John aligundua kuwa mtu huyo hakuwafanyia jambo jema watoto hao tofauti na Dedan ambapo walipoiona picha yake walitazama bila woga wowote.
Akawageukia tena watoto wale na kuanza kuwahoji. Walisimulia kila kitu kilichowatokea ikiwemo jinsi Henry alivyowachukua shuleni kwao kwa kujifanya mjomba wao.
Pia wakasimulia walivyopelekwa nyumbani na kufungwa kamba ambapo chumba cha pili walisikia sauti ya baba yao, yaani Side akilia kwa uchungu kabla ya baadaye kusikia mlio wa kuogofya ambao afande John alitambua kuwa walikuwa wakimaanisha mlio wa risasi.
Mwisho kabisa wakaelezea jinsi moto ulivyowaka na kuwazingira kila kona.
“Aliyeyafanya yote hayo ndiye huyu?” aliuliza afande John kwa mara nyingine huku akitoa picha ya Henry na kuwaonesha watoto wale jambo ambalo liliwashtua sana na kuwafanya wapige kelele kwa nguvu.
“Afande, mahojiano gani hayo ya kuwatisha watoto kiasi hicho? Naomba uondoke mara moja!” Dk. Denis aliongea kwa jazba akimtimua afande John.
Kwa kutambua hilo, afande John akatekeleza agizo la daktari bila ubishi kwa kuwa alitambua fika kuwa watoto wale walikuwa bado kwenye mfadhaiko kwa yote yaliowatokea, hivyo kama Dk. Denis asingemkataza angeweza kuwasababishia presha na matatizo mengine.
Afande John aliondoka mara moja katika wadi hiyo, safari hii angalau alikuwa na uhakika kuwa amepata mahali pa kuanzia.
“Hallow afande Prisca! Umepata chochote?” aliongea afande John kupitia simu yake ya mkononi huku akitembea kuelekea mahali alipoipaki pikipiki yake.
“Ndiyo mkuu, wengi kati ya hawa wasichana waliopo pichani, wamewahi kuripotiwa wamepotea mitaani mwao. Sasa sijui kama walitoroka makwao kwa makusudi au vipi?” alizungumza afande Prisca ambaye ni afisa upelelezi kitengo cha uhalifu kwa njia ya mtandao.
“Mh…Hapo kuna tatizo, nakuja sasa hivi,” alijibu afande John na kuondoka hospitalini hapo.
Kwa mbali Henry aliyekuwa amejibanza kwenye foleni za wagonjwa, alimtazama afande John akiondoka. Akaishusha kofia yake chini zaidi na kuficha sehemu kubwa ya uso wake kisha akaingia ndani ya hospitali ileile aliyotoka afande John, mkononi mwake akiididimiza bastola yake aina ya ‘revolver’ ndani ya mifuko ya koti lake.
Bila kutiliwa mashaka na mtu yeyote, Henry akaingia mpaka kwenye varanda kuu na kuelekea chumba walichokuwamo watoto wa Side.
***
Akiwa mwenye kukosa tumaini, Carolina alimtazama Salima kuanzia chini mpaka juu kana kwamba hakutaka amsahau kabisa katika kumbukumbu zake.

Katika kutazama huko, mara akagundua kidoa chekundu katika kiganja cha mkono wa Salima. Ghafla akamfuata na kumshika mkono wake akikitazama kidoa kile kilichofanya kipele kidogo juu ya mshipa wake wa damu.

Kwa hasira Salima akamsukuma Carolina na kumtaka aondoke chumbani kwake mara moja.
Kwa tahadhari ya kutoharibu mipango yake, Carolina alitoka nje ya chumba cha Salima akiongozana na Sonia na Julieth ambao wote walipigwa na butwaa wakiwa hawajui maana ya kitendo alichokifanya Carolina.

“Wewe una uhakika kama yule ndiye Salima?” aliongea Carolina kwa ghadhabu akimwangalia Julieth usoni kana kwamba alidanganywa na kupelekwa kwa mtu mwingine mbali na Salima.
“Ndiye yeye mwenyewe…kama huamini waulize wote humu ndani.” Julieth alijitetea baada ya kuona uso wa Carolina ukiwa umefura hasira.
“Umeshawahi kumuona Salima akiwa katika hali ile au amebadilika?”
“Salima ni mpole na mwenye aibu nyingi, leo amebadilika sana, hata mimi mwenyewe amenishangaza.”
Kwa jibu hilo la Julieth, tayari Carolina alielewa kuwa huenda msichana huyo alikuwa amechomwa sindano ya dawa za kulevya ‘Ecstasy 33’ iliyomfanya apoteze haiba na kumbukumbu zake za awali. Carolina alilijua hilo kwa kuwa hata yeye mwenyewe alishawahi kuchomwa sindano hizo na mtu ambaye si mwingine zaidi ya Dr. Church; Mkemia hatari ambaye kipaji chake alikitumia vibaya kwa kuumiza kundi fulani la watu na kujinufaisha mwenyewe.
Miaka kadhaa iliyopita, Mzee huyo aliajiriwa na ‘Serenity,’ huku kazi yake kubwa ikiwa ni kutumia dawa zake kwa msichana yeyote aliyeonekana kutoendana na taratibu za ‘Serenity,’ hasa katika suala la kutumika kimapenzi.
“Bila shaka Salima ni msichana mwenye msimamo sana kiasi cha kudungwa madawa. Kwa sasa sina la kufanya. Itanilazimu nimsubiri mpaka atakapopata ahueni,” Carolina alijisemea kimoyomoyo akikumbukia jinsi alivyokuwa akichomwa sindano hizo kila mara alipovunja kanuni za jumba hilo.
Akajiangalia mikononi na kuona alama za makovu ya sindano zile yakiwa yameanza kufifia. Akashusha pumzi kwa nguvu akitafakari jinsi ya kutoka ndani ya jengo hilo akiwa na Dedan, mwanaume aliyedhamiria kumpata kwa hali yoyote.
***
Wakati huo Dedan alikuwa akipata huduma nzuri tofauti na wenzake. Yeye alipata nafasi ya kuwa karibu zaidi na Madam Flaviana. Wakazungukia kila kona ya jumba la ‘Serenity’ isipokuwa upande wa vyumba vya wasichana waliowekwa tayari kwa ajili ya kuuzwa kwa wanaume Wakizungu.
Kwa hali hiyo, Dedan akawa kama mmoja wa wafanyakazi wa karibu wa madam Flaviana huku mwanamke huyo akiwa makini kutomkutanisha na Salima wala Caro akiepuka kuharibu mipango yao.
***
Henry bila kusuasua, aliufungua mlango wa chumba walichokuwemo watoto wa Side huku mkono wake wa kulia ukiishika vyema bastola yake. Akaingia ndani na kutupa macho yake juu ya vitanda na kuwaona watoto wote wawili waliokuwa wamelala kwa kujifunika kwa mashuka mwili mzima.
Akakenua meno yake na kuwafuata taratibu huku akiufunga mlango kwa nyuma. Akajongea mpaka kwenye kitanda cha mtoto wa kwanza na kufunua shuka kwa kutumia mdomo mrefu wa bastola yake, akitumaini hapo atakiona kichwa cha mtoto mmoja wapo ili amuulie mbali lakini badala yake akauona mto.
Alipofunua shuka lote alikutana na mito na mashuka yaliyopangwa vizuri na kufanya shepu kama ya watu waliolala. Kabla hajafanya chochote alishtukia mdomo wa bastola ukimgusa nyuma ya kichwa chake.
“Taratibu rusha bastola yako pembeni na uinue mikono juu. Ukijaribu kufanya chochote nakufumua ubongo wako,” ilisikika sauti ya afande John.
“Kivyovyote huyu mtu atakuwa anajua vyema kuitumia bastola yake. Hapa sina ujanja zaidi ya kutii maagizo yake,” Henry alijionya mwenyewe kimoyomoyo na kufanya kama alivyoagizwa.
Kufumba na kufumbua Henry alishtukia yupo chini huku mikono yake ikiwa imefungwa pingu kwa nyuma. Pamoja na mwili wake wa miraba minne, Henry hakuwa na ujanja wowote mbele ya afande John.
Kwa mshangao, Henry akabaki akistaajabu jinsi ambavyo afande John alirudi hospitalini hapo haraka kiasi kile, wakati kwa macho yake alimshuhudia akiondoka? Baada ya dakika chache, askari wengine walifika katika eneo hilo na kumpeleka Henry kituoni kwa ajili ya mahojiano.
***
Siku zikazidi kuyoyoma huku Salima akiwa amebakiza siku tatu kabla ya ujio wa Prince Khalfani; mgeni ambaye yeye na Julieth walipangiwa kuwa naye katika kipindi chote cha ziara atakayoifanya nchini.
Mr. Chakos na Madam Flaviana chini ya usimamizi wa Madam Bernadeta, walikesha wakifanya kazi kuhakikisha Salima au ‘Caro’ kama walivyomwita anakuwa katika afya nzuri na kupatiwa mafunzo yote muhimu ilimradi asiwaangushe wakati wa ziara hiyo. Wakahakikisha anakariri vyema maneno mengi ya kiarabu na kuelewa baadhi ya tamaduni zake.
Baada ya kuhakikisha kila kitu kinaendelea vizuri wakakaa kimya wakisubiri ugeni huo.

Nini kiliendelea hapo? Tukutane siku ya kesho

No comments

Powered by Blogger.